MANCHESTER, England
Kabla ya wikiendi hii kufunga bao la kwanza miongoni mwa matatu katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Tottenham, mashabiki wa soka England walijiuliza maswali kadhaa kuhusu uwezo wa mwanasoka mkongwe na maarufu duniani, Cristiano Ronaldo.
Akiwa na umri wa miaka 36 sasa, kurejea kwake Manchester United kulizua hamasa ya aina yake kwa mashabiki – na tayari amekwisha kufunga mabao kadhaa kwa timu yake – lakini ana mchango wowote kwa kikosi hicho?
Usajili wake ulikuwa sawa na mwana mpotevu kurejea nyumbani akitokea Juventus. Hali hiyo ilitokea wakati kila mtu akidhani Ronaldo angekwenda Manchester City!
Lakini baada ya kufunga mabao manne katika mechi zake tatu za kwanza, akafunga mabao mawili tu katika mechi sita zilizofuata kabla ya juzi – yote yakiwa ni ya ushindi wa dakika za mwisho katika Ligi ya Mabingwa dhidi ya Villarreal na Atalanta.
United wamelazimika kubadili mbinu za mchezo ili kumpa nafasi mshindi mara tano wa tuzo ya Ballon d’Or na Kocha Ole Gunnar Solskjaer amejikuta katika wakati mgumu, timu yake ikionekana kuwa nyuma kiubora kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa, hasa baada ya kufungwa nyumbani mabao 5-0 na Liverpool.
Mwanasoka mwenzake wa zamani, Leonardo Bonucci, anadhani Juventus ilikuwa timu bora zaidi kabla ya kusajiliwa Ronaldo na nahodha wa zamani wa Liverpool na Scotland, Graeme Souness, haamini kuwa anapaswa kuanza katika kila mchezo.
Ronaldo ni msaada au kikwazo?
Mabao matatu ya Ronaldo katika mechi sita za Ligi Kuu ni ujio mzuri kabisa – mawili katika mechi yake ya kwanza dhidi ya Newcastle na moja dhidi ya West Ham katika mechi yake ya pili – lakini kwa kiwango chake si jambo la kujivunia.
Mara ya mwisho kumaliza msimu wa ligi akiwa na asilimia 50 au chini ya kiwango cha kufunga mabao ilikuwa mwaka 2006-07, msimu wake wa nne akiwa United, alipofunga mabao 17 katika mechi 34.
Mabao hayo yakamfanya kushika nafasi ya nne katika wafungaji wa Ligi Kuu, huku Didier Drogba akichukua Kiatu cha Dhahabu kwa mabao 20.
Bado ni mapema lakini wachezaji 14 wamefunga mabao mengi zaidi yake msimu huu, wakiwamo Hwang Hee-chan wa Wolves na Ismaila Sarr wa Watford.
Badala yake, ushujaa wa Ronaldo unaonekana zaidi Ligi ya Mabingwa – mashindano ambayo yeye ndiye aliyefunga mabao mengi zaidi, mabao 137.
Mabao yake sita yanamfanya kuifungia United jumla ya mabao 124 wakati akiwa na mabao 450 kwa Real Madrid; rekodi ya dunia ya mabao 115 kwa Ureno, mabao 101 kwa Juventus na matano aliyofunga akiwa na Sporting Lisbon.
Siku hizi anacheza kama namba tisa tofauti na awali alipokuwa akicheza kama winga alipowasili kwa mara ya kwanza England akitokea Sporting.
Anashika nafasi ya 216 kwa kugusa mpira mara 243 uwanjani; lakini anashika nafasi ya 16 kwa kugusa mpira mara 39 katika eneo la adui kwenye Ligi Kuu ya England.
Ronaldo ni wa nane kwa kupiga mashuti 25 kwenye msimu huu wa Ligi Kuu, akiwa nyuma ya wachezaji wenzake wa United, Mason Greenwood na Bruno Fernandes. Anashika nafasi ya tisa kwa mashuti yaliyolenga goli.
“Unaweza kufunga mabao na kufurahisha mashabiki, lakini sidhani kama anaweza kucheza kila mechi,” anasema mchambuzi wa soka wa Sky Sports, Souness na kuongeza:
“Ninaweza kuwa naye (kwenye timu), lakini mazungumzo yanapaswa kuwa ‘hautaanza kila mechi lakini ushawishi wako utakuwa mkubwa kwa miezi tisa’.”
Ana ushawishi wowote?
Si kivile. Takwimu zake za kusukuma mipira haziridhishi. Ni mchezaji mmoja tu kwenye Ligi Kuu – ukiachana na waliocheza chini ya dakika 15 – aliye chini ya takwimu za Ronaldo (0.74 kwa dakika 90); beki wa Everton, Mason Holgate.
Kwa mujibu wa data za Statsbomb, Ronaldo anashika nafasi ya 384 kwa kusukuma mbele mipira ndani ya dakika 90. Kwenye Ligi Kuu msimu huu kuna wachezaji 429, wakiwamo magolikipa.
Edinson Cavani – aliyecheza mechi 26 kwenye Ligi Kuu msimu uliopita – alikuwa na wastani wa 3.86 kwa dakika 90.
Mwandishi wa ESPN anasema: “Kilichobadilika kwa United msimu huu ni Ronaldo. Wana mchezaji kule mbele ambaye hafanyi kazi ya maana.
“Cavani hukimbia mbele mara kwa mara. Kukimbia kwake kuna maana, anafanya mashabiki na wachezaji wenzake kusonga mbele. Kama Ronaldo asingekuwapo, United ingekuwa na umoja zaidi.”
Mchambuzi wa BBC, Micah Richards, anasema: “Kama unamwingiza Ronaldo, unacheza staili gani? ‘Balance’ (usawa) iko wapi? Bila shaka kama Ronaldo anapatikana, unaweza kumwingiza. Lakini weka watu wengine nyuma yake wa kumsaidia.”
Katika umiliki wa mpira, Ronaldo amefanikiwa kufanya hivyo mara tatu tu katika eneo la adui – na ametoa pasi 48 katika eneo la timu yake.
Katika upigaji pasi kwa ujumla, yupo chini sana – nafasi ya 208 kwa pasi 169 huku wachezaji 195 wakipiga pasi mara mbili yake.