Na Isri Mohamed

Golikipa wa Mamelod Sundowns, Ronwen Williams amechaguliwa kuwania tuzo kubwa za mpira duniani ‘Ballon D’or’ katika kipengele cha magolikipa kumi bora duniani ”YashinTrophy’

Katika kipengele hicho, Williams anashindanishwa na na Diogo Costa (FC Porto), Gianluigi Donnarumma (Paris Saint Germain), Gregor Kobel (Borussia Dortmund), Andriy Lunin (Rea Madrid), Mike Maignan (AC Milan), Giorgi Mamardashvili (Valencia), Emiliano Martinez (Aston) Villa), Unai Simon (Athletic Bilbao), na Yann Sommer (Inter Milan).

Jina la Ronwen Williams ambaye pia anaichezea timu ya taifa ya Afrika Kusini (Bafana Bafana) limeingia kwenye rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza anayecheza Afrika kupata nafasi ya kuwania tuzo hizo za kwanza kwa ukubwa duniani.

Msimu uliopita ulikuwa bora sana kwa Williams kwenye ngazi ya timu ya Taifa ambapo alishinda tuzo ya Golikipa bora wa AFCON 2023, huku akivaa medali ya shaba ya AFCON.

Katika michuano hiyo ya AFCON, hatua ya robo fainali wakicheza dhidi ya Cape Verde, Williams aliokoa penalti nne.

Aidha William akiwa mlinda lango namba moja wa Mamelod Sundown ameisaidia klabu yake kutwaa ubingwa wa ligi kuu nchini Afrika Kusini, sambamba na ubingwa wa African Football League akiwa na clean sheet 35.

Tuzo za Ballon D’or zitatolewa Oktoba 28, kwenye ukumbi wa Théâtre du Châtelet jijini Paris, Ufaransa.