Ardhi ni kichomi
ARDHI
601. Tanzania ina eneo la Kilomita za mraba 942,000. Kati ya hizo kilomita za mraba 888,578 ni eneo la ardhi. Idadi ya watu kwa kilomita ni ndogo isipokuwa kwa maeneo machache kama Wilaya za Ukerewe, Rungwe, Lushoto, Moshi, Arumeru na Bukoba ambapo idadi ya watu kwa kilomita ya mraba inafikia au kuzidi 230.
Inakadiriwa kwamba asiliami 75 ya eneo haikaliwi kutokana na matatizo ya mazingira, mbung’o na ukame. Kiasi cha kilomita za mraba 407,578 ni misitu na vichaka. Kilomita za mraba 487,100 ni za ardhi nzuri inayofaa kwa kilimo na makazi ya binadamu.
Ardhi iliyoko chini ya kilimo ni asilimia 10.1 tu kati ya eneo hilo asilimia 93.4 au kilomita za mraba 46,000 intumiwa na wakulima wadogo wadogo chini ya taratibu za kimila (Customary Tenure) na asilimia 6.6 inatumika kwa kilimo cha mashamba makubwa yenye hati miliki.
Ijapokuwa kilomita za mraba 611.238 au asilimia 69 ya eneo lote zinaweza kutumika kwa shughuli za ufugaji ni kilomita za mraba 438,700 tu zinazotumika kwa sasa. Kwa kuwa ni kilomita za mraba 487,100 tu zinzoweza kutumika kwa ajili kilimo na makazi ya binadamu, kumekuwepo na msukumo mkubwa wa matumizi ya ardhi hiyo kutokana na ongezeko la watu, kupanuka kwa kilimo pamoja na ufugaji.
Baadhi ya makabila yenye mifugo mingi yamekuwa yanarandaranda nchi nzima na imefikia hatua ambapo ng’ombe wanatoka mkoa wa Mwanza hadi bonde la Usangu mkoani Mbeya kutafuta malisho. Miji nayo imeendelea kukua kwa kasi kubwa kutokana na watu wengi kuhamia mijini (Rural Urban Migration).
Kasi hii imesababisha mahitaji makubwa ya viwanja kiasi kwamba watu wengi wanalazimika kutumia mbinu mbali mbali ikiwemo ya kutoa rushwa ili waweze kupata viwanja.
602. Kwa muda mrefu Taifa halijawahi kuwa na Sera ya Ardhi yenye kuonyesha wazi wazi mgawanyo wa Matumizi ya Ardhi kwa nchi nzima. Mnamo mwaka 1991 Serikali iliteua Tume iliyoongozwa na Prof. Issa Shavji kuandaa Sera ya Ardhi na kuiwasilisha serikalini. Sera hiyo imekubalika lakini mpaka sasa haijaanza kutekelezwa. Kutokana na hali hii watu wamekuwa wanaanzisha ujenzi, mashamba na malisho kiholela tu.
603. Historia ya matumizi ya ardhi na sheria zinazohusika na matumizi hayo ni kama historia ya kawaida ya nchi yetu. Matumizi ya ardhi kabla ya kufika kwa wakoloni yalikuwa yanatofautiana katika sehemu moja hadi nyingine kulingana na shughuli za uchumi, siasa na maisha ya watu hadi nyingine hulingana na shughuli za uchumi, siasa na maisha ya watu wa sehemu hiyo.
Matumizi hayo yalifuata mila na desturi za kila sehemu ambazo pia zilitegemea kiwango cha maendeleo ya sehemu hizo. Utawala wa Kiarabu katika pwani ya nchi yetu pamoja na Zanzibar haukubalidilisha sana matumizi ya ardhi. Mabadiliko makubwa katika usimamizi wa matumizi ya ardhi yaliletwa na Serikali ya Kijerumani.
Mnamo mwaka 1895, Wajerumani kwa kutumia Imperial Decree walitwaa ardhi yote ya iliyokuwa Tanganyika (Deutch – East – Africa). Decree hiyo iliyojulikana kama Creation, Acquisition and Conveyance of Crown Land of 1895 ilitwaa ardhi yote na kuiweka mikononi mwa Mfalme na Gavana ndiye aliyekuwa na mamlaka ya kugawa ardhi hiyo kwa matumizi.
Chini ya decree hio Wazawa (Natives) hwakuruhusiwa kuuza zaidi ya hekta moja ya ardhi kwa wageni bila ya kupata kibali kutoka kwa Gavana. Decree hiyo ilisimamiwa ipasavyo na hakuna kumbukumbu yeyote ya kuonyesha kwamba iliwahi kuvunjwa. Sheria hii ilikuwa na shabaha ya kulinda wazawa katika miliki ya ardhi.
Utawala wa Mwingereza ulirithi utawala wa Wajerumani baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia (1914-1918). Mnamo mwaka 1923 walitunga sheria ya ardhi (Land Ordinance, Cap 113) ambayo inatumika hadi sasa. Sheria hio ilikuwa na misingi mikubwa mitatu nayo ni:-
(i) Watu walianza kupewa hati za kumiliki ardhi, jambo ambalo lilikuwa geni kwa wananchi.
(ii) Milliki ya ardhi kwa kufuata mila na desturi ya wazawa ilitambulika (yaani Customary Land Tenure).
(iii) Ardhi yote katika Tanganyika iliyokaliwa na mtu yeyote au ni pori iliwekwa mikononi mwa Umma.
Pamoja na kupitisha sheria hiyo Waingereza walitunga sheria nyingine ya kuuza ardhi, yaani Land (property and conveyancing) Ordinance Cap 334. Sheria zote hizi bado zinatumika na zimekuwa zinafanyiwa marekebisho madogo madogo kila inapobidi. Ingawa Serikali ya Kikoloni ilikuja na sera ya kufanya ardhi kuwa mali inayoweza kuuzika kama mali nyingine yoyote katika uchumi unaotegemea mitaji, bado waliwalinda wazawa (Natives).
Wazawa ndiyo pekee waliruhusiwa kamiliki ardhi chini ya Customary Land Tenure na kwa kutumia Hati Sheria iliwazuia wazawa kuuza ardhi. Taratibu za ardhi (Land regulations) za 1948 zilitilia mkazo jambo hili na zilitafsiriwa kuwa mtu wa Tanganyika ni mtu asiye na asili ya Bara la Ulaya, Asia na ambaye sio Msomali.
Waswahili ambao ni matokeo ya ndoa kati ya wazawa na Waarabu waliwekwa kundi moja na wazawa. Tanzania huru ilirithi sheria zote hizi wakati wa kupata uhuru mwaka 1961. Marekebisho ya kwanza katika sheria ya ardhi yalifanyika mwaka 1969 ambapo miliki ya ‘freehold’ ilifutwa na ‘right of occupancy’ ikaanza kutumika.
Sheria hiyo ilitawaliwa na sera ya ardhi kwa mtumiaji (Land to the Tiller). Katika miliki ya Freehold mwenye ardhi hakupewa masharti yeyote na ardhi ilikuwa mali yake (awe anaitumia kwa mema au mabaya), alikuwa na haki ya kuigawa anavyotaka bila ya kuingiiliwa na dola na asingeweza kunyang’anywa ardhi hiyo kwa vyovyote vile.
Utaratibu wa miliki ulioletwa na marekebisho ya 1969 na kama ifuatavyo:-
(i) Kwamba miliki hiyo ni ya muda maalum. Miliki itakuwa kwa vipindi vifupi na virefu na kwa vyovyote vile muda wa mwisho ni miaka 99.
(ii) Katika hati ambayo itatolewa kuna masharti maalum kwa anayepewa.
(iii) Mtu anayemilkishwa ardhi hawezi kuigawa ardhi hiyo. Kuiweka reheni (Mortagage) bila kibali cha Kamishna wa Ardhi.
(iv) Mwenye miliki atawajibika kulipa kodi ya kiwanja serikalini.
(v) Miliki hiyo inaweza kufutwa na Rais kama Rais ataridhika kwamba mmilikaji amekiuka masharti au kama ardhi hiyo inahitajika kwa manufaa ya umma kwa mujibu wa sheria ya Land Acquisition Act No. 47/1967 iliyotungwa rasmi kwa ajili hiyo.
604. Sekta ya Ardhi imetwaliwa na Sheria Kuu ya Ardhi ya mwaka 1923 (Land Ordinance Cap 113 of 1923). Sambamba na sheria hii kuna sheria nyingine zaidi ya 30 zinazoshughulikia na mambo ya Ardhi na hazieleweki kwa urahisi katika mazingira yetu. Mathalan kuna Fisheries Act of 1970, Forestry Ordinance of 1964 [na] Land Acquisition Act of 1967.
Land (Property and Converyancing) Ordinance of 1923, Land Registration Ordninance of 1953, Land Survey Ordinance of 1957, Local Government (District Authorities) Act of 1982, Local Government (Urban Authorities) Act of 1983, National Investment (Promotion and Protection) Act of 1990 [na] National Land Use Planning Commission Atc 1984.
[Nyingine ni] National Parks Ordinance of 1959, Ngorongoro Conservation Atc 1959, Petroleum (Exploration and Profuction) Act of 1980, Professional Surveyors (Registration) Act of 1977, Public Lands (Preserved Areas) Ordinance of 1954, Range Development and Management Act of 1964, Registration of Documents Ordinance of 1923, Right of Occupancy Act of 1963.
Rural Farm Land (Acquisition and Regrant) Act of 1966, Rural Land (Planning and Utilization) Act of 1973, Town and Country Planning Ordinance of 1956, Urban Leaseholds Act of 1968, Wildlife Conservational Act of 1971, Capital Development Authority Order of 1973, Land Regulation Act of 1948, Local Customary Law Act of 1963 na Township (Bulding) Rules of 1931.
605. Kuna aina mbili za kumiliki Ardhi hapa nchini:
(i) Miliki chini ya Sheria za Kimila (Customary Land Tenure), Mfumo huu umeenea sehemu za vijijini na mara nyingi ukubwa wa eneo unajulikana kwa kutumia mipaka ya asili.
(ii) Miliki ya ardhi kwa Hati Miliki (Right of Occupancy). Ardhi hii huwa inapimwa kitaalam (Cadastal and Aerial Surveys) na kumilikishwa kwa muda wa miaka 33 au 66 au 99.
606. Baada ya kuanzishwa kwa Serikali za Mitaa kulizuka mvutano baina ya Wizara ya Ardhi na Wizara ya Serikali za Mitaa kuhusu mamlaka kugawa ardhi katika maeneo ya miji. Ili kupata suluhu ya mvutano huu, mwaka 1989 Ofisi ya Waziri Mkuu ilitoa mwongozo ambao uliunda Kamati za kugawa ardhi katika ngazi za Wilaya, Mikoa na Wizara. Kila kamati imewekewa viwango vya ukubwa wa ardhi inayoweza kugawa mjini na vijijini.
607. Kundi la miliki ya Ardhi kwa Hati miliki ndilo lenye matatizo mengi yanayosababisha mianya ya rushwa. Hii ni kwa sababu eneo la ardhi hupimwa na kumilikishwa kwa mtu mmoja mmoja, taasisi, shirika, chama au kampuni kwa muda maalum. Ili kazi hii iweze kutendeka maeneo yanayotakiwa kugawanywa kwa wateja kama mashamba au viwanja yanabidi kupimwa kitaalam.
608. Kwa bahati mbaya, upimaji wa viwanja haujawahi kwenda sambamba na mahitaji ya viwanja kutokana na uhaba wa wataalam, ufinyu wa bajeti za mamlaka zinazohusika pamoja na kukosekana kwa dhamira ya serikali kuipa kipaumbele sekta ya ardhi nchini.
Kila mwaka kuna maombi mengi kuliko viwanja, jambo ambalo limesababisha wale wachache waliokabidhiwa dhamana ya kusimamia kutawala na kuendeleza ardhi kushawishika kukiuka kanuni na taratibu za utendaji kazi zilizowekwa kwa manufaa yao.
Baadhi ya matajiri na watu wenye madaraka wameweza kuvamia na kujenga katika maeneo yaliyotengwa mahsusi kwa shughuli za huduma za jamii kama za kidini, shule, zahanati, soko, makaburi na burudani.
609. Uhaba wa viwanja umelazimisha wananchi wengi kujenga katika mabonde na kuvamia maeneo ambayo bado hayajapimwa au ambayo ni ya wazi. Wananchi wengi wanaokosa viwanja wameamua kutafuta maeneo yaliyo kando kando ya miji (periphery areas) na ambayo hajapimwa na kujenga majumba, na mara nyingine majumba ya kifahari kiasi kwamba itakuwa vigumu kuyabomoa wakati itakapobidi kupima viwanja katika maeneo hayo.
Utaratibu huu holela wa upanuzi wa miji yetu (Lateral Unplanned Expansion) unasababisha gharama za kutoa huduma muhimu kama maji, umeme na barabara kuwa kubwa sana.
610. Kwa kuwa madhumuni ya taarifa hii ni kubaini maeneo sugu ya rushwa yanayozua kero kwa wananchi na kuipa Serikali sura isiyostahili Tume imeridhika kwamba umilikaji wa ardhi katika maeneo ya miji ndilo eneo ambalo litahitaji ufumbuzi wa haraka.
Chini ya ‘Town and Country Planning Ordinance’ ya mwaka 1956, Waziri anayeshughulikia mambo ya Ardhi anayo mamlaka ya kutangaza eneo la ardhi kuwa ‘planning area’. Waziri akishatangaza hivyo, inabidi mpango kabambe wa eneo uandaliwe na lipimwe kwa ajili ya viwanja na mwishowe kupewa vibali vya ujenzi wa nyumba katika viwanja hivyo. Utaratibu unaotakiwa kufuatwa katika kila ngazi ni kama ifuatavyo:
UTARATIBU WA UPIMAJI NA MATAYARISHO YA RAMANI
611. Ardhi au kiwanja hupimwa baada ya michoro iliyotayarishwa na Idara ya Upimaji na Ramani kuidhinishwa na Mkurugenzi wa Mipango Miji kwa kushauriana na Kamishna wa Ardhi. Michoro ya viwanja hutayarishwa kwa kuzingatia picha zilizopigwa kutoka angani za maeneo yanayohusika. Kisheria michoro yote ya viwanja katika miji inapaswa kuzingatia majumuisho ya ‘Master Plans’ amnbayo ndiyo michoro ya msingi wa maeneo yanayohusika.
MIPANGO YA MATUMIZI YA ARDHI
612. Chini ya Sheria ya Mipango ya Miji na Vijiji Sura 378, mamlaka zinazoruhusiwa kutoa michoro yaani Halmashauri na Wizara ya Ardhi, lazima zitayarishe michoro ya viwanja kufuatana na mpangilio wa Mpango Kabambe (Master plan) wa eneo linalohusika. Michoro ya Halmashauri hupelekwa kwa Afisa Mipanngo Miji na Afisa Ardhi wa Miji au Mkoa ambaye huipeleka kwa Mkurugenzi wa Mipango Miji.
Taratibu za Upimaji
613. Kutokana na maelezo yaliyotangulia, kama taratibu zitazingatiwa ipasavyo, hakuna kiwanja chochote kitakachopimwa bila idhini ya Mkurugenzi wa Mipango Miji.
614. Baada ya Mkurugenzi wa Mipango Miji kuridhika na mchoro huupeleka kwa Kamishna wa Ardhi ambaye kama naye ataridhika basi mchoro huo hupelekwa kwa Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani ili aendelee na taratibu za kupima eneo linalohusika.
615. Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani hutoa maelekezo kwa maofisa wa Upimaji wa Mikoa au Jiji kuendelea na upimaji. Wakati wa kupima, taarifa za upimaji wa maeneo yaliyopakana na kiwanja kinachopimwa huwa ni muhimu kujulikana. Gharama za upimaji nazo pia huwekwa bayana.
616. Endapo wakati wa kupima, mpimaji atakuta hali halisi kwenye ardhi ni tofoauti na mchoro mpimaji ataangalia ukubwa wa tofauti na marekebisho. Endapo tofauti ni kubwa mpimaji hulazimika kurudisha mchoro kwa Mkurugenzi wa Mipango Miji pamoja na vielelezo ili kufanya marekebisho.
617. Kazi ya kupima ikimalizika inapelekwa kwa Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani ikiwa na kumbukumbu zifuatazo:
(i)Maombi ya kutaka eneo lipimwe na idhini aliyotoa Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani.
(ii)Maelezo ya chanzo cha hesabu zilizotumika (Datum Points).
(iii)Namba ya “Town Planning Drawing” iliyotumika na usahihi wake;
(iv)Uthibitisho wa kuonyesha kwamba mwombaji ardhi au Afisa Ardhi ameonyeshwa mipaka ya ardhi na kwamba ameweka saini kwenye “Beacon Certificate (BC).”
(v)Kuwepo na uthibitisho kwenye “Beacon Certificate” kwamba mawe ya mpaka yamewekwa.
(vi) Uthibitisho kwamba upimaji umefuata sheria zilizopo.
618. Mkurugenzi wa Upimaji wa Ramani akiridhika na upimaji uliofanywa huzipa namba ramani hizo na kuweka saini na muhuri wake. Aidha anatengeneza nakala sita (6) za ramani ambazo hupewa namba. Nakala hizo husambazwa kwa Kamishna wa Ardhi, Mkurugenzi wa Mipango Miji, Afisa Ardhi wa Wilaya au Mji. Msajili wa Hati na nyingine anaihifadhi kwenye Maktaba ya “Approved Registered Survey Plans.”
619. Hatua ya mwisho ni kwa Kurugenzi ya Upimaji na Ramani kutayarisha “Deed Plans” nakala tatu kwa kila kiwanja kilichokubaliwa (Registered Survery Plan) na kukzipeleka kwa mamlaka za kutengeneza Hati za Kumiliki Ardhi (Mkoa au Jiji) ili wakamilishe taratibu za kutengeneza hati ya kumiliki ardhi.
MAONI
620. Idara ya Upimaji na Ramani na Maendeleo Mijini zimekuwa zinakabiliwa na matatizo mengi ambayo baadhi yake ni:-
(i) Sheria inayosimamia Upimaji na Ramani – Sura 390 ni ya mwaka 1957. Sheria ya Mipango ya Miji 378 ni ya mwaka 1956. Pamoja na marekebisho yaliyokwishafanywa bado zinahitaji kufanyiwa marekebisho zaidi ili zilingane na wakati kwa kuzingatia hali halisi ya mazingira ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.
(ii) Sheria hizi kama sheria nyingine kuu za Ardhi zinagongana na Sheria Na.9 ya 1982 inayosimamia Serikali za Mitaa. Sheria kuu ya mipango Miji (Cap.378), Ardhi (Cap.113) na Usajili wa Ardhi (Cap.334) zimebainisha na kugawa madaraka baina ya Waziri anayeshughulikia na upangaji wa Miji, Kamishna wa Ardhi, Mkurugenzi wa Upimaji wa Ramani na yale ya Halmashauri za Miji.
Sheria Na. 8 ya 1982 imetoa madaraka ya kuidhinisha mipango na michoro ya viwanja mijini kwa Waziri anayehusika na Mamlaka za Miji. Kutokana na migongano ya sheria hizo na kutokuwepo kwa uwazi kuhusu uhusiano wa kiutawala na kiutendaji baina ya vyombo hivi, maamuzi yake nayo yamekuwa yanagongana.
(iii) Kwa mujibu wa sheria ya Mipango Miji Cap. 378, Halmashauri ya Jiji, Manispaa, Miji na Wilaya zina mamlaka ya kuandaa na kutekeleza Mipango ya Matumizi ya Ardhi katika maeneo ya Miji vile vile, Halmashauri za Miji ndizo zenye madaraka ya kudhibiti uendelezaji wa Ardhi katika maeneo ya Miji yao. Ukweli ni kwamba Halmashauri za Miji na hasa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeshindwa kutekeleza majukumu iliyonayo ya kupanga matumizi ya ardhi au kuandaa mikakati ya kupima viwanja na badala yake kuingilia shughuli ya ugawaji viwanja.
(iv) Mpango Kabambe wa Jiji la Dar es Salaam uliandaliwa na Wizara ya Ardhi mwaka 1979. Mpango huu unapaswa kufanyiwa marekebisho kila baada ya miaka 10 (kumi). Jambo hili bado halijatekelezwa. Moja ya malengo mkuu ya mradi wa Sustainable Dar es Salaam Project ni kuandaa “Strategic Urban Development Plan” ya Jiji ambayo itachukua nafasi ya Master Plan ya mwaka 1979. Hadi sasa Halmashauri ya Jiji haijaweza kutoa hata rasimu ya kwanza ya mpango huo.
(v) Mapendekezo yote ya mipango ya kuendeleza ardhi kutoka za mijini au mikoani hayana budi kujadiliwa na Kamati za Mipango Miji. Kamati huchelewesha kutoa maoni hayo kwani vikao vya Kamati hizo havifanyiki mara kwa mara. Hatima yake ni kucheleweshwa kuwasilishwa kwa mipango hiyo kwa Waziri wa Ardhi, jambo linalosababisha kuchelewa kupimwa viwanja na kusababisha uvamizi na ujenzi holela.
Eneo la Mbezi Beach Jijini Dar es Salaam ni mfano halisi wa uvamizi huo. Maeneo ambayo Halmashauri ya Jiji imechelewesha maamuzi ya maendeleo ya Mipango Miji ni Kariakoo, Kurasini na katikati ya Jiji. Wizara ya Ardhi iliandaa mipango ya Uendelezaji wa maeneo hayo tangu mwaka 1993.
(vi) Uhaba wa fedha ambao unasababisha ukosefu wa vifaa vya upimaji ardhi, usafiri na fedha za kulipa fidia pia umesababisha ukosefu wa ramani za msingi zenye uwiano wa scale 1: 2,500, 1:5,000 na 1:10,000 kwa zaidi ya miji 90 nchini jambo ambalo linaathiri upangaji wa matumizi ya ardhi mijini.
(vii) Halmashauri za miji na wilaya zinakosa fedha za kutayarisha miundombinu ambayo ni hatua muhimu katika kuendeleza sera za miji kwa mfano barabara, mifereji ya maji machafu n.k.
621. Upimaji ambao umekuwa unafanywa na wapimaji binafsi au wapimaji wa umma, lakini kwa kuajiriwa na watu binafsi kinyume na taratibu zilizowekwa umeongeza migogoro ya ardhi au kuzusha viwanja ambavyo havipo kwenye mipango ya kuendeleza ardhi ya maeneo hayo.
Je, unafahamu Jaji Warioba katika ripoti hii aliyoiandaa mwaka 1996 alipendekeza nini kifanyike kubadili hali hii? Ingawa ripoti hii imeandikwa mwaka 1996, inaendelea kuwa na maudhui yenye uhalisia na yenye kuonyesha upungufu uleule hadi sasa na hivyo inastahili kufanyiwa kazi. Usikose JAMHURI wiki ijayo. Mhariri.