Licha ya dunia kuwa na jumuiya nyingi za kisiasa na kiuchumi, Umoja wa Ulaya (EU) ni kati ya jumuiya za kisiasa na kiuchumi zilizofanikiwa kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na jumuia nyingine duniani.
Ni jumuiya inayounganisha watu zaidi ya milioni 500 kutoka mataifa wanachama ishirini na nane huku pato la jumuiya likitajwa kufikia dola trilioni 18.45.
Umoja wa Ulaya (EU) ndiyo jumuiya yenye nchi nyingi tajiri zaidi duniani, huku mafanikio yake kiuchumi yakitajwa kuchangiwa na mapinduzi ya viwanda miaka mingi iliyopita, lakini kwa sasa sekta ya huduma ndiyo sekta iliyo mhimili wa uchumi kwa nchi nyingi za jumuia hiyo hasa huduma za kifedha kutoka mataifa makubwa ya umoja huo kama Ufaransa, Uingereza, Ujerumani na Italia.
Licha ya kupoteza nguvu ya ushindani wa kiviwanda kwa Bara la Asia hasa kwa nchi kama China, Indonesia, na sasa Vietnam na Bangladesh, Umoja wa Ulaya umeendelea kuwa moja ya mihimili mikubwa kwa uchumi wa dunia, huku mataifa yake yakiendelea kuwa kati ya nchi muhimu kwa maendeleo ya sayansi, teknolojia na utafiti kwa nyanja mbalimbali, jambo linaloendelea kuwaweka kwenye ramani ya uchumi wa dunia.
Italia ni moja ya nchi muhimu sana kwa uchumi wa bara la Ulaya na hata dunia. Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) za mwaka 2014, Italia ndiyo nchi ya tisa duniani kwa kuwa uchumi mkubwa duniani, huku sekta ya huduma ikiwa ndiyo mhimili mkuu wa uchumi wa nchi hiyo kwa kuchangia asilimia 73 na sekta ya viwanda ikiwa na mchango wa asilimia 25 na kiasi kilichobaki kikiwakilisha mchango wa sekta ya kilimo.
Licha ya kuwa na utajiri huo, Italia kama yalivyo mataifa mengine makubwa ndani ya umoja huo, imeelemewa na mzigo mzito wa madeni.
Aprili mwaka huu, deni la taifa la nchi hiyo lilitajwa kufikia asilimia 135 ya pato lake la taifa. Kwa lugha nyingine ni kwamba, deni la taifa la Italia kwa sasa ni zaidi ya pato lake la taifa linalofikia dola trilioni 2.17 huku kukiwa na matumaini ya ukuaji wa uchumi kwa asilimia 0.6 na mfumuko wa bei wa asilimia 0.7 kupungua kwa uwiano wa deni kwa pato la taifa la nchi hiyo kunakotarajiwa kuanzia mwaka 2015 kunahitaji ukuaji mkubwa zaidi wa uchumi kuliko ilivyo sasa. Mfumuko wa bei wa wastani pamoja na bajeti yenye ziada ambayo imekuwa historia ya nchi ya Italia kwa kipindi kirefu.
Italia inatajwa kuwa kwenye mdororo wa uchumi kwa mwaka wa sita sasa tangu kutokea mtikisiko wa uchumi wa dunia mwaka 2008, ulioziumiza zaidi nchi tajiri ulimwenguni na kusababisha kufilisika kwa kampuni kubwa kama Lehmann Brothers, Conseco, Enron, MF Global, Citigroup na Shirika la Ndege la Amerika.
Italia imekuwa nyuma kiteknolojia ikilinganishwa na nchi nyingine kubwa kama Ufaransa, Ujerumani na Uingereza huku pia idadi ya wazee ikiongezeka kwa miongo kadhaa iliyopita.
Italia imeshindwa kuendana na mabadiliko ya kasi ya teknolojia yaliyopo hivi sasa, jambo linaloifanya kushindwa kukidhi viwango vya kiushindani kwenye uchumi wa dunia ikilinganishwa na mataifa mengine yanayoinukia kwa kasi kama China, na nchi nyingine zilizoendelea.
Kuendelea kuwa nyuma kiteknolojia kumeoneshwa na kushuka kwa ubora wa elimu nchini humo, ukuaji mdogo wa uchumi na uwekezaji mdogo katika teknolojia na rasilimali watu.
Kuongezeka kwa idadi ya wazee kumeendelea pia kusababisha uwekezaji katika maeneo hayo upungue.
Pengo la uvumbuzi kati ya Italia na nchi nyingine ni jambo jingine linaloendelea kuiumiza Italia kiuchumi.
Kwa kuangalia nchi ya Marekani, ambapo vigezo vya juu zaidi vya ushindani wa kiteknolojia hutumika kupima ushindani duniani inaonesha kwamba pamoja na kusuasua, Sweden imeonekana kuwa mbele kiuvumbuzi kuliko nchi za Italia na Ufaransa hasa katika umilikaji wa hatimiliki. Umilikaji wa hatimiliki kwa wingi zaidi kwa nchi ya Sweden unachangiwa zaidi na uwekezaji katika utafiti.
Sweden hutumia kati ya asilimia 3.5 na 3.8 ya pato lake la taifa kwa ajili ya utafiti, wakati Italia hutumia kati ya asilimia 1 na 1.3 ya pato lake la taifa na nchi ya Ufaransa ikitumia asilimia 2.25 ya pato lake la taifa katika utafiti.
Kupungua kwa idadi ya vijana nchini Italia ambao ndiyo injini kuu ya kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia kwa nchi yoyote duniani, huku vijana wengi wakikabiliwa na tatizo la ajira nchini humo hasa kwa kundi lenye umri kati ya miaka 15 na 25 huku idadi ikifikia asilimia 33 kwa mwaka 1999 na mwaka 2014 ikikadiriwa kufikia asilimia 42.
Mwaka 2013, idadi ya watu wasio na ajira za kudumu chini ya miaka 25 imefikia asilimia 46.8. Uwekezaji unaoendelea kufanywa na Sweden katika utafiti umeifanya Sweden kutumia teknolojia ya juu katika uzalishaji tangu miaka ya 1990.
Uwekezaji wa Italia katika utafiti ni mdogo sekta kwa sekta nchini humo. Uvumbuzi kwa Sweden huchangiwa kwa kiasi kikubwa na uwekezaji kwenye utafiti, biashara na ujasiriamali pamoja na matumizi makubwa ya tafiti mbalimbali katika sekta zote za uchumi nchini humo.
Hata hivyo, nguvu ya kiuvumbuzi ya Sweden imetokana na uwekezaji wa muda mrefu katika elimu nchini humo.
Hali ni tofauti kwa Italia ambayo inaonekana dhahiri kwamba moja ya vyanzo vya matatizo ya uchumi wa Italia ni sekta yake ya elimu. Kwa mujibu wa takwimu za maendeleo ya watu (HDI) ubora wa rasilimali watu inayozalishwa Sweden uko juu zaidi ya ile ya Italia.
Hii inaonekana kwenye uwiano wa miaka ya masomo na matunda ya elimu wanayopata watu ambayo haifanani na mafanikio ya uchumi wa nchi hiyo, kigezo ambacho hata hapa kwetu Tanzania kinajidhihirisha. Idadi ya wasomi inaendelea kuongezeka kila kukicha hapa Tanzania lakini ongezeko hilo haliendani na hatua tunazopiga kama taifa kiuchumi.
Ili nchi ipige hatua za kweli kiuchumi, ni lazima uwepo uhusiano chanya kati ya elimu inayotolewa na matunda ya elimu hiyo pale inapotumika katika kada mbalimbali.
Ndiyo maana nchi nyingi zilizoendelea “hazitaki mzaha” kwenye suala la elimu. Kama elimu inayotolewa haichangii maendeleo ya eneo mahali huska, maendeleo yatakuwa ndoto. Hii ni kati ya sababu kubwa zinazoifanya Italia iwe hapo ilipo leo hii.
Takwimu zinaonesha uwekezaji katika sekta ya elimu nchini Italia ni mdogo ikilinganishwa na Sweden na Ufaransa. Mwaka 2011, Sweden iliwekeza asilimia 6.82 ya pato lake la taifa katika elimu huku Ufaransa ikiwekeza asilimia 5.68 wakati Italia ikiwekeza asilimia 4.29 tu ya pato lake la taifa.
Siyo Waitaliano tu ndiyo wanaowekeza kiasi kidogo katika elimu kwa sababu ya matunda machache wanayopata, Serikali ya Italia pia inaona uwekezaji huo una matunda machache hivyo fedha huwekezwa sehemu nyingine.
Utafiti uliofanywa na Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD) mwaka 2012 ulibaini kwamba watoto wa wazazi wengi walio na elimu ndogo, watoto wao pia hukutwa kwenye mazingira mabovu kielimu.
Matunda machache yanayopatikana kutokana na uwekezaji mdogo kielimu, hutoa fursa ndogo sana kwa ukuaji mkubwa wa kiuchumi hasa kwa kipindi hiki ambacho Italia ina mzigo wa madeni, jambo linaloashiria kuendelea kuongezeka kwa idadi ya watu wasio na ajira na kuendelea kuizamisha Italia katika kada za ushindani wa kiuchumi na kibiashara duniani.
Nimalizie tu kwa kusema kwamba Italia ya sasa inahitaji mapinduzi makubwa katika sekta ya elimu. Sekta hii ndiyo mhimili mkuu wa ushindani wa nchi yoyote duniani. Uwekezaji huo ni lazima ufanywe hasa katika utafiti kwenye sayansi na teknolojia pamoja na matumizi ya tafiti zinazofanywa sehemu mbalimbali duniani na zinazogusa sekta zake zote za uchumi.
Ni kwa uwekezaji huu ndipo watarejea kwenye ramani za uvumbuzi duniani. Na uvumbuzi ndiyo msingi mkuu wa elimu bora, maendeleo thabiti, na uchumi imara. Hakuna uvumbuzi unaotokea popote pale bila kuwekeza kwenye sekta ya elimu.
Ni lazima pia waziangalie sheria zao za uhamiaji. Kwa sasa hawana jinsi zaidi ya kuruhusu wahamiaji ambao watakuwa nguvukazi katika nchi hiyo, ambayo inatajwa kuwa na ongezeko la wazee huku idadi ya watoto wanaozaliwa ikipungua ikilinganishwa na miaka ya nyuma. Kama Italia inahitaji mapinduzi ya kweli kimaendeleo ianze kufanya mabadiliko sasa.
Mwandishi wa makala hii anapatikana kupitia namba 0763643199
Email: [email protected]