Uuzwaji wa shamba kubwa la kahawa la Gararagua lililopo Wilaya ya Siha mali ya Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Kilimanjaro (KNCU) umedaiwa kugubikwa na madudu mengi, ikiwamo kuuzwa chini ya thamani halisi ya bei ya soko, pamoja na kutokujulikana zilipo ekari 2,000.

Shamba hilo liliuzwa mwaka 2017 na KNCU kwa dola za Marekanai milioni 4.2 sawa na Sh bilioni 9.24, ikiwa ni mkakati wa chama hicho kujinasua na madeni makubwa likiwamo deni la Sh bilioni 5.2 ambalo chama hicho kilikuwa kinadaiwa na Benki ya CRDB.

Liliuzwa kwa Kampuni ya Tanbreed/Africado baada ya chama hicho kuvunja mkataba na mwekezaji aliyekuwa akiendesha shamba hilo Kampuni ya Ocean Link Shipping Services Limited na kukubali kumlipa fidia ya Sh bilioni 2.9 malipo ambayo yanadaiwa kugubikwa na utata pia.

KNCU ilivunja mkataba na mwekezaji huyo uliokuwa wa miaka 30 na ambao ungefikia ukomo mwaka 2030, hivyo mwekezaji huyo alilipwa fidia hiyo ya miaka 16 iliyobaki kulingana na mkataba wake kama angeendelea na uwekezaji.

Hata hivyo ripoti ya ukaguzi uliofanywa na Mkaguzi wa Ushirika Mkoa wa Kilimanjaro imebaini madudu mengi kwenye mchakato mzima wa kuuzwa kwa shamba hilo ambalo kwa mujibu wa ripoti hiyo lilikuwa na ukubwa wa ekari 5,414 mwaka 1980.

Akiwasilisha muhtasari wa ripoti ya ukaguzi iliyoishia Juni 30, mwaka jana kwenye Mkutano Mkuu wa 35 wa KNCU wiki iliyopita, Mkaguzi wa Ushirika Mkoa wa Kilimanjaro, Joseph Macha, anasema kwa mujibu wa hatimiliki ya shamba hilo yenye namba 4359 iliyotolewa Oktoba 1980 shamaba hilo lilikuwa na ukubwa wa ekari 5,414.

Anasema pamoja na hati hiyo kuonyesha shamba hilo lilikuwa na ekari 5,414, uthaminishaji wa shamba hilo uliofanywa Februari 2015 unaonyesha shamba hilo lina ukubwa wa ekari 3,414 na kuhoji zilipo ekari 2,000.

Kutokana na udanganyifu huo katika kutathmini ukubwa wa shamba hilo, ripoti hiyo imebainisha kuwa KNCU imekosa mapato ya Sh 5,545,931,759 ikiwa ni wastani wa Sh 2,772,966 kwa kila ekari, huku hatua zikiwa hazijachukuliwa kutokana na udanganyifu huo.

Mkaguzi huyo katika ripoti yake hiyo ametoa mapendekezo kwa Bodi ya KNCU iliyopo kufanya uchunguzi juu ya kutoonekana kwa ekari hizo 2,000 kwenye ripoti za chama hicho na kuchukua hatua dhidi ya waliohusika na udanganyifu huo.

Madudu mengine yaliyofichuliwa kwenye ripoti hiyo ni shamba hilo kuuzwa chini ya thamani halisi ya bei yake ambapo liliuzwa kwa Sh  9,240,000,000  huku thamani ya bei ya soko kwa mujibu wa ripoti ya uthamini wa shamba hilo ya mwaka 2015  ikiwa ni Sh 9,942,000,000.

Kutokana na shamba hilo kuuzwa chini ya bei halisi ya soko, mkaguzi huyo anasema katika ripoti yake kuwa KNCU ilipata hasara ya Sh milioni 642 na kutoa mapendekezo ya kufanyika uchunguzi juu ya jambo hilo.

Ripoti hiyo ya ukaguzi inadaiwa Bodi ya KNCU iliyokuwepo awali ikiongozwa na  Aloyce Kittau na makamu wake, Hatibu Mwanga, inadaiwa kuilipa Kampuni ya Uwakili ya Kisaka Sh milioni 236 kama malipo ya ushauri kwenye mchakato wa uuzwaji wa shamba hilo.

“Tulijaribu kuomba nyaraka zinazoonyesha makubaliano ya KNCU na Kampuni ya Uwakili ya Kisaka ikiwamo mikataba lakini uongozi wa ushirika ulishindwa kuthibitisha pamoja na hati za malipo ya fedha hizo,” anasema mkaguzi huyo katika ripoti yake.

Madudu hayo ndiyo yaliyoisukuma serikali kupitia kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuunda timu ya kuchunguza uuzwaji wa shamba hilo na matokeo ya uchunguzi huo ‘yakawasukuma’ ndani waliokuwa viongozi wa Bodi ya KNCU.

Mwenyekiti wa bodi hiyo na makamu wake pamoja na aliyekuwa Meneja wa KNCU, Honest Temba wakafunguliwa mashitaka ya uhujumu uchumi kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi wakidaiwa kutumia madaraka yao vibaya na kuisababishia KNCU hasara ya Sh bilioni 2.9.

Katika shitaka la kwanza, viongozi hao wanadaiwa kuwa kati ya Julai 2014 na Novemba 2017 wakiwa viongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Kilimanjaro (KNCU) walitumia madaraka yao vibaya.

Mwendesha Mashitaka wa Jamhuri, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Abdallah Chavula, alidai katika hati ya mashitaka kuwa katika tarehe tofauti, washitakiwa hao waliilipa kampuni hiyo ya Oceanic Link Shipping Services Ltd iliyokuwa mwekezaji katika shamba hilo fidia ya Sh bilioni 2.9, kitendo ambacho kiliinyima haki KNCU.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka iliyosomwa na wakili huyo mwandamizi wa serikali mbele ya Hakimu Pamela Mazengo wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, washitakiwa hao kwa pamoja na kwa makusudi, waliilipa kampuni hiyo kiwango hicho cha pesa na kuisababishia hasara KNCU ya Sh bilioni 2.9.

Mpaka sasa viongozi hao wanashikiliwa katika Gereza Kuu la Mkoa la Karanga hadi watakapopangiwa tarehe ya kuanza kusikilizwa katika Mahakama Kuu baada ya kunyimwa dhamana na hata ‘walipokimbilia’ Mahakama Kuu Kitengo cha Makosa ya Uhujumu Uchumi na Ufisadi waligonga mwamba.

Mbali na hao, wamo viongozi wa Kiwanda cha Kukoboa Kahawa cha Tanganyika Coffee Curing (TCCCo), Maynard Swai, aliyekuwa mwenyekiti wa bodi na Andrew Kleruu aliyekuwa meneja wa kiwanda hicho nao walifikishwa mahakamani wakidaiwa kutumia madaraka yao vibaya.

Walisomewa mashitaka na Wakili huyo huyo Mwandamizi wa Serikali, Abdallah Chavula na  wanadaiwa kati ya Januari 2014 na Desemba 2015 walitumia madaraka yao vibaya kwa kununua mtambo wa kukoboa kahawa bila kufuata taratibu.

Kulingana na hati ya mashitaka, washitakiwa hao wanadaiwa kununua mtambo huo wa kukoboa kahawa kutoka Kampuni ya Brazafric ya Brazil bila kufuata taratibu na kuisababishia TCCCo hasara ya Sh bilioni 1.67. Watuhumiwa wote hao wanashikiliwa katika Gereza la Karanga.