πŸ“Œ Dkt. Biteko amwakilisha Rais Samia kuwa mgeni maalum Kusimikwa Askofu Romanus Mihali

πŸ“Œ Asema Serikali itahakikisha uchaguzi unakuwa wa huru na haki

πŸ“Œ TEC yaipongeza Serikali kwa kuendeleza Uhuru wa kuabudu nchini

Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewaomba viongozi wa dini nchini kuliombea Taifa wakati huu wakati Tanzania inaelekea katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani ili kuendelea kuwa na amani.

Dkt. Biteko amesema hayo Aprili 27, 2025 Iringa Mjini alipomwakilisha Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa mgeni maalum katika sherehe ya kusimikwa na kuwekwa wakfu kwa Askofu wa Jimbo la Iringa, Mhashamu Romanus Mihali.

Dkt. Biteko amesema Serikali chini ya Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inalojukumu la kuhakikisha uchaguzi Mkuu unadanyika kwa amani na haki.

β€œWito wangu kwa kanisa ni kuendelea kuliombea Taifa liendelee kuwa na amani,” amesema na kuongeza kuwa atamtamtaatifu Mhe. Rais kuhusu ahadi ya maaskofu kuliombea taifa hili kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao.

Askofu Mkuu mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amempongeza Askofu Mihali kwa wadhifa huo na kumshauri kutumikia watu akizingatia kuwa yeye ni mwanadamu aliyeinuliwa kati ya wanadamu na kuwekwa kati yao ili awatumikie.

Amemtaka kuongoza na kuwaelekeza huku akiwaonya kwa uvumilivu utakaotokana na kuomba baraka za Mungu.

β€œ Kumbuka kuwahudumia mapadre, mashemasi, watu masikini na wageni wanaohitaji huruma yako nawe utakuwq umefanya kazi ya kitume.” Amesema Kardinali Pengo.

Pia amemtaka kushirikiana na makanisa yote hasa yanayohitaji msaada ambapo amesema kufanya hivyo atakuwa ametimiza maelekezo ya Kanisa.

Aidha, amewataka waumini kumpokea kiongozi wao kwa moyo wa shukrani na furaha huku wakimheshimu kama mtumishi wa kristo.

Naye Makamu wa Rais wa Baraza la maaskofu Tanzania ( TEC) Mhashamu Eusebius Nzigilwa ameipongeza Serikali kwa ushirikiano wake na madhehebu ya dini nchini.

β€œ Mgeni rasmi ambaye umemwakilisha mheshimiwa Rais, tunakushukuru kwa kuungana nasi na hii insonesha namna Serikali inavyothamini na kulinda uhuru wa kuabudu nchini” amesema.

Aidha, Askofu Nzigilwa ameiomba Serikali kuendeleza ushirikiano na madhehebu ya Dini.

Pia Askofu Nzigilwa amewahimiza waumini wakatoliki kuliombea Taifa wakati huu kuelekea Uchaguzi Mkuu ili taifa liendelee kuwa na mani, umoja na mshikamano.

Amewataka watanzania kuchagua viongozi, wenye uwezo, wazalendo wanaoishi kwa kuzingatia misingi ya haki na uadilifu kwa maendeleo na Ustawi wa Taifa.

Mwakilishi wa Baba Mtakatifu nchini Askofu Mkuu Angelo Ankantino amemshukuru Askofu mstaafu Ngalalekumtwa kwa maboresho, amenshukuru kwa huduma bora kwa kanisa.

Amentaka Askofu mpya kuwa kiongozi mwema mwenye moyo wa upendo na kujali, mwenye unyenyekevu huku akilinda haki kwa wote.

β€œjenga daraja kati ya Mungu na waumini ili kuendeleza ushirikiano na muunganiko kati Mungu na waumini” amesema.

Akizungumza baada ya kusimikwa, Askofu Mihali amempongeza Dkt. Biteko kwa hotuba ambayo amesema imejawa ubunifu mbinu zenye mvuto kwa wasikilizaji.

Pia amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan hatua yake ya ukinara wa kuendelea kuwaunganisha Watanzania.

Kabla ya kuhitimisha ibada ya misa, mwashamu Mihali alipita na kutoa baraka kwa umini ikiwa ni ishara ya kuanza kutumikia wadhifa huo mpya katika ngazi ya askofu.

Sherehe hizo zimehudhuriwa na maelfu ya wananchi wakiwemo maaskofu, mapadre, mafrateli, watawa wa kike na wakiume pamoja na viobgozi mbalimbali wa Serikali na wabunge.