Dar es Salaam
Na Alex Kazenga
Kamanda wa Polisi Mkoa wa kipolisi (RPC) Ilala, Deborah Magiligimba, anadaiwa kupuuza amri ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, JAMHURI linataarifu.
Inadaiwa kuwa Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi imemuandikia barua RPC kumtaka atoe askari wa kulinda usalama wakati wa ubomoaji wa nyumba za watu waliovamia eneo la Mbondole, Kata ya Msongola, Dar es Salaam.
Barua hiyo ya Msajili wa Mahakama (nakala tunayo) ni ya Mei 17, 2021 na ya kumkumbusha iliyotumwa kwake Januari 5, mwaka huu.
“Barua zote mbili amezipuuza, wala hajatoa majibu kutuelekeza ni hatua gani zaidi tunapaswa kuchukua,” anasema Martin Nasson, mlalamikaji anayedai kuvamiwa kwa viwanja vyake.
Kampuni ya udalali ya Yono Auction Mart ndio waliopewa jukumu la ubomoaji wa nyumba za wakazi zaidi ya 300 katika eneo linalomilikiwa na Nasson na mkewe, waliopewa ushindi na Mahakama Kuu katika shauri la ardhi Na. 88/2017.
Akizungumza na JAMHURI, Mkurugenzi wa Yono Auction Mart, Stanley Kevela, amesema:
“Mahakama ikitoa amri kinachofuata ni utekelezaji. Sasa ninashangaa mwaka mzima umepita tangu msajili amwandikie barua RPC kutupatia askari.
“Haiwezekani amri ya mahakama kutenguliwa na RPC. Uwezo huo wanautoa wapi?
“Mimi ninashangaa na kujiuliza, ni nani amewapa mamlaka RPC na wenzake kuwa wasuluhishi katika mgogoro huu wa Mzee Nasson? Huku ni kuingilia uhuru wa mahakama.”
Barua inayolalamikiwa kutojibiwa ni yenye Kumb. Na. EXACUTION Na. 29/2020.
Anasema tangu mwaka jana RPC amekuwa akimzungusha kumpatia askari akisingizia kusubiri kibali kutoka kwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam (ZPC) na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP).
“Barua imeelekezwa kwa RPC wa Ilala, si ZPC wala IGP, kutwambia kuwa anasubiri kibali kutoka kwa wakubwa wake ni kutuzuga tu,” anasema Kevela.
Mdai katika sakata hilo, Nasson, anasema Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala na ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam zimekuwa zikipotoshwa na wananchi wa Mbondole wakitaka ziwasaidie kubatilisha amri ya mahakama.
“Kuna barua kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwenda kwa wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na makatibu tawala wa mikoa na wilaya, inayowataka kutoingilia amri za mahakama hasa wakati wa utekelezwaji wake,” anasema Nasson.
Barua hiyo ni ya Agosti 17, 2020 (nakala tunayo) iliyosainiwa na Jaji Kiongozi, ikiwataka viongozi husika kuzingatia mipaka ya kazi zao na kutoingilia uhuru wa mahakama.
Zipo taarifa kuwa ukwamishaji wa ubomoaji huo unafanywa makusudi kuziokoa nyumba za askari polisi wastaafu waliojenga huko, miongoni mwao wakiwa ni waliokuwa wamepewa jukumu la kuimarisha ulinzi wakati uvamizi ulipoanza.
Akizungumza na JAMHURI, RPC Deborah anapingana na kauli ya Kevela, akisema hakuwa amepata amri ya mahakama.
“Mwaka jana nilikuwa bado mgeni, nilihamia hapa mwezi Juni. Barua ya utekelezaji ndiyo imetufikia, sasa tunajiandaa kuifanyia kazi. Sisi hatuna shida,” anasema RPC.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng’wilabuzu Ludigija, amekiri kuufahamu mgogoro huo, akisema baada ya Nasson, aliyeshinda shauri mahakamani kushindwa kuelewana na wakazi wa Mbondole, ameuhamishia mgogoro kwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Gazeti la JAMHURI limefika zaidi ya mara mbili kwa mkuu wa mkoa kupata ufafanuzi bila mafanikio, huku katibu wake akidokeza kuwa uamuzi utakaotolewa na mkuu wa mkoa huenda ukawa mwarobaini wa watu kuvamia viwanja vya wengine mkoani Dar es Salaam.
Chanzo cha mgogoro
Nasson anasema eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 29 lilivamiwa na wananchi kutoka Kitunda wakidai kuwa ni mali yao.
