Hatima ya Chama cha Ushirika cha Wakulima wa eneo la Bonde la Ufa katika mikoa ya Manyara na Arusha (RIVACU) sasa iko mikononi mwa Rais John Magufuli, baada ya Baraza la Ardhi la Mkoa wa Manyara kuirudisha katika kiwanja cha ushirika huo kampuni ya Njake Enterprises Oil Limited.
Njake Enterprises Oil Limited, inayojihusisha na biashara ya mafuta, inamilikiwa na Jafet Lema.
Lema aliwahi kutajwa katika kashfa ya ukwapuzi wa fedha za akaunti ya EPA, lakini yeye na wenzake waliepuka mkono wa sheria baada ya Rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete, kuwataka warejeshe fedha hizo ili washishitakiwe.
Uamuzi wa kuirejesha Njake ulifanywa wiki iliyopita na Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi Mkoa wa Manyara, Cyriacus Kamugisha, baada ya maombi yake. Dalali aliyeteuliwa na Mahakama – kampuni ya Kibaigwa Auction Mart ya mjini Babati – ndiyo iliyotekeleza agizo hilo.
Kwa mujibu wa mkataba wa miaka 10 uliosainiwa Desemba 18, 2002 kipengele cha 16 na pande zote mbili, RIVACU ilitakiwa kununua uwekezaji uliokuwapo kama sharti la mkataba au pande zote zikubaliane kuongeza mkataba huo.
Mwanasheria wa Kampuni City Trust iliyosimamia kumwondoa mpangaji huyo wiki iliyopita, Donald Mwakingwe, anasema bado hawajakata tamaa kurejesha mali zote za ushirika, likiwamo eneo ililokabidhiwa Njake kwa kibali walichopewa na Mrajis wa Vyama vya Ushirika.
Mwenyekiti wa RIVAVU, Lohay Langay, ameomba Rais Magufuli aingilie kati, akisema hatua iliyochukuliwa inarudisha nyuma jitihada za kufufua ushirika nchini.
“Sisi hatupingi hatua iliyochukuliwa na Baraza la Ardhi, lakini tunachofahamu masuala yote ya ushirika yanazungumzwa mezani, na siyo kwenye vyombo vya kisheria.
“Hatuna tena cha kufanya zaidi ya kuomba Rais aingilie kati ili mali zetu zirejee mikononi mwetu na hatimaye kufufua ushirika ambao tayari ulishaanza kusahaulika tofauti na miaka 30 iliyopita,” anasema Langay.
Mwanasheria wa Njake Enterprises Oil Limited, Rigold Nkya, anasema hatua iliyochukuliwa na RIVACU ya kumwondoa mteja wake haikuzingatia taratibu za kisheria.
Anasema amefungua jalada la jinai kwa hatua za kisheria ili kukomesha kile alichokiita tabia iliyozoeleka ya baadhi ya watu kujichukulia sheria mkononi.
“Ufungaji wa kituo ulikuwa batili kwa kuwa mteja wangu hakupewa notisi kama sheria inavyoelekeza, wala hakukuwa na amri yoyote ya Mahakama iliyomtaka mteja wangu kuondolewa, mbaya zaidi kilichofanyika si kumwondoa, bali ni kuharibu kabisa mali ndiyo maana nimefungua jalada la madai namba BAB/RB/223/ 2017,” anasema Nkya na kuongeza:
“Hatuna nia ya kudhulumu mali za ushirika, hatudaiwi kama inavyopotoshwa na viongozi wa RIVACU, tunachotaka ni mkataba uzingatiwe kama tulivyokubaliana, hatua waliyochukua inakiuka mkataba na tayari tulishalipa fedha za pango kwa miezi mitatu kuanzia Januari hii (2017) mpaka Machi, mbona hawasemi?”
Wiki iliyopita RIVACU ikishirikiana na wanasheria wa City Trust Debt Collectors na Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini waliwaondoa wapangaji, wakiwamo Njake kwa madai kuwa hawalipi kodi pango.