Ni hali ambayo mara nyingi mtu huhisi tumbo lake limejaa wakati wote. Kila mmoja amewahi kupata hali hii mara kadhaa kwa nyakati tofauti.
Japo ni hali ambayo kwa kawaida hutokana na ulaji kupita kiasi, lakini kuna baadhi pia hawana tabia ya kula kupita kiasi lakini bado wanakutana na hali hii ya kuhisi matumbo yao yamejaa wakati wote.
Hivyo, ni vema kufahamu kuwa sambamba na tabia za ulaji lakini kuna sababu nyingine zinazochangia hali hiyo, kama vile mwili kuhifadhi kiwango kikubwa cha maji lakini pia inaweza kutokana na matatizo mengine ya kiafya kama vile dalili ya vidonda vya tumbo ambayo huambatana na uwepo wa gesi tumboni.
Uwepo wa vidonda vya tumbo huongeza ujazo wa tumbo na matatizo mengine yanayojitokeza kwenye mfumo wa mmeng’enyo wa chakula.
Zifuatazo ni sababu zinazochangia kwa kiasi kikubwa kujaza tumbo na kusababisha kero kwa walio wengi.
Premenstrual syndrome: Hili ni jina la kitaalamu linalotafsiri baadhi ya matatizo ya kiafya madogo madogo kama vile uchovu, maumivu na hata kichefuchefu yanayojitokeza kwa mwanamke wakati akikaribia kuingia kwenye mzunguko wa hedhi.
Premenstrual syndrome pia inasababisha mwili kuhifadhi kiwango kikubwa cha maji kutokana na mabadiliko ya mfumo wa homoni kwa wakati huo. Hivyo, ndani ya kipindi hicho ni kawaida kwa mwanamke kuhisi tumbo lake limejaa.
Ulaji wa chumvi kwa wingi ni moja ya sababu zinazochangia tumbo kujaa. Ni dhahiri kwamba mwili unahitaji chumvi, lakini mara nyingi tumejikuta tukitumia zaidi kiwango stahiki kinachostahili kuingia mwilini.
Chumvi ikizidi mwilini inaupa mfumo wa mwili kuhifadhi kiwango kikubwa cha maji na chumvi pia inaweza kusababisha matatizo mengine makubwa ya kiafya kama vile shinikizo la juu la damu.
Kwa siku za karibuni matumizi ya vyakula vilivyosindikwa yameongezeka maradufu, na ni muhimu kuzingatia kuwa asilimia kubwa ya vyakula vilivyosindikwa vimewekwa kiasi kikubwa cha chumvi na hata kama usipohisi ladha ya chumvi kwenye vyakula hivyo haina maana kuwa havijawekewa chumvi.
Hivyo ni vema kusoma kwa umakini vibandiko vilivyowekwa kwenye vyakula hivi ili kujua kiasi cha ‘sodium’ kilichomo kwenye vyakula husika.
Unywaji wa soda na vinywaji vingine vya kiwandani pia unachangia sana kulifanya tumbo muda wote liwe limejaa. Soda na vinywaji vingine kama vile bia, shampeni au vinywaji vinavyotumika kuongeza sukari ya mwili vimewekewa kiasi fulani cha gesi katika utengenezaji wake.
Unapokunywa moja ya vinywaji hivi vinaenda kuongeza ujazo kwenye mfumo wako wa chakula. Wakati ukiendelea kunywa, unaweza kutoa kiasi kidogo cha gesi, wengi wamezoea kuita kubeua.
Hii inatokea pale unapokunywa kinywaji chenye gesi na ghafla inakujia hali kama unacheua hivi, lakini kinachotoka ni gesi. Hii haimaanishi kuwa kwa kufanya hivyo gesi yote uliyoipata kutoka kwenye kile kinywaji imetoka, hapana.
Kiasi kikubwa cha gesi hiyo huendelea kubaki kwenye utumbo wa chakula na inaendelea kubaki ndani ya utumbo hadi hapo itakapotoka taratibu, aidha kwa njia ya mdomo au kwa njia ya haja kubwa.
Ikumbukwe kuwa karibu soda zote zimewekewa sukari kwa wingi sana na huenda kiwango cha sukari kilichomo kwenye soda kikazidi kiwango kinachostahili kuingia mwilini, hivyo sukari hii inapoingia mwilini inaulazimisha mwili kuhifadhi kiwango kikubwa cha maji kwenye mfumo wa chakula na kibaya zaidi unajiweka kwenye hatari kubwa ya kupata magonjwa ya kisukari.
Tafadhali zingatia kuwa si baadhi tu ya soda, bali soda karibu aina zote zinaweza kukuletea madhara haya.