Mkoa wa Ruvuma umeweza kukusanya mapato kwa asilimia 110.8 katika mwaka 2021/2022. 

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amesema katika kipindi hicho Halmashauri zote nane zimeweza kukusanya mapato ya zaidi ya shilingi bilioni 21 kati ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 19.33.  

“Nitumie fursa hii kuwapongeza wakurugenzi kwa kusimamia vizuri ukusanyaji mapato,nawakumbusha wakurugenzi suala zima la kusimamia mapato na ushuru kwani fedha hizo ndizo zinatumika katika kujenga miradi mbalimbali ya maendeleo “, amesema.

Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA kwa kuweza kukusanya mapato kwa zaidi ya shilingi bilioni 19 kwa mwaka wa fedha 2021/2022 sawa na asilimia 101.52.

Hata hivyo amesema Mkoa wa Ruvuma unaendelea kuimarika kiuchumi kwa kuimarisha miundombinu,shughuli za uzalishaji Mali,biashara,uwekezaji na shughuli za uchimbaji madini hasa madini ya makaa ya mawe. Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Mkoa wa Ruvuma.