“Rushwa ni wizi wa fedha za umma”. Hivyo ndivyo Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania na kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki, Roeland van de Geer, anavyotaka Watanzania waielewe rushwa.
Rushwa, kwa mujibu wa Balozi Geer, ni chanzo kikubwa cha ukiukwaji wa haki za binadamu, kushamiri kwa umaskini pamoja na ukosefu wa maendeleo hasa kwenye maeneo ya Serikali za Mitaa wanakoishi watu wengi zaidi.
Pamoja na kutambuliwa kama serikali za watu, kutokana na kugusa moja kwa moja maisha ya kila siku ya wananchi, utendaji wa Serikali za Mitaa nchini Tanzania umegubikwa na dosari lukuki huku rushwa ikiwekwa juu kabisa ya dosari hizo.
Tume ya Jaji Warioba iliibua kuwa kwenye Serikali za Mitaa rushwa imeshamiri wakati wa kuajiri watumishi au kuwapandisha vyeo, utoaji wa leseni za biashara au kuidhinisha kuendesha biashara katika maeneo yasiyoruhusiwa kisheria.
Tume ikabaini pia kwamba madiwani na wajumbe wa Mabaraza ya Usuluhishi kwenye Kata walikuwa wakidai rushwa ili kupendelea katika uamuzi, ilhali katika Halmashauri za Miji rushwa ilikuwa imeshamiri katika ugawaji wa zabuni, ugawaji wa viwanja na meza za biashara kwenye masoko.
Ni dhahiri kushamiri kwa rushwa kunafifisha matakwa ya Katiba inayovielekeza vyombo vya Serikali vyote, kuelekeza sera na shughuli zake zote katika kuhakikisha kwamba utu na haki zote za binadamu zinalindwa, kuheshimiwa na kuthaminiwa.
Hali kadhalika, kuhakikisha kwamba aina zote za dhuluma, vitisho, rushwa, uonevu na upendeleo zinaondolewa na kwamba matumizi ya utajiri wa Taifa yanatilia mkazo maendeleo ya wananchi na mno zaidi; katika kuondosha umaskini, ujinga na maradhi.
Moja ya sababu ya kushamiri kwa rushwa kwenye Serikali za Mitaa ni unyonge wa wananchi, hususan silika yao ya kukaa kimya badala ya kupaza sauti na kuchukua hatua.
Lakini sasa silika hiyo itaanza kubadilika kutokana na uwepo wa mradi wa kuwajengea wananchi uwezo wa kuzuia na kutokomeza rushwa kwenye Serikali za Mitaa unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU).
Ukiwa umepewa jina la “Tuungane Kutetea Haki Zetu”, mradi umelenga kuunganisha nguvu za wadau wa Serikali za Mitaa – Wananchi, Vyombo vya Habari, Mashirika ya Hiari, Madiwani na Watendaji kufanya kazi pamoja katika kuongeza nguvu katika kuzuia na kupambana na rushwa.
Mradi huo unaendeshwa katika mikoa saba ikihusisha wilaya 40 zenye kata 1,055 zinazokaliwa na watu takriban milioni 11; idadi ambayo ni sawa na asilimia 25 ya Watanzania wote.
Meneja wa Mradi huo, Maria Kayombo, anasema kuwa mashirika matatu ya hiari- Konrad Adenauer Stiftung (KAS), Chama cha Walimu wa Somo la Uraia Tanzania (CETA) na Action for Democracy and Local Government (ADLG) – yameunganisha nguvu kuendesha mradi kwa Ufadhili wa Sh bilioni 2.5 kutoka EU.
Kwa mujibu wa Kayombo, mradi unaendeshwa kwenye mikoa mitatu ya Kanda ya Kusini Mashariki – Lindi, Pwani na Ruvuma na katika mikoa mingine minne ya Kanda ya Ziwa – Geita, Kagera, Simiyu na Mara.
Lengo kuu la mradi ni kupunguza hulka ya rushwa miongoni mwa watendaji wa Serikali za Mitaa kwa kujenga ukaribu wa kiutendaji kati ya Mashirika ya Hiari, mamlaka za Serikali za Mitaa na Wananchi na hivyo kuwa na mfumo wa kisiasa ulio wazi na wa uwajibikaji.
Sauti moja yenye lengo la kuhimiza uwazi na uwajibikaji kwenye rasilimali za umma italeta uelewa mpana kwa wananchi na ushiriki wao kwenye maendeleo, hivyo kuwa chachu ya mabadiliko kwenye jamii zao.
Mashirika ya Hiari ni kiungo muhimu kati ya Serikali za Mitaa na wananchi kutokana na kusheheni wataalamu katika fani mbalimbali wenye ujuzi wa kusukuma mabadiliko ya kijamii. Hali kadhalika, Mashirika ya Hiari yanayo nafasi kubwa katika kushawishi mabadiliko ya tabia, mwenendo na mtazamo wa kijamii kuhusu rushwa pamoja na kupanua uelewa na weledi wa jinsi ya kuitokomeza.
Hii ndiyo maana mradi umejielekeza kwenye ujenzi wa daraja la uhusiano baina ya Mashirika ya Hiari, Wananchi na mamlaka katika Serikali za Mitaa, ambazo kwa kuimarishwa zitaweza kutekeleza wajibu wao kwa kuwajibika kwa uwazi.
Jumla ya Mashirika ya Hiari 25 yanaendeshwa katika ngazi za wilaya katika mikoa hiyo saba. Vile vile madiwani 80 wa kuchaguliwa na watendaji kutoka wilaya 40 katika halmashauri za mikoa hiyo ya mradi watanufaika na mradi bila kusahau wananchi katika kata 1,055 za mikoa iliyomo kwenye mradi.
Zaidi ya hapo, inatarajiwa kuwa mwishoni mwa mradi hapo mwaka 2019, Mashirika ya Hiari kama vile lile la Human Rights Frontiers Coalition Against Corruption (HRFCA) la mkoani Ruvuma, yatakuwa yameimarika kuweza kufuatilia mapato na matumizi ya rasilimali za umma.
Kwa Upande mwingine, wananchi katika maeneo ya mradi watakuwa wamejengewa uelewa na ufahamu wa kutosha wa kutetea rasilimali za umma na hasa uamuzi wa jinsi ya kuzitumia rasilimali hizo.
Kwa upande wake, Serikali za Mitaa zitakuwa zimeimarishwa kwa kujengewa uwezo wa kushirikiana na Mashirika ya Hiari kwa minajili ya kuelekeza mapato ya rasilimali za umma kwenye maeneo yenye manufaa kwa ustawi wa watu.
Matarajio ya mradi ni kwamba Mashirika ya Hiari yatawawezesha wananchi kufuatilia matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo na huduma za kijamii baada kujengewa uwezo na kushirikishwa katika uamuzi unaohusu fedha za umma.
Hali kadhalika, Serikali za Mitaa zitakuwa zimeimarishwa kwa kujengewa uwezo na kuimarisha uhusiano wake na Mashirika ya Hiari ili kuboresha uwazi na uwajibikaji katika mapato na matumizi ya fedha za umma katika ngazi zote.
Uteuzi wa wilaya hizo ulizingatia ukweli kwamba hizi ni wilaya zilizoko pembezoni kimaendeleo na kwa sababu ya kukosa sauti, wananchi wanapuuzwa na viongozi au watendaji wala rushwa.
Kupitia Mashirika ya Hiari inatarajiwa wananchi watakuwa na uwezo wa kupaza sauti badala ya kukaa kimya pasipo kuchukua hatua. Hii ndiyo maana vyombo vya habari vilivyoko kwenye maeneo ya mradi vimeshirikishwa ili wananchi waweze kusikika sauti zao juu ya masuala yanayowakera hasa rushwa na kutowajibika miongoni mwa watumishi wa umma.
Sauti ya watu ni sauti ya Mungu. Inatarajiwa kwamba sauti ya wananchi itachangia kupunguza na kutokomeza rushwa na kujenga tabia ya uwazi na uwajibikaji. Hii ndiyo maana Balozi Geer, anataka wananchi waelewa kuwa rushwa ni wizi na chanjo yake siku zote ni uwazi!
Balozi Geer anataka wananchi watambue kuwa rushwa inachangia kwa kiasi uvunjaji wa haki za binadamu, kukoleza umaskini na kudumaza maendeleo. Ifike mahala, mwananchi asifikirie kwamba anaweza tu kushinda au kupata haki mahakamani kwa kutoa rushwa. Ni vema taasisi hizi za umma zikafanya kazi kwa usawa kwa kila mtu, anasema.
Juhudi kuwa inaelekezwa kuwajengea uwezo wananchi wa kuelewa haki zao. Uelewa wao ni muhimu ili waweze kudai badala ya kukaa kimya. Uelewa wao pia utawasaidia katika kutafsiri kama kiasi kilichofikishwa huko ni sahihi au kimemegwa na kupelekwa kusikohusika.
Kwa kutumia vyombo vya habari katika maeneo yao, inatarajiwa mwishoni mwa mradi wananchi watakuwa na sauti siyo tu ya kulalamika, lakini mno zaidi kujengwa katika kufanya uamuzi wa aina ya viongozi /wawakilishi wanaowataka kiuwezo na kimaadili.
Kiwango cha elimu kwa madiwani – kujua kusoma na kuandika tu – kimelalamikiwa sana Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuwa ni kikwazo katika kusimamia mapato na matumizi ya fedha za umma kwenye Serikali za Mitaa.
Ndiyo maana Richard Shaba wa Konrad Adenauer Stiftung, anasema kupitia mradi huu, wananchi wataweza kupata uelewa na ujuzi wa kupima uwezo wa watu kabla ya kuwachagua katika nafasi za uongozi badala ya kuwachangua kama wasindikizaji.