Wakati linavamiwa anadai tayari alikuwa amekwisha kuliboresha kwa kulipima ambapo liligawanywa mara mbili na kuwa viwanja viwili; Na. 15 kilichopo kitalu ‘D’ na kupewa hati Na. 93606 na kiwanja Na. 16 kitalu ‘D’ chenye hati Na. 95973.
Kwa mujibu wa nyaraka za ununuzi, Nasson alilinunua eneo hilo ndani ya miaka miwili; yaani 2003 na 2004, kutoka kwa wananchi sita tofauti ambao ni Nasoro Boli, Gina Abas akiwa na Amos Sibora na Bwile Nyangele.
Wengine ni Mohamedi Mlala, Said Lubale na Rajabu Lubale. Watu hawa ni wakazi wa Mbondole.
“Ununuzi ulifanyika mbele ya mwenyekiti wa kijiji na kuthibitishwa kimaandishi mbele ya viongozi wa kijiji na kata,” anasema Nasson, akisema lengo lake lilikuwa kujenga shule ya sekondari.
Nasson (79), na mkewe Loice (75), ni wastaafu wa taasisi mbili tofauti za serikali, wanaodai kuwa fedha yote ya kiinua mgongo waliyopata wameiwekeza katika eneo hilo.
Anasema wavamizi waliobomoa nyumba waliyokuwa wamejenga waliiba pia vifaa mbalimbali vya ujenzi na kuchoma moto bustani ya miti iliyokuwapo.
Nasson anasema yeye na familia yake waliripoti matukio hayo Kituo cha Polisi Stakishari na kufikisha taarifa ya uvamizi kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala.
Baada ya kupata taarifa, manispaa na polisi wa Stakishari walishirikiana kudhibiti uvamizi kwa msaada mkubwa wa aliyekuwa mwenyekiti wa kijiji, hivyo kuwazuia wavamizi kuendelea kuchimba mchanga.
“Yule mwenyekiti alitishiwa maisha mara nyingi, na mwaka 2014 akaamua kuachia ngazi, Mwenyekiti mpya aliyechaguliwa akawa upande wa wavamizi, akaruhusu uvamizi kuendelea,” anasema.
Mbali na sakata hilo kufikishwa ngazi ya manispaa, pia lilifikishwa kwa mkuu wa wilaya wa wakati huo, Sophia Mjema, aliyetoa agizo kuzuia shughuli yoyote kufanyika eneo lenye mgogoro.
Baada ya kuona maagizo ya DC na viongozi wengine yamepuuzwa, Nasson anasema Novemba 7, 2017, walifungua kesi Mahakama Kuu, Dar es Salaam, ambapo ilitoa amri ya kusitishwa shughuli katika eneo hilo.
“Wakati amri ikitolewa na mahakama hakuna ujenzi wa nyumba hata moja uliokuwa umekamilika. Cha kushangaza baada ya amri ya mahakama ndipo kasi ya kujenga ilipoongezeka,” anasema Nasson akisisitiza kuwa aliyechochea kasi ya ujenzi ni aliyekuwa mwenyekiti wa kijiji.
Shauri liliendeshwa kwa miaka miwili na Desemba 4, 2019 hukumu ilitoka ikiwataka wavamizi kumpisha Nasson kwenye eneo lake na kumlipa fidia ya Sh 800,000,000.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano aliyeteuliwa na wavamizi wa eneo la Nasson, Jacob Enos, ameliambia JAMHURI kuwa wapo tayari kumlipa fidia na kumtafutia eneo jingine endapo atakubali kukaa mezani kwa mazungumzo.
“Tunatambua kuwa viwanja hivi tuliuziwa kitapeli, tunajua pia kuwa mahakama imempa haki; lakini tunamuomba ashirikiane na sisi tupate mwafaka mzuri wa pamoja,” anasema Enos.
Mjumbe wa kamati hiyo, Hamis Warioba, anasema kuna eneo lenye ukubwa wa ekati 30 wamelipata Chalinze na wapo tayari kwenda kumwonyesha Nasson iwapo ataridhia.
Mwenyekiti wa sasa wa Mtaa wa Mbondole, Thomas Nyanduli, anakana tuhuma za kuchochea uvamizi, akidai kuwa maeneo mengi katika Kata ya Msongola yamevamiwa kwa nguvu na si rahisi kudhibiti.
Diwani wa Kata ya Msongola, Aziz Mwalile, anasema namna pekee ya kuumaliza mgogoro huo ni kutumia busara kwani hayupo anayeweza kuipinga amri ya mahakama.