Ruvu Shooting imeilazimisha Yanga sare ya mabao 2-2 kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam
Yanga walikuwa wa kwanza kujipatia bao katika dakika ya 19 ya mchezo kupitia kwa Matheo Anthony kabla ya Ruvu Shooting kusawazisha ikiwa ni dakika ya 30 kupitia kwa Khamis Mcha kwa njia ya penati baada ya beki Abdallah Shaibu ‘Ninja’ kuushika mpira eneo la hatari.
Wakati ubao ukiwa unasomeka 1-1, Yanga waliweza kuongeza bao lingine la pili dakika ya 39 kupitia kwa Maka Edward aliyepiga shuti kali na kumshinda kipa wa Ruvu Shooting, Abdallah Rashid.
Dakika 45 zilimazilika Yanga wakiondoka kifua mbele kwa mabao mawili na Ruvu Shooting wakiwa na moja.
Kipindi cha pili kilipoanza ilichukua takribani dakika moja tu ambapo Issa Kanduru aliifungia Ruvu bao la pili na kuweza kubadilisha ubao wa matokeo kuwa 2-2. Mpaka dakika 90 zinamalizika, Yanga 2, Ruvu 2.
Matokeo hayo ya sare kwa Yanga yanairahisishia Azam FC kujitengenezea mazingira mazuri ya kumaliza ligi ikiwa nafasi ya pili, ambapo endapo Yanga ingeshinda leo ingehitaji sare pekee dhidi ya Azam ili iweze kuishusha Azam kwenye nafasi hiyo.
Kwa namna msimamo wa ligi ulivyo, sasa Azam inahitaji sare tu katika mechi ijayo dhidi ya Yanga ili iweze kumaliza ligi ikiwa nafasi ya pili wakati Yanga inapaswa kushinda ili kukalia nafasi hiyo pia.
Yanga imefikisha pointi 52 huku Azam ikiwa ina 55, hivyo Yanga ikishinda itakuwa ina alama 55, alama ambazo itaiwezesha kuchukua nafasi ya pili kutokana na utofauti wa mabao ya kufunga na kufungwa.