*Arusha yasisimka, mageti yakifungwa mahakamani
*Wananchi wadai mkoa una nuksi ya viongozi vijana
*Wadaiwa kuwaangusha waliowaamini, ni masikitiko
*Uvumi Makonda kukamatwa watawala mitandaoni
ARUSHA
Na Hyasinti Mchau
Kesi ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai ole Sabaya, imeacha gumzo kubwa jijini Arusha, ambapo wananchi walio wengi sasa wameamini kuwa “cheo ni dhamana,” uchunguzi wa JAMHURI umebaini.
Pamoja na baridi inayorindima katika Jiji la Arusha na vitongoji vyake, Polisi jijini hapa wamelazimika kufunga mageti kuzuia mamia kwa maelfu ya wananchi waliojitokeza kushuhudia Sabaya akifikishwa mahakamani.
Wakazi wa Arusha walianza kufika mahakamani mapema asubuhi ya Ijumaa iliyopita kushuhudia historia ikiandikwa kwa Ole Sabaya (34) na wenzake wakisomewa mashitaka sita tofauti.
Hali hiyo inatokea baada ya miaka kadhaa ya tuhuma kuzagaa katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro kuhusu mienendo na vitendo vya kimwamba vya kijana huyo, ambavyo awali vilipuuzwa na wasimamizi wa sheria.
Ole Sabaya anakuwa kiongozi wa kwanza wa serikali kutenguliwa uteuzi wake na Rais Samia Suluhu Hassan, kisha kufikishwa mahakamani kwa tuhuma kadhaa, zikiwamo za unyang’anyi wa kutumia silaha.
Yeye na wenzake watano wamefikishwa mahakamani chini ya ulinzi mkali na baadaye kurejeshwa mahabusu Gereza la Kisongo kutokana na mashitaka yanayowakabili kutokuwa na dhamana.
Mashuhuda wa kesi hiyo walikaa nje ya mahakama kuanzia asubuhi ya Ijumaa iliyopita, huku wakiongezeka kadiri muda ulivyokuwa ukisonga mbele.
Umati ulishangilia kwa nguvu wakati magari yaliyowachukua Sabaya na wenzake yakiondoka kwa kasi mahakamani kuelekea Gereza la Kisongo kumpa Sabaya maisha mapya ambayo hakuwahi kuyawaza.
Wengine wanaoshitakiwa na DC Sabaya ni msaidizi wake binafsi, Sylivester Nyengu a.k.a Kicheche (26), Enock Mnekeni (41), Watson Mwahomange ‘Malyamungu’ (27), John Aweyo ‘Mike One’ na Daniel Mbura wenye umri wa miaka 38 kila mmoja.
Wananchi wazungumza
Akizungumza na JAMHURI baada ya Sabaya na wenzake kufikishwa mahakamani, ofisa mstaafu wa JWTZ mwenye cheo cha ‘Warranty Officer 1’, amesema iwapo mahakama itathibitisha tuhuma dhidi ya Ole Sabaya na genge lake, itakuwa ni aibu si kwake peke yake, bali pia chama kilichomuamini.
“Vijana wamewaangusha waliowaamini na kuwapa madaraka. Hii ni aibu hata kwa chama chake kwa kuwa Mkuu wa Wilaya ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa wilayani kwake.
“Vijana wanapaswa kujifunza kutokana na haya yanayoendelea hata kama bado hayajathibitishwa. Wasibweteke na kujiona wamefika wakati safari bado,” anasema ofisa huyo mstaafu akiomba kutotajwa jina gazetini.
Kauli hiyo inaungwa mkono na aliyekuwa Diwani wa Kata ya Sombetini jijini Arusha, Musa Mkanga, akiwataka wananchi kuwa na subira wakati mahakama ikiendelea na kazi yake.
“Ni kuwa watulivu, hakuhitajiki hasira hata kama kuna watu waliowahi kuumizwa kwa namna yoyote ile,” anasema.
Anasema ni bahati mbaya kwa Mkoa wa Arusha kuwa na viongozi vijana wanaolewa mapema madaraka, akimtaja kiongozi mwingine (jina tunalihifadhi) kama mfano usiofaa kwa vijana.
Kiongozi huyo pia anatajwa katika vijiwe kadhaa jijini Arusha, akihusishwa na ugomvi usio na maana kati yake na Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, wakati akiwa bado Mkuu wa Wilaya ya Longido.
“Hata kabla ya Ole Sabaya kiongozi (huyu) alikuwapo na alikuwa na vituko kweli kweli. Sijui kwa sasa anamtazama vipi Chongolo ambaye amegeuka kuwa bosi wake,” anasema Dennis Mosha, mkazi wa Kwa Morombo, Arusha.
Mmoja wa watu waliowahi kuonja ‘sulubu’ za Ole Sabaya, mfanyabiashara wa mapazia anayemiliki duka la Shaahid Store, Ally Ajarin, anasema:
“Mimi niwashauri vijana wanaopata uongozi kuwa na subira. Sina cha zaidi. Kwa sasa tuiache serikali izungumze.”
JAMHURI limewahi kuandika habari kuhusu kuvamiwa kwa duka la Ajarin ambapo Diwani wa sasa wa Sombetini, Bakari Msangi, alichukuliwa na mabaunsa wa Ole Sabaya. Msangi ni mmoja wa walalamikaji katika moja ya kesi alizosomewa Ole Sabaya.
Katika shauri hilo lenye kuvuta hisia za wengi, Jamhuri inawakilishwa na Mkurugenzi Msaidizi Ofisi ya Taifa ya Mashitaka, Tumaini Kweka, mawakili wa serikali wakuu waandamizi, Abdallah Chavula na Tarsila Gervas.
Mashauri yaliyotajwa mahakamani
Katika shauri la uhujumu uchumi namba 27/2021, Ole Sabaya anakabiliwa na mashitaka manne huku wenzake wanne wakikabiliwa na mashitaka mawili.
Mkurugenzi Msaidizi wa Mashitaka, Kweka, amemweleza Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Martha Mahumbuga, kuwa katika shitaka la kwanza Ole Sabaya anadaiwa kuongoza genge la uhalifu kinyume cha sheria akishirikiana na washitakiwa wengine ambao si watumishi wa umma.
Inadaiwa kuwa Januari 20, mwaka huu katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Arusha, Ole Sabaya akiwa ni ofisa wa umma (Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro), alikiuka majukumu yake ya kiofisi, akishirikiana na Mnikeni, Mwahomange, Aweyo na Nyengu.
“Kwa kujua na kwa malengo ambayo si halali, kwa kutumia mamlaka yake kama ofisa wa umma; mshitaiwa wa kwanza alijipatia manufaa ambayo ni kinyume cha sheria,” anaeleza Kweka mahakamani.
Mashitaka ya pili na tatu yanamkabili Ole Sabaya peke yake, akidaiwa kushiriki matukio ya rushwa, ambapo Januari 20, mwaka huu jijini Arusha, alishiriki vitendo vya rushwa kwa kumshawishi Francis Mrosso ampatie Sh milioni 90, akimuahidi kumsaidia kesi za jinai (ukwepaji kodi) zilizokuwa zikimkabili. Inadaiwa kuwa siku hiyo Ole Sabaya alipokea fedha hizo maeneo ya Kwa Morombo jijini Arusha.
Katika shitaka la nne la utakatishaji fedha linalowakabili washitakiwa wote, Kweka anasema Ole Sabaya akishirikiana na Mnikeni, Mwahomange, Aweyo na Nyengu wanadaiwa kuwa siku hiyo ya Januari 20, mwaka huu maeneo ya Kwa Morombo, walijipatia kiasi hicho cha fedha huku wakifahamu kwamba fedha hizo ni mazao ya uhalifu; ikiwa ni mwendelezo wa kosa la vitendo vya rushwa.
Washitakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwani mahakama hiyo haina mamlaka kisheria kusikiliza shauri hilo, ambapo upande wa Jamhuri uliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa kwa shauri hilo, kwani upelelezi bado haujakamilika.
Unyang’anyi wa kutumia silaha
Kesi nyingine iliyosomwa siku hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Salome Mshasha, wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, ni ya jinai namba 66; kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha.
Watuhumiwa wa kesi hiyo ni Ole Sabaya, Nyengu na Mbura, ambapo Wakili Mkuu Mwandamizi wa Serikali, Tarsila, ameiambia mahakama kuwa Februari 9, mwaka huu, Mtaa wa Bondeni jijini Arusha, washitakiwa hao kwa pamoja waliiba kiasi cha Sh 390,000 mali ya Bakari Msangi ambaye ni Diwani wa Sombetini.
“Baada ya wizi huo, walimfunga pingu, wakampiga makofi, mateke, ngumi na wakatumia silaha aina ya bunduki kumtisha ili wabaki na fedha hizo,” anasema Tarsila.
Shitaka la pili la unyang’anyi wa kutumia silaha lililosomwa na wakili huyo, inadaiwa kuwa Februari 9, mwaka huu katika Mtaa wa Bondeni jijini Arusha watuhumiwa hao waliiba simu aina ya Tecno na fedha, Sh 35,000 mali ya Ramadhani Rashid.
“Baada ya wizi huo walimpiga makofi, ngumi, mateke na wakatumia silaha kumtisha ili waweze kubaki na mali ambazo walimuibia,” anaieleza mahakama Wakili Mkuu Mwandamizi wa Serikali.
Washitakiwa wote watatu wamekana mashitaka ambapo kesi hiyo haina dhamana hivyo wamepelekwa mahabusu, Gereza la Kisongo.
Kesi hiyo inatarajiwa kutajwa tena Juni 18, mwaka huu.
Katika mitandao ya kijamii, sehemu mbalimbali za matukio ya kijamii kama misiba na harusi, bila kuacha nyumba za starehe na baa, jina la Sabaya limegeuka gumzo kubwa, kwani kila mtu anayetenda jambo lolote kinyume cha utaratibu kwa sasa anaitwa Sabaya.
Makonda akamatwa?
Asubuhi ya Jumapili mitandao ya kijamii ilijazwa na taarifa za kukamatwa kwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
Wananchi kadhaa waliozungumzia uwezekano wa Makonda kukamatwa wanadai kuwa suala hilo linawezekana hasa kutokana na ukwasi mkubwa anaodaiwa kuwa nao.
“Sintashangaa kusikia Makonda akihojiwa! Ni tajiri sana. Si rahisi kuwa na fedha kiasi kile kwa mshahara wake,” anasema mkazi mmoja wa Mwanza kwa njia ya simu, akitolea mfano wa jumba la kifahari analomiliki mkoani humo.
Hata hivyo, JAMHURI limewasiliana na watu walio karibu na Makonda kufahamu kilokoni ambao wamesema Makonda hajakamatwa. “Mimi nilikuwa naye leo asubuhi. Ni mzima wa afya. Anasoma mitandao anacheka. Anasema hajawahi kufanya hayo wanayomsingizia na kwamba wanaomwombea mabaya yatawakuta wao wenyewe,” amesema mtu huyo.
JAMHURI limeendelea kumtafuta Makonda bila mafaniko hadi tunakwenda mitamboni.