RAIS wa Kenya William Ruto amekiri ukiukaji uliofanywa na vikosi vya usalama vya nchi hiyo, kufuatia maandamano ya kupinga wimbi la hivi majuzi la madai ya utekaji nyara ambayo yamezua ghadhabu nchini humo.

Ruto amesema kwenye hotuba yake ya mwaka mpya kuwa kumekuwepo na matukio ya matumizi ya nguvu kupita kiasi na ya kinyume cha sheria yaliyofanywa na polisi. Hata hivyo hakufafanua ni vitendo vya aina gani.

Kiongozi huyo amesema kuwa ni muhimu kukumbuka kwamba kila uhuru una ukomo, na usalama wa umma na utaratibu wa sheria lazima vizingatiwe kwanza kabla ya uhuru wa mtu yeyote.

Vikosi vya usalama vya Kenya vinatuhumiwa kwa kuwashikilia watu kadhaa kinyume cha sheria tangu maandamano ya kuipinga serikali yaliyoongozwa na vijana mwezi Juni na Julai yalipokandamizwa vikali.