NGULI wa soka nchini Brazil ambaye ni mshindi wa tuzo ya mwanasoka bora wa dunia Balon d’Or mwaka 2005, Ronaldo de Assis Moreira maarufu kwa jina la Ronaldinho ametagaza rasmi kustaafu kusakata kabumbu.

Kwa mujibu wa BBC, aliyethibitisha kustaafu kwa mwanasoka huyo ni kaka yake ambaye pia ni wakala wake Roberto Assis ambaye amesema kuna jambo watalifanya nchini Brazil, Ulaya na hata Asia kama ishara ya kuwaaga rasmi mashabiki wake wa soka.

Hata hivyo Ronaldinho mwenye umri wa miaka 37, hajacheza mchezo wowote tangu mwaka 2015 lakini anakumbukwa zaidi alipoiongoza timu yake ya taifa ya Brazil kushinda kombe la dunia mwaka 2002, kabla ya kushinda kombe la mabingwa Ulaya akiwa na Barcelona.

Ronaldinho alianza safari yake ya soka katika klabu ya Gremio nchini Brazil kisha akahamia PSG ya Ufaransa mwaka 2001 na baadaye kukipiga na Barcelona kwa misimu mitano akishinda mataji mawili ya La Liga na moja la mabingwa Ulaya.

Baada ya kuitumikia Barcelona, Ronaldinho pia alikipiga katika klabu ya AC Milan ya Italia na kuisadia kushinda taji moja la Seria A katika msimu wa 2010/11.

Baada ya hapo alirejea nchini Brazil na kujiunga na Flamengo mwaka 2011, kabla ya kuhamia katika vilabu vya Atletico Mineiro, Queretaro na Fluminense.