Rufaa ya kupinga hukumu ya kifungo cha miezi mitano jela iliyotolewa kwa mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ na Katibu wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga imewasilisha Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya.
Mmoja wa mawakili wa Sugu, Faraji Mangula amesema tayari maombi ya rufaa yao yamepokewa na kupewa kumbukumbu namba 29/2018.
“Tayari rufaa yetu imeshapokewa Mahakama Kuu (Mbeya) na tunachosubiri ni kupangiwa tarehe ya kuanza kusikiliza tu, ila tunachoshukuru watu wa Mahakama hii wapo vizuri kushughulikia suala hili,” amesema Mangula.
Mbali na kukataa rufaa hiyo, lakini pia mawakili hao wanakusudia kuomba dhamana kwa wateja wao ili waweze kuwa nje katika kipindi ambacho wanakuwa wanasikiliza rufaa yao.
Sugu na Masonga walihukumiwa baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli.
Wawili hao walitoa kauli hiyo Desemba 30 mwaka jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Mwenge jijini Mbeya.