ARUSHA

Na Hyasinti Mchau

Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai ole Sabaya, amedai mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kwamba alikwenda kwenye duka la Shaahid Store kutekeleza maagizo ‘kutoka juu’.

Akiongozwa na Wakili Mosses Mahuna wakati akitoa utetezi mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Odero Amworo, Sabaya amedai alikwenda kumkamata mmiliki wa duka hilo kwa maelekezo kutoka kwa mkuu wake, wakati huo alikuwa Rais Dk. John Magufuli.

Sabaya anasema Februari 9, mwaka huu alipigiwa simu na ‘mamlaka iliyomteua’ na kupewa maelekezo kwenda Arusha kufanya kazi, na kwamba kuna watu wanne wanamsubiri Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro.

Anadai akiwa na watu hao ambao ndio waliokuwa na taarifa zote, walielekea eneo waliloelekezwa (Shaahid Store) karibu na Soko Kuu la Arusha.

Wakiwa hapo, walimuulizia mwenye duka, Mohamed Saad na kuambiwa kuwa hayupo.

Sabaya ameieleza mahakama kuwa baada ya kumkosa mmiliki, akawasiliana na mamlaka iliyomtuma na kuelezwa kuwa kuna mawasiliano yamefanyika kwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha aliyeelekezwa kuwa watu waliokutwa dukani hapo wapelekwe polisi.

“Ni kawaida kwangu kupata maelekezo kutoka juu kwa mamlaka ya uteuzi, kwani miezi mitatu kabla ya siku ya tukio, nilielekezwa kufanya kazi maalumu na kukamata mitambo ya kutengeneza fedha bandia, Sh milioni 800, jijini Dar es Salaam,” amedai Sabaya.

Amedai kuwa katika ukamataji huo yeye alikuwa msimamizi mkuu, na kwamba hata Gavana wa Benki Kuu na aliyekuwa Waziri wa Fedha wakati huo (sasa Makamu wa Rais), Dk. Philip Mpango, wanafahamu.

Kuhusu wizi wa fedha ndani ya duka hilo na kumpiga Diwani Bakari Msangi, Sabaya  amekana tuhuma hizo, huku pia akiwakana washitakiwa wenzake, Daniel Mbura na Sylvester Nyegu, akidai kuwa hawafahamu.

Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa baada ya mahakama hiyo kumkuta Sabaya na wenzake na kesi ya kujibu.