*‘Wajanja’ walamba Sh milioni 400 kwa siku ‘kwa kazi maalumu’

DAR ES SALAAM


Na Mwandishi Wetu

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi maofisa wa ngazi za juu wa Wizara ya Fedha na Mipango wakikabiliwa na tuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma, ikiwamo kujilipa zaidi ya Sh milioni 400 kwa siku moja.

Hali hii inatokea wakati taifa likiwa bado linasubiri taarifa ya ukaguzi wa Hazina kufikishwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Mapema wakati wa siku za mwanzo za utawala wake, Rais Samia aliagiza ukaguzi ufanyike Benki Kuu na Hazina kuangalia mafungu yaliyotolewa kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu, kauli iliyochukuliwa na wengi kuwa kuna harufu ya ufisadi ndani ya taasisi hizo nyeti.

Miongoni mwa maofisa waliosimamishwa kazi ni Mkaguzi Mkuu, Mkaguzi Msaidizi na baadhi ya watendaji wa wizara hiyo, ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za umma zinazowakabili.

Majaliwa ameonekana kushangazwa na namna maofisa hao walivyokuwa wakijilipa mamilioni ya fedha kwa kazi za ndani ya wizara na wakati mwingine kwa siku moja tu.

“Dosari hizi tumeanza kuziona mwezi wa tatu. Machi 31, mwaka huu ambapo kupitia Vocha namba 2430 ililipa Sh milioni 251.5 kwa kazi maalumu.

“Kazi maalumu na hao waliofanya kazi yenyewe wala hawaonekani,” anasema Majaliwa akionekana kuchukizwa na ubadhirifu huo ndani ya wizara nyeti kama hiyo.

Amemtaka Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Salum Hamdun, kufanya uchunguzi wa tuhuma hizo.

“Tunahitaji uchunguzi wa haraka. Matumizi ya mafungu mbalimbali. Fedha zinahama hapa kwenda Hazina Ndogo zina shida kubwa. Malipo haya yatafanyika kwa utaratibu huu kwa muda gani? Kama siku moja zinaweza kutoka Sh milioni 400. Siku mbili, wiki, mwezi itakuwaje? Tutabaki na fedha za kujenga zahanati kweli? Hatuwezi.” anahoji Majaliwa.

Waziri Mkuu anahoji ni kazi gani maalumu ya kujilipa hadi Sh milioni 251 kwa siku, akitaka kujua ni kazi gani watu wa Hazina walizonazo nje ya zile za kawaida hata kujilipa fedha zote hizo.

“Siku hiyo hiyo, Machi 31; kupitia vocha namba 2433 mlijilipa Sh milioni 198.8 kwa madai kuwa ni honoraria. Hebu zijumlishe fedha hizi jumla ni shilingi ngapi.

“Siku moja zidisha mara siku mnazokaa hapa. Siku tatu baadaye zimetumika Sh milioni 146 kwa ajili ya kuandika mpango kazi wa manunuzi! Hii ni sehemu ya kazi yenu, kama si kazi yenu ni nani aliileta hapa?” anasema na kuhoji.

Miongoni mwa maofisa waliotajwa na Majaliwa ni Judicate Urassa, Afia Ndyamukama, Tobesi Matiku, Dennis Kanza, Alikye Mwakitekele, Frederick Bush, Tumaini Mwakalange na Idelfonce Masoud.

Majaliwa amemtaka Kamanda wa TAKUKURU iwapo atakuta kweli kumefanyika unadhirifu huo kuwachukulia hatua kali za kisheria wote waliohusika.

Katika ubadhirifu huo, amesema Aprili 8, mwaka huu watumushi 27 wa Hazina walilipwa Sh milioni 44.5 zikiwa ni posho ya ‘kazi maalumu’ iliyofanyika kwa muda wa wiki nne. 

Aprili 13, mwaka huu kiasi kingine cha fedha, Sh milioni 155.2 kililipwa kwa watumishi 68 ambao nao walipewa posho ‘ya kazi maalumu’ iliyodumu kwa wiki tatu na Majaliwa anashangaa ni kikokotoo gani kinachotumika kufanya malipo na kutofautisha kazi ya wiki nne na wiki tatu.

Mlolongo wa ufujaji wa fedha ndani ya Wizara ya Fedha na Mipango unaendelea kubainisha kuwa Aprili 30, mwaka huu zililipwa Sh milioni 43.9 kwa ajili ya kuandaa mpango wa kuhifadhi mazingira.

“Na siku hiyo hiyo zikalipwa Sh milioni 14.4 kwa ajili ya Siku ya Wanawake. Fedha nyingine, Sh milioni 43 zililipwa siku hiyo na kufanya jumla ya malipo yaliyolipwa ndani ya siku hiyo moja kuwa ni Sh milioni 101.8.

“Tuna sherehe ngapi (kwa mwaka)? Je, watumishi wote wanaokwenda kwenye sherehe tukiamua kuwalipa? Tutajenga vituo vya afya?” anasema.

Kana kwamba haitoshi, asubuhi ya Mei Mosi mwaka huu (siku ya mapumziko) kulifanyika malipo ya Sh milioni 184.1 na mchana wa siku hiyo hiyo zikalipwa Sh milioni 264 kwa ajili ya ‘kazi maalumu’. 

“Yaani sisi tukiwa Mwanza tunasherehekea Siku ya Wafanyakazi Duniani, nyinyi hapa ndani mnalipana posho!” anasema kwa uchungu.

Anasema malipo ya Sh milioni 146.5 yaliyofanyika Mei 3, mwaka huu kwa watumishi 125 kwa ajili ya kuandaa Mpango Kazi wa Manunuzi ambayo ni sehemu ya majukumu yao ya kila siku, yalifuatiwa na malipo ya Sh milioni 171.2 siku hiyo hiyo kwa ajili ya kuandaa nyaraka za Bunge.

Majaliwa amesema Sh milioni 155 zililipwa kwa baadhi ya watumishi zikiwa ni posho ya kuandaa miongozo ya kazi. 

“Yaani hii kazi ya ukaguzi imeyagundua haya yote kwenye maeneo manne tu. Huu ni utaratibu wa wapi? Mnazidi kutupunguzia imani, na sijazungumzia eneo la kuhamisha mafungu na utaratibu wa kuhamisha fedha kisha mnakwenda kuzichukua huko mlikozihamishia,” anasema.

Waziri Mkuu amewataka watendaji wa wizara hiyo kujenga uaminifu kwa wanaokusanya mapato kwa kufanya kazi kwa uaminifu na alitahadharisha kuwa watakaoendekea kucheza na fedha za umma hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

Aidha, Waziri Mkuu aliwapongeza watendaji wengine wa wizara hiyo ambao wameendelea kufanya kazi kwa weledi akisema: “Na nimesema hapa si wote. Wapo wenzenu wachache wanatumia vibaya nafasi zao kuichafua Wizara ya Fedha.”

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.