Kenya inashusha pumzi baada ya Mswada wa Fedha wa 2024 uliozua utata kutupiliwa mbali. Rais William Ruto hatimae ametangaza kusikiliza kilio cha wakenya walioupinga mswada huo kwa nguvu zote.
Akilihutubia taifa kwa mara ya pili tangu maandamano kulitikisa taifa kwa saa kadhaa zilizopita, rais William Ruto alisisitiza kuwa amesikiliza kilio cha wakenya na kwamba wao ndio muhimu.
Rais Ruto pia ametangaza hatua za kubana matumizi ili kuweza kumudu mahitaji ya Serikali na taifa kwa jumla. Ruto aliyebadili kauli na kuwa mpole, alitoa pia rambirambi kwa jamaa za waandamanaji waliopoteza maisha kwenye purukushani za hapo jana.
Kiongozi wa taifa alisisitiza kuwa bado azma ya kufanya majadiliano na vijana iko palepale kwani anajali maslahi yao. Kauli hizo zinaungwa mkono na Askofu Dr Charles Marita ambaye ni mwenyekiti wa baraza la maaskofu tawi la Nakuru.
Ifahamike kuwa bunge la taifa lilianza likizo hii leo hadi wiki ya mwisho ya mwezi ujao wa Julai. Yote hayo yakiendelea, vikosi vya jeshi la taifa vinaendelea kupiga doria kwenye ikulu na sehemu muhimu za serikali katika miji mikuu ya Nairobi, Mombasa, Kisumu na Nakuru.
Tayari chama cha mawakili nchini Kenya, LSK kimeanzisha mahakamani mchakato wa kushinikiza jeshi hilo kuondoka mitaani. Mchakato ambao utaanza rasmi kesho Alhamisi. Jeshi limekuwalikipiga doria tangu usiku wa kuamkia leo.