Viongozi mbalimbali nchini wakiwemo wanasiasa, viongozi wa dini wameitaka serikali kuwa na mijadala ya wazi hasa mijadala inayohusu tunu na mageuzi ya kisasa yanayokuza uchumi wa Taifa.
Hayo yamebainishwa Juni 19,2023 jijini Dar es Salaam wakati wa mjadala wa kitaifa uliolenga kulinda na kuendeleza umoja wa kitaifa wakati wa mageuzi ya kisiasa na kiuchumi.
Mdahalo huo uliandaliwa na Kampuni ya Media Brains uliokuwa na majadiliano yaliyojikita katika Mkataba wa Kiserikali (IGA) uliohusisha serikali ya Dubai na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuhusu maendeleo ya bandari.
Wakizungumza katika mdahalo huo, wadau hao wamesema ipo haja ya kulinda maadili ya taifa wakati wa kujadili kuhusu mikataba inayohusu sehemu ya utekelezaji wa bandari ya Dar es Salaam kwa sababu kuna baadhi hutoa taarifa za upotoshaji.
Akiwa mmoja wa wanajopo katika mdahalo huo, Mfanyabiashara Rostam Aziz amesema Tanzania imefika ilipo kutokana na uongozi thabiti wa viongozi waliopita kwa kuangalia maslahi ya nchi.
Aidha Rostam amesikitishwa na aina ya majadiliano kuhusu bandari ya Dar es Salaam ambayo yamejikita katika misingi ya udini,siasa na ukabila ambao ni hatari kwa nchi.
“Tuko katikati ya mjadala mzito unaohusisha ustawi wa uchumi wa nchi, lakini kuna sauti zinazoibuka ambazo zinaleta migawanyiko, hii si njia sahihi,” amesema Rostam
Amesema mjadala wa kuhusu bandari ya Dar es Salaam unaendeshwa kishabiki na kuongeza kuwa kuruhusu sekta binafsi kuendesha bandari hiyo ni jambo la busara.
“Ni fahari kuwa katika sehemu ambayo nchi nyingi zinaitegemea bandari ya Dar es Salaam, ukiacha watu wa kwetu hapa hapa kuna nchi jirani zinategemea bandari ya Dar es Salaam..
“Hivyo ni muhimu tukazitumia ili ziweze kusaidia uchumi wa nchi yetu na kutumia hayo aliyotupa Mungu kwamba tupo katika eneo ambalo tunaitegemea bandari yetu kuhakikisha inafanikisha kwa ufanisi mkubwa,”ameogeza Rostam.
Amesema ni vema Wananchi wakatunza umoja wao wa kitaifa na kuweza kutoa majadiliano yao yaliyowezeshwa na kiongozi mmoja ambaye ni mwanamke wa shoka, Rais Samia pamoja na kuwepo kwa usalama wao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi(TPSF), Angelina Ngalula amesema uwekezaji unaofanywa hapa nchini mdau wa kwanza kwenye biashara zinazofanywa hapa nchini ni serikali.
“Sekta binafsi ndiyo engine ya uchumi kwasababu kupitia shughuli zake hutengeneza ajira ambapo zaidi ya asilimia 80 kwenye nchi zinazoendelea zinazalosha ajira,”alisema Ngalula
Aidha Ngalula ameongeza kuwa Wananchi wanapaswa kuwa wamoja katika mhajadala wa bandari katika kujikita kuzungumzia agenda iliyopo badala ya kumshambulia mtu.
“Tushindane kwa facts, figure tuweke mezani.Nimekaa bandari takribani miaka 18, naelewa bandari ya Dar es salaam na nyingine ambazo tunapakana nazo.
“Fursa ambazo tumezikosa kwa muda mrefu ni kubwa sana ambazo zingeweza kubadilisha kabisa uchumi wa nchi yetu ni kwasababu sisi tumekaa kama kisiwa shughuli ya bandari lazima kusimamia mnyororo mzima wa usafirishaji.
“Usiposimamia vizuri mnyororo wa usafirishaji utajikuta upo nje ya biashara,”ameongeza Ngalula
Amesema shughuli ya bandari inapaswa kuwa kusimamia mzigo unapotoka, usafirishaji hadi ufike kwa mhusika.
Amefafanua kuwa Tanzania inamiliki bandari na kumsubiri mtu ambaye nchi haina miadi naye kusafirisha mizigo bandarini badala ya kutafuta mzigo ili kufikisha unapokwenda.
Amesema ili kufanikisha hilo, kampuni inahitajika ili kufanya yote hayo ambaye mwenye uwezo wa kuwasiliana na wenye mizigo, makampuni makubwa huko walipo na kuleta nchini.
Amesema Bandari ya Dar es Salaam inafanya kazi kwa njia ambayo inahitaji uwekezaji mkubwa katika teknolojia mpya za utunzaji na uhifadhi wa mizigo.
Kwa upande wake Katibu wa Baraza la Maaskofu Tanzania(TEC), Charles Kitima amesema mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi Tanzania yanaendelea hivyo inahitajika nguvu ya kuelimishana.
Amesema suala la kukuza uchumi wa nchi si geni hapa nchini, kwasababu hata Hayati Mwalimu Nyerere aliamini ushirikiano wa serikali na sekta binafsi nchini na alizikaribisha.
Amesema hakuna haja ya kupuuza sauti ya wawekezaji wa ndani katika maendeleo ya nchi.
Akichangia mada katika mdahalo huo, kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amesema ipo haja ya kuunda kampuni ya uendeshaji ya Bandari ya Dar es Salaam ambayo itaingia ubia na DP World kufanya kazi bandari ya Dar es Salaam ili kuwezesha ushirikishwaji wa wenyeji ili kuua mjadala unaoendelea wa kuuza au kubinafsisha.
“Tofauti ya rasilimali bandari na rasilimali dhahabu, ni kwamba dhabau unaichimba ukiondosha hairudi bandari huwezi kuiondoa na ndiyo maana huo mjadala wa kuuza nashangaa Mzee wasira ulishtuka hata wakiuza itakuwa pale pale tu, huwezi kuibeba na kuiondoa,”amesema Zitto.
Kwa mujibu wa Zitto amesema kampuni hiyo inaweza kumilikiwa na wageni na wazawa ili wapate uwezo wa kuendesha bandari hivyo kumiliki kampuni nzima.
Aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema amesema si dhambi kuleta mwekezaji katika nchi na haiwezi kukwepa na kwamba kukataa uwekezaji nin jambo baya.
Amesema hakuna udini katika masuala ya uwekezaji wa bandali ila wapo wanaotaka kuzuia hoja kwa kuweka masuala ya dini kwenye mjadala huo ambao ndiyo walipaswa kukemewea.
Lema ambaye ni Mfanyabiashara ameshauri “Nchi hii inahitaji mwekezaji zaidi ya bandarini, inahitaji wabia wengi nchi hii ilikuwa inajivunia makaa ya mawe sasa hivi yanapigwa vita,”amesema lema.
Nae Mwanasiasa Mkongwe, Stephen Wasira amesema serikali inapaswa kutoa elimu zaidi ili kutoa wasiwasi wananchi kuhusu uuzwaji wa bandari ya Dar es Salaam.
“Mitandao ya kijamii inapandisha pressure sana, utaona bandari inauzwa mara inauzwa miaka 100 …yaani iuzwe halafu miaka 100 nikapata hisia huu upotoshaji .
“Sasa tumeridhika bandari haibinafsishwi wala kuuzwa Watanzania tusaidiwe kuelewa bandari haiuzwi hatutabinafsisha tena ni project ya sehemu tu ya bandari,”amesema Wasira.