Mwanasoka mahiri aliyewahi kukipiga kwa mafanikio Manchester United chini ya Kocha Alex Ferguson, Wayne Rooney, amekiri hadharani kuwa kamari ni moja ya mambo yaliyoathiri kiwango chake uwanjani kwa kiasi kikubwa.
Rooney, ambaye wakati fulani alikuwa nahodha wa timu ya taifa ya Uingereza akilipwa paundi 300,000 kwa wiki na Manchester United, anasema alitumia kiasi kikubwa cha mshahara wake huo kucheza kamari.
Kilichomponza, anasema, ni kuanza kushinda katika mchezo huo hadi ukamwingia akilini akiamini kuwa nayo ni njia ya kujiongezea utajiri.
“Lakini baadaye nikaanza kushindwa. Lakini niliendelea kucheza nikiamini kuwa nitarudisha pesa zangu,” anasema.
“Huku nilikuwa ninatakiwa kuichezea klabu yangu na timu ya taifa lakini mawazo ya kamari yakawa yananiandama, hivyo kuathiri kiwango changu uwanjani,” anabainisha.
Inakadiriwa kuwa staa huyo wa soka alijiingiza katika deni la paundi 700,000 katika kipindi cha miezi mitano kutokana na kuzama kwenye kamari.
Mwaka 2008 alipoteza paundi 65,000 katika kipindi cha saa mbili kupitia kamari katika kasino moja.
Rooney, mwenye umri wa miaka 34 sasa, anaeleza: “Nilikuwa kijana ‘barobaro’ ambaye alipata fedha nyingi ghafla. Kwa kila mechi ya ugenini nikiwa Manchester United unakaa katika hoteli na ukiwa na timu ya taifa unakuwa hotelini kwa siku kati ya saba na kumi.
“Unaboreka na kufanya mambo yasiyo na maana ili kujifanya mchangamfu. Wakati huo kucheza kamari ilikuwa moja ya shughuli za kuchemsha akili. Lakini kabla hujajua madhara yake, unakuwa umeshapoteza kiasi kikubwa cha fedha.”
Anawaonya vijana kuwa waangalifu wanapojiingiza kwenye uchezaji kamari. “Nilianza kwa kushinda na nikaamini kuwa hiyo ilikuwa njia rahisi ya kupata fedha. Lakini kumbe unazama taratibu,” anasema.
“Namshukuru Mungu kuwa niliweza kulipa madeni yangu na kuachana na kamari. Nilijifunza kutokana na makosa. Kama ukiendelea kucheza, unapoteza zaidi. Hapo ndipo unapoweza kujikuta katika hali mbaya,” anabainisha.