COASCO yawafunda wanachama

  • Watumishi wahamasishwa kujiunga

Na Vicky Kimaro, Dodoma

TUME ya Madini Saccos imepata hati inayoridhisha katika ukaguzi wa Hesabu za Chama zinazoishia Desemba 31, 2023 baada ya kufanyiwa ukaguzi na Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) Tanzania Bara.

Hayo yamesemwa leo Oktoba 18, 2024 na Mwakilishi wa COASCO Amina Kitua, katika Mkutano wa nne wa mwaka wa Madini SACCOS uliofanyika katika ukumbi wa Mkandarasi jijini Dodoma.

Amina amesema, zipo changamoto ndogo za kitendaji zilizoonekana ambazo zimeainishwa na kushauri kufanyiwa kazi kama mkakati wa kuimarisha Tume ya Madini SACCOS.

“Mikopo iliyotolewa ilifuata taratibu zote zinazotakiwa, ndio maana kwenye ukaguzi wetu haujagusa eneo la fedha, ila kuna upungufu uliosababishwa na uchanga wa chama hivyo tumetoa ushauri ili kuimarisha chama,”amesema Amina

Naye Mwenyekiti wa Tume ya Madini SACCOS, Endrewcus Masero amesema Tume ina watumishi 900 kati yao watumishi 426 ndio wanachama wa SACCOS idadi ambayo ni ndogo kwa kuwa lengo ni watumishi wote kujiunga na SACCOS hiyo.

“Katika kipindi cha Januari hadi Septemba 2024 wanachama wapya 53 wamejiunga ikiwa ni sawa na asilimia 26 ya lengo la wanachama wapya 200 tulilokuwa tumejiwekea na hivyo kufikisha idadi ya wanachma 426,”amesema Masero.

Amesisitiza kuwa bado linaendelea zoezi la kuhamasisha wanachama wapya kujiunga na SACCOS kuanzia Tume ya Madini Makao Makuu na Ofisi zote za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa.

Katika hatua nyingine akielezea utendaji wake, Massero amesema SACCOS ya Tume ya Madini imefanikiwa kutoa mikopo ya Shilingi milioni 394 kwa wanachama 86 sawa na asilimia 20.19 ya wanachama wote.