Nimeshtushwa hivi karibuni kusikia dawa ya kuua magugu inayoitwa Roundup ikitangazwa kuuzwa madukani na kituo kimojawapo cha redio nchini. Mwaka 2015 Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitamka kuwa glyphosate, ambayo inatumika kutengeneza Roundup, inaweza kusababisha saratani.
Nilishangaa zaidi, baada ya kufanya uchunguzi mfupi, kugundua kuwa dawa hiyo imekuwa inatumika nchini kwa miaka zaidi ya 20. Labda ni kuanza kwangu kilimo katika miaka ya hivi karibuni ndiyo kumenifungua macho na kusikia kitu ambacho zamani nisingekisikia.
Mwenye kuelekeza masikio Marekani hatakosa kusikia kuwa kampuni ya Bayer inakabiliwa na maelfu ya kesi mahakamani ikituhumiwa na wadai mbalimbali kuwa wamepata maradhi ya saratani kwa sababu ya kutumia Roundup.
Taarifa kamili za kesi hizo zinahitaji toleo maalumu la peke yake la gazeti hili kwa sababu ya wingi wake. Mpaka kufikia Oktoba 30, 2019 idadi ya watu 42,700 walikuwa na kesi hizo za madai mahakamani.
Pamoja na kuwapo madai hayo, bado zipo taarifa mbalimbali za matokeo ya tafiti ambazo zinasema kuwa hakuna ushahidi wa uhakika kuwa viambatishi vilivyomo ndani ya Roundup vinasababisha saratani. Moja ya mashirika machache ambayo yanasema vingine, pamoja na WHO, ni shirika moja la utafiti wa kisayansi la Australia ambalo limetamka kuwa Roundup “inaweza kuwa inasababisha saratani.”
Kesi nyingi za madai zilizojitokeza dhidi ya Bayer zilifunguliwa baada ya mahakama nchini Marekani kutoa hukumu, Agosti 10, 2018, dhidi ya Bayer na kumpa mdai Dewayne Johnson dola za Marekani milioni 289 ambazo baadaye zilipunguzwa hadi dola milioni 89.
Katika hukumu ya kesi hiyo ilionekana kuwa kampuni ya Monsanto haikutoa tahadhari ya kutosha kwa watumiaji wa Roundup juu ya uwezekano wa kupata saratani kwa kutumia bidhaa yao. Baada ya hapo zimefuata kesi nyingine mbili za madai kama hayo ambazo Bayer imeshindwa.
Kama kuna suala linalojitokeza bayana juu ya hukumu za kesi dhidi ya Monsanto na Roundup ni kufanikiwa kwa Monsanto, na baadaye Bayer, kuzuia mahakama kutamka kuwa matumizi ya muda mrefu ya Roundup yanasababisha saratani. Lugha ya kisheria inayotumika huweka lawama zaidi kwa Bayer kushindwa kutoa tahadhari kuwaRoundup “inaweza kusababisha saratani.”
Roundup iliingia sokoni kwa mara ya kwanza mwaka 1973 ikitengenezwa na kampuni ya Monsanto; kampuni ambayo ilinunuliwa na Bayer mwaka 2018. Kama nchini Marekani imechukua miaka zaidi ya 45 kwa kesi za mwanzo kabisa dhidi ya Bayer na bidhaa yake ya Roundup, basi tutarajie kwamba sisi ambao tumeanza kutumiaRoundup miaka 20 iliyopita tunaweza kuanza kushuhudia dalili za madhara yake baada ya miaka 25 ijayo.
Kwa kuwa Bayer imekata rufaa dhidi ya kesi ilizoshindwa, na hasa kwa sababu ya uwezo mkubwa wa fedha wa Bayer, basi inawezekana sana kuwa itachukua muda mrefu sana kabla haijathibitishwa mahakamani kuwa Roundup ni hatarishi kwa binadamu.
Hali hii siyo nzuri kwetu. Maana yake ni kuwa tunaendelea kuuzia Roundup ikiwa upo uwezekano kuwa tunanunua sumu, tukiamini kuwa tunanunua dawa.
Labda si muhimu sana kufahamu mara moja kama Bayer watamaliza rufaa zote na kushindwa. Kama ambavyo si busara, kama unaishi miongoni mwa nyoka wenye sumu, kuweka ndani dawa inayotibu sumu ya nyoka.
Ilichukua muda mrefu sana wa vuta nikuvute mpaka baadhi ya nchi zilipokubali utafiti unaothibitisha kuwa matumizi ya sigara yanahatarisha afya ya mtumiaji na hata wale wasiovuta sigara.
Matokeo yake ni kuwa leo hii hatukatazwi kuvuta sigara ila tunapewa tahadhari kuwa sigara ni bidhaa ambayo inaweza kuhatarisha afya ya mvutaji. Unaambiwa nunua ukifahamu kuwa unahatarisha afya na maisha yako.
Tukisubiri miaka 50, kama ilivyotokea kwenye malumbano ya athari za sigara, halafu itokee kuthibitishwa bila shaka yoyote kuwa Roundup ni hatari kwa afya ya binadamu watateketea wengi.
Kwa kuwa baadhi ya tafiti zinaashiria Roundup inasababisha saratani, ni wakati mwafaka sasa wa tahadhari kubandikwa kwenye vifungashio vya Roundup kutahadharisha wanunuzi juu ya uwezekano kuwa wakiitumia wanaweza kupata saratani.
Wajibu wa kwanza kabisa wa serikali ni kulinda usalama wa raia wake. Likifanyika hili serikali haitapata sifa yoyote. Sana sana, itapongezwa tu kwa kutimiza wajibu wake.
Barua pepe: [email protected]