Uchovu ni kitu cha kawaida katika maisha ya binadamu. Kila mwanadamu hupitia hali hii na hasa baada ya kupitia shughuli mbalimbali ambazo zilitumia nguvu sana ya mwili au hata akili pia.
Ni rahisi sana kuweza kutambua sababu uchovu wa mwili kutokana na shuguli za kila siku.
Lakini je? Vipi kwa upande wa mtu yule ambaye anahisi uchovu uliokithiri tena wa mara kwa mara tofauti na kiasi cha kazi iliyoutumikisha mwili wake au akili yake? Hili ni swali linalowasumbua wengi.
Leo nitaeleza kupitia safu hii sababu kuu za uchovu wa mara kwa mara tena ule uliokithiri ambao wakati mwingine sababu yake haiwezi kutambulika kwa haraka.
Aidha naomba nikukumbushe msomaji kwamba, sababu hizi ndizo zinazosababisha uchovu kwa kiasi kikubwa. Lakini pia wakati mwingingine uchovu husababishwa na matatizo mengine ya kiafya.
Hivyo ni vyema kuwaona watoa huduma wa afya kwa vipimo ikiwa haupo kwenye sababu hizi laki bado unapata uchovu wa mara kwa mara.
Kitu cha kwanza kinachosbabisha uchovu uliokithiri ni kukosa muda wa kutosha wa kupata usingizi. Kiafya unashauriwa kupata muda kadhaa wa kulala na kuweza kupumzisha akili na muda huu hutofautiana kati ya umri na umri ambapo watoto wenye umri wa miaka 0-3 wanatakiwa kulala kwa masaa 14 hadi 17 kwa siku.
Muda huu hupungua taratibu kadri mtu anavyokua na kuongezeka umri ambapo kwa watoto wa umri wa miaka 4-17 kiafya wanatakiwa kulala kwa mud usiopungua masaa 10 lakini wale wa umri wa kuanzia miaka 18 hadi miaka ya kukaribia 60 wanashauriwa kulala kwa muda wa masaa yasiyopungua 8.
Muda huu wa masaa ya kulala pia unaongezeka kadri mtu anavyozeeka kuanzia miaka 60 na kuendelea. Hivyo vi vyema kutambua kiasi cha muda stahiki unaopaswa kulala kulingana na umri wako. Kinyume na hapo tatizo la uchovu wa mara kwa mara linaweza kuwa la kudumu kwako.
Aidha nashauri ni vyema kuacha kutumia vihatarishi vinavyoathiri mfumo wa akili na kusababisha mtu kushindwa kupata usingizi wa kutosha kama vile uvutaji wa sigara, bangi na vitendo vya ulevi kwa ujumla na kuacha unywaji wa vinywaji vyenye caffeine kama vile kahawa na vinywaji vya kiwandani vya kuongeza nguvu.
Mlo pia ni moja ya sababu zinazochangia uchovu. Watu wengi hawajui kama aina ya chakula unachokula pia kinaweza kuwa sababu ya uchovu.
Ndiyo maana inashauriwa kula mlo kamili wakati wote lakini sio mlo kamili tu lakini pia kula kwa wakati na kiasi stahiki cha ulaji. Kutokula kiasi cha kutosha cha chakula kinaweza kumfanya mto kuhisi njaa na kupata uchovu.
Lakini kwa upande wa pili, ulaji wa kupita kiasi sio tu hatari kwa afya lakini pia kunasababisha uchovu na hasa kama mtu akishiba kupita kiasi au kuvimbiwa kama ilivyozoeleka. Na hapa kwenye mlo pia nashauri kunywa maji ya kutosha.
Mwili ukikosa kiwango stahiki cha maji mwili hukosa nguvu na kuwa mchovu. Katika toleo lijalo nitaendelea kukueleza sababu zaidi zilizopo nyuma ya uchovu uliokithiri. Usikose mwendelezo wa makala hii katika toleo lijalo.