Ripoti ya awali kuhusu uchunguzi wa mchakato wa ununuzi wa mabehewa mabovu uliofanywa na Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), imebaini kuwa menejimenti ya kampuni hiyo haikuwa makini kushughulikia maombi ya kuongezewa muda, yaliyowasilishwa na Kampuni ya Hindusthan Engineering and Industries Limited ya nchini India.
Uchunguzi umebaini kuwa mkataba wa zabuni namba PA/113/2012-13/ME/G/OE/014 ya ununuzi wa mabehewa 274 ya mizigo, Kampuni ya Hindusthan Engineering and Industries Limited iliwasilisha maombi ya kuongezewa muda Juni 13, 2014 na kurudia tena ombi lake Septemba 12, 2014 lakini menejimenti ya TRL ilipuuza kwa kutojibu maombi hayo.
Zabuni nyingine inayochunguzwa ni namba PA/113/2012-13/ME/G/OE/013 iliyosainiwa kati ya TRL na kampuni hiyo Machi 21, 2013 inayohusu ununuzi wa mabehewa 25 ya mizigo yenye thamani ya dola za Marekani 2,561,187.50. Taarifa ya uchunguzi wa awali kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) inaeleza kwamba zabuni hiyo iligawanywa katika makundi matatu ikiwa ni pamoja na ununuzi wa mabehewa 174 ya mizigo, mabehewa 50 ya kusafirisha mafuta ya petroli na mabehewa mengine 50 ya mizigo (container carrier wagons).
Kwa makundi yote matatu yanayojumuisha idadi ya mabehewa 274 kwa mkataba uliosainiwa kati ya TRL na Kampuni ya Hindusthan Engineering and Industries Limited Machi 21, 2013, wenye thamani ya dola 28,487,500 za Marekani.
Licha ya kutopewa majibu ya maombi yao, kampuni hiyo ilituma tena maombi yake ya kuongezewa muda wa mkataba kwa menejimenti hiyo Januari 18, mwaka huu, na kukubaliwa na Bodi ya Zabuni ya TRL, Januari 23, mwaka huu, ambayo iliongeza muda wa zabuni hiyo hadi Aprili 30, mwaka huu.
Uchunguzi pia umebaini kuwa uandaaji wa mahitaji ya mabehewa yaliyokuwa yakihitajika ulikuwa dhaifu baada ya Kamati nne za ukaguzi kutumwa nchini India kwa nyakati tofauti, kukagua utengenezaji wa mabehewa hayo na kuendelea kutolewa mapendekezo ya marekebisho ya mahitaji.
Imebainika zabuni zote mbili ikiwamo ya ununuzi wa mabehewa 25 ya mizigo namba PA/113/2012-13/ME/G/OE/013 na mabehewa 274 kwa zabuni namba PA/113/2012-13/ME/G/OE/014, ulifanywa kwa fedha iliyotengwa kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2012/2013 kwa kutumia kanuni na taratibu za Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2004 ambayo ilifutwa na Sheria namba 7 ya 2011.
Pamoja na hayo, zabuni zote mbili zilifanyika kwa njia ya ushindani wa kimataifa na uchunguzi unaeleza kuwa zilitangazwa kwenye magazeti ya ndani pekee, bila hata kutangazwa kwenye gazeti moja la kimataifa kama inavyoelekezwa kwenye Nyongeza ya Kwanza ya Sheria ya Ununuzi wa Umma.
Kutokana na kitendo hicho, ushiriki wa kampuni za nje ulikuwa mdogo kwa kukosa taarifa hizo za tangazo la zabuni. Kutoa tangazo hilo kwenye magazeti ya ndani pekee kulileta matokeo ya wazabuni kumi tu kuwasilisha maombi yao katika kila zabuni.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Waziri wa Uchukuzi, Samwel Sitta, alimsimamisha kazi kwa muda Mkurugenzi Mtendaji wa TRL, Kipallo Kisamfu, na watumishi wengine wanne baada ya kuhusishwa na ununuzi wa mabehewa mabovu 274 na kuisababishia kampuni hasara ya sh 230 bilioni.
Wengine waliosimamishwa kazi TRL kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yao ni Mkurugenzi Mkuu wa Ndani wa Kampuni hiyo, Jasper Kisiraga, Meneja Mkuu wa Manunuzi, Ferdinand Soka, Mhasibu Mkuu, Mbaraka Mchopa, na Mhandisi Mkuu wa Mitambo, Ngosomwile Ngosomiles.