Na Mwandishi wetu.
Oktoba 4 mwaka 2020 Yanga walitangaza kuachana na kocha wao mserbia, Zlatko Krmpotic, ikiwa ni siku 37 toka aajiriwe kwa wanajangwani hao. Uamuzi huo ulitangazwa na Yanga SC ikiwa ni baada ya kumaliza mechi yao kwa ushindi wa goli 3-0 dhidi ya Coastal Union.
Kocha mserbia akiwa anatoka uwanjani kama shujaa kutokana na magoli matatu safi yaliyowekwa nyavuni na Carlos Carlinhos, Haruna Niyonzima na Yacouba Sogne akakutana na taarifa kwamba HAUTAKIWI.
Alitumuliwa akiwa ameshinda mechi 3 zote za mwanzo ingawa alilalamikiwa kwa soka lisilovutia lakini alipohojiwa na waandishi wa habari alikuwa akisema kwake cha muhimu ni point 3 na sio jambo jingine lolote.
Juzi nimemsikia kocha mbrazil Robertinho akiwajibu waandishi kuhusu kumfanyia mabadiliko Clatous Chama dakika ya 37 akisema kwake cha muhimu point 3 zimepatikana na hajali kuhusu nani anacheza na nani hachezi. Ghafla nikakumbuka yaliyomkuta Zlatko Krmpotic.
Chama hajasafiri na timu kwenda Dodoma kwa madai ya kupatwa na homa. Kocha Robertinho naye hana habari kwa sababu anaamini timu imesajili wachezaji wengi na wote wana mchango wa kuipa timu matokeo bila kumtegemea mchezaji mmoja. Kwake muhimu ni point 3 tu.
Mashabiki wanasema kocha aingie kwenye mfumo wa Chama kama anaona Chama haiingii kwenye mfumo wake. Ni kauli ya kipuuzi wala haina chembe ya ufundi ndanimwe lakini amini hiyo kauli asipoizingatia itamuondoa Msimbazi.
Yes ataondoka kama Zlatko wa Yanga kwa sababu timu zetu zina watu wake wanaowaabudu sio falsafa fulani. Mashabiki wa Bongo hawajawahi kuwa mashabiki wa makocha bali wachezaji wao wanaowapenda na ukitaka kufupisha maisha yako Kariakoo wachukie wale wanaowapenda wao.
Robertinho anatakiwa kusoma andiko la Yanga kwa Zlatko Krmpotic katika kitabu cha Oktoba sura ya 2020 mstari wa 4 kifungu kidogo cha 3 ili apate kanuni ya kubaki Msimbazi kwa usalama.