Wabunge wakithiri ulaji rushwa
Duru za uchunguzi zinaonyesha kuwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa inakabiliwa na tuhuma nyingi na nzito za ulaji rushwa. Matukio ya ulaji rushwa yameripotiwa kutokea kila wakati ambao Kamati hiyo inapokuwa kwenye ukaguzi wa hesabu.

Mmoja wa wakurugenzi aliyezungumza kwa masharti ya kutotajwa jina alisema, “Tunaombwa pesa sana. Wabunge si kwamba wanashawishiwa, bali wanadai rushwa kwa nguvu. Halmashauri zote zinachanga fedha za kuwapa.”

Anatoa mfano kwamba hata Halmashauri za Jiji la Dar es Salaam hivi karibuni zilichanga Sh milioni 25 wakahongwa baadhi ya wabunge ambao ni wajumbe wa Kamati hiyo, inayoongozwa na Mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema (TLP).

Chanzo cha habari kinasema kwamba fedha zinazochotwa ni zile za miradi ya zahanati, madarasa, afya, maji na mingine ya kijamii.

“Mkurugenzi analazimika kutoa fedha za miradi, anatoa kwa kuwa wabunge wanapokwenda kukagua na kukuta upungufu, hawahoji. Wanajua upungufu uliopo umetokana na fedha walizopewa. Nakuhakikishia kuwa miradi mingi inakwama kwa sababu kuna fedha zinazoliwa na watumishi wa halmashauri na sasa wajumbe wa Kamati za Bunge,” amesema.

Wakati Serikali ikijiandaa kusoma bajeti yake ya mwaka 2012/2013 bungeni keshokutwa, imebainika kuwa halmashauri nyingi zimepokea fedha za maendeleo kati ya asilimia 24 na 30. Pamoja na uchache huo, bado wabunge wasio waadilifu wanachotewa.