Yafuatayo ni maelezo ya mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Aziz, wakati wa uzinduzi wa kampuni ya utoaji huduma za gesi, Taifa Gas, anayoimiliki. Katika kampuni hiyo, Rostam ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi. Uzinduzi huo ulifanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli wiki iliyopita, Kigamboni, jijini Dar es Salaam.

“Mheshimiwa Rais, waheshimiwa mawaziri, mheshimiwa mkuu wa mkoa, waheshimiwa wakuu wa wilaya zote za Mkoa wa Dar es Salaam, waheshimiwa viongozi wote na wageni waalikwa mabibi na mabwana.

“Mheshimiwa Rais, nimepewa nafasi na muda mfupi wa kusalimia na kutoa neno dogo la shukrani mahususi kwako wewe binafsi na kwa serikali yetu. Kama alivyoeleza kwa ufasaha Mkurugenzi Mtendaji wa Taifa Gas, tuna kila sababu ya kukushukuru wewe binafsi Mheshimiwa Rais na serikali kwa namna mlivyotumia muda wetu takriban wa miaka minne uliokaa madarakani kujenga misingi imara na uwanja sawa wa kibiashara, kwa wafanyabiashara na wawekezaji nchini.

“Mheshimiwa Rais, mafanikio ambayo sisi kama Taifa Gas na wawekezaji wengine wa nje na ndani tulioanza kuyaona sasa ni matokeo ya kazi kubwa ambayo umeifanya kwa weledi mkubwa tangu umeingia Ikulu Oktoba, mwaka 2015.

“Kazi hiyo ambayo wakati fulani ilikulazimu uchukue hatua madhubuti na ngumu ndiyo ambayo sasa unathibitishia taifa na wawekezaji wa ndani na wale wa kimataifa kwamba wewe si tu mtetezi wa kweli wa Watanzania wanyonge, bali pia ni rafiki mkubwa wa sekta binafsi.

“Kauli ambazo umekuwa ukitoa na ambazo zimekuwa zikifuatiwa na hatua kadha wa kadha, ni ushahidi ulio bayana, tunatambua vema uimarishaji wa sekta binafsi utakaotekelezwa katika uwanja ulio sawa ndio utakaozaa kodi na ajira ambazo zitachangia kwa kiwango kikubwa kuimarisha huduma za kijamii sambamba na kujenga miundombinu ambayo hatimaye itasaidia kuwatoa Watanzania walio wengi katika unyonge na umaskini wa kihistoria.

“Mheshimiwa Rais, historia itakukumbuka vema katika hili. Mheshimiwa Rais, jambo hilo wakati fulani limekuwa ni gumu sana kwa kueleweka miongoni mwa wawekezaji na wafanyabiashara ambao pasipo kujua walifikia kwa makosa hatua ya kufikiri kwamba wewe si rafiki wa sekta binafsi.

Msimamo wako thabiti dhidi ya matendo ya zamani ya ujanja ujanja katika biashara na uwekezaji na ukwepaji kodi ndivyo ambavyo leo hii vimetufanya baadhi yetu ambao kwa miaka mingi tuliamua kuwekeza mitaji yetu nje ya Tanzania kupata moyo na kuanza tena kurejesha mitaji yetu hapa nchini na kuwekeza.

“Mheshimiwa Rais, Taifa Gas ni moja tu ya mifano ya uwekezaji huo, kwani tayari tumeamua kuwekeza kiasi kingine cha miradi chenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 500 katika miaka mitatu ijayo.

“Mheshimiwa Rais, uamuzi huo ambao utaongeza ajira kwa maelfu ya Watanzania na kupanua wigo wa kodi kwa serikali tumeufanya si kwa jambo lolote, bali kwa sababu ya hatua mbalimbali ambazo wewe binafsi na serikali mmezichukua na kuthibitisha namna mazingira ya kibiashara yanavyozidi kuwa rafiki kwa wafanyabiashara na wawekezaji makini, wabunifu na wanaoheshimu miiko ya biashara, kanuni na sheria za nchi.

Nimalizie salamu zangu kwa kutoa wito kwa wafanyabiashara wenzangu wa ndani na nje ya nchi watambue kwamba milango ya uwekezaji Tanzania iko wazi kwa uwekezaji madhali tu tunafanya kwa kufuata sheria, taratibu na kanuni za nchi.