Wafanyabiashara pasua kichwa

 

519. Misamaha ya kodi inayotolewa na IPC imekuwa ikitoa mwanya wa kuvuja kwa mapato ya serikali. Baadhi ya wawekezaji wamekuwa wakiomba misamaha kwa vitu vingi kuliko wanavyohitaji kukamilisha miradi yao. Kwa mfano pale ambapo mwekezaji alihitaji marumaru 10,000 aliomba msamaha wa kodi kwa ajili ya marumaru 20,000 au 30,000.

Vifaa hivyo vikishafika anauza vile vilivyozidi mahitaji yake. Aidha, wengine wanapewa misamaha ya kodi kwa zana au vifaa ambavyo wanavitumia tofauti kabisa na matarajio yaliyokusudiwa.

Kwa mfano ndege na magari yaliyopewa misamaha kwa ajili ya mradi wa Hill Top Hotel ya Kigoma yanatumika kwa shughuli binafsi hapa jijini au kuendeleza miradi mingine inayomilikiwa na wawekezaji hao, lakini haina vibali vya IPC.

Hali hii inatokea pengine kutokana na IPC kutokuwa na ujuzi na utaalam wa kuchambua mahitaji halisi ya miradi hiyo ama uzembe au sababu za kibinafsi. Mfano mzuri umeonyeshwa katika Kiambatisho E.

520. Chini ya Sheria ya Forodha ya 1976, bidhaa zinazoagizwa na Mashirika ya Hisani (Charitable Organisations) zinapata misamaha ya kodi. Utaratibu huu ulikuwa unadhibitika huko zamani wakati Mashirika haya aliyopokuwa machache (mengi yalikuwa ya dini) na yalikuwa yanaleta bidhaa kwa ajili ya manufaa ya wananchi wengi.

Siku hizi kumezuka mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo baada ya kuandikishwa na Wizara ya Mambo ya Ndani nchini yanafaidika na misamaha ya kodi inayotolewa kwa mashirika ya hisani. Ingawa Sheria ya Fedha Na. 2 ya1996 imeeleza bayana kwamba misamaha itatolewa kwa vifaa vya mashirika ya dini vya kuanzisha miradi ya elimu, afya na maji pamoja na vifaa vitakavyonunuliwa na mashirika hayo kwa kutumia fedha za wahisani, kuna haja ya kuwa macho kwa sababu wanaoteuliwa na mashirika hayo kushughulikia mizigo hiyo sio watu wa dini na wanaweza kurubuniwa na wafanyabiashara ili kukwepa kodi.

521.  Katika miaka ya nyuma, baadhi ya waagizaji bidhaa waliruhusiwa kulipa ushuru kwa awamu na kutakiwa kulipa kiasi kidogo tu wakati wa kuondoa mizigo bandarini. Waagizaji wengi walionufaika na utaratibu huu wamekwepa au kushindwa kulipa kodi hizo kama ilivyokubaliwa na hivyo kuikosesha serikali mapato. Pamoja na kwamba Hazina imeshindwa kukusanya malimbikizo ya kodi hizo bado inadiriki kuendeleza utaratibu huu kwa waagizaji wapya.

 

MAPENDEKEZO

 

522. Misamaha yote ya kodi ifanyike katika misingi ya sheria, tofauti na misamaha inayotokana na maamuzi na hisani ya mtu au watu husika (discretionary exemptions). Yaani “discretionary exemptions” zisipewe  nafasi katika utendaji wa Mamlaka mpya ya Mapato. Sheria irekebishwe ili iweke pendekezo hili bayana na mapendekezo ya misamaha ya kodi yafanywe kwanza na Mamlaka ya Mapato.

523. (i) Sheria ya Forodha ya 1976 irekebishwe ili misamaha ya kodi itolewe kwa Mashirika ya Hisani tu. Aidha, sheria iorodheshe bidhaa ambazo zitafaidika na misamaha hiyo.

 (ii)Misamaha ya kodi inayotolewa na Kituo cha Uwekezaji Rasilimali (IPC) izingatie bidhaa halisi zinazohitajika katika utekelezaji wa uwekeazaji unaodhamiriwa na kwa kipindi maalum.

 (iii)IPC ikishapendekeza orodha ya bidhaa zinazotakiwa kusamehewa kodi chini ya sheria ya IPC, Wizara ya Fedha isiongeze tena bidhaa nyingine katika fomu hiyo.

 (iv)IPC ifanye uchambuzi wa kina kuhusu bidhaa au vifaa inavyopendekeza kusamehewa kodi. Pale ambapo inashindwa iwajibike kutafuta utaalam kutoka  vyombo husika ili wawekezaji wapewe misamaha kwa vifaa vile tu vitakavyotumika kwenye miradi.

 (v)Kwa sababu imedhihirika kwamba baadhi ya wawekezaji wamepewa misamaha na kuitumia vibaya chini ya hati ya IPC, Tume inapendekeza kwamba uchambuzi wa kina ufanywe ili kujua wahusika na kiasi cha kodi kilichokwepwa ili kuhakikisha kuwa kodi hiyo inalipwa na hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi yao ikiwa ni pamoja na wale walioorodheshwa katika Kiambatisho E.

 (vi)IPC itakiwe kufuatilia na kuwasilisha taarifa kuhusu utekelezaji wa miradi iliyopewa kibali cha IPC.

 

TATIZO LA MAWAKALA

 524. Watu wengi wanaoagiza bidhaa nje hutumia Kampuni za Uwakala wa kuondoa mizigo bandarini na viwanja vya ndege. (Clearing and  Forwarding Agents). Kampuni hizi zimegawanyika katika makundi matatu yaani:

 (i) Mtu ambaye hana ofisi (Breafcace Agents). Kundi hili linajumuisha wananchi wa kawaida pamoja na watumishi wa Idara ya Forodha.

(ii) Makampuni yaliyoandikishwa chini ya Chama cha Uwakala kuondoa mizigo (Tanzania Association of Forwarding Agents – TAFA).

(iii) Mashirika kwa kutumia watumishi wao kuondoa mizigo bandarini.

 525. Ili makampuni haya yaweze kupata leseni, maombi ya leseni ya Uwakala yanachunguzwa na jopo la Wajumbe kutoka TAFA, Wizara ya Biashara na Viwanda, NASACO, TCFB na Forodha. Kiutaratibu Kamishna wa Forodha anatakiwa kukubali leseni za Uwakala kwa kuzingatia mapendekezo ya jopo hilo. Utaratibu huu umekumbwa na matatizo yafuatayo:

 (i) Katika nyakati tofauti Kamishna amekuwa hazingatii mapendekezo ya jopo hilo na hivyo kuruhusu leseni kutolewa kwa makampuni ambayo kwa mujibu wa jopo hayastahili kupewa leseni.

 (ii) Baadhi ya viongozi wa juu serikalini wamekuwa wanatoa shinikizo kwa Kamishna wa Forodha kumtaka atoe leseni kwa watu ambao wasingestahili kutokana na taarifa zao mbaya machoni mwa idara na jopo.

 Kutokana na hali hiyo biashara ya Uwakala wa kuondoa mizigo bandarini imekuwa kwa kasi sana. Wakati fulani kulikuwa na Wakala zaidi ya 2,000 lakini kwa sasa Idara ya Forodha imewapunguza kufikia 527.

 526. Pamoja na juhudi hizi bado kuna Wakala ambao kwa kushirikiana na watumishi wa idara wanawashughulikia wateja wao kwa kutumia mihuri na risiti bandia za malipo ya ushuru kuondoa mizigo bandarini.

 527. Mawakala wa kuondoa mizigo wamekuwa wanagushi hati za dhamana ya mizigo inayopelekwa nchi jirani na hivyo mizigo hiyo kuuzwa nchini bila ya kulipiwa kodi.

 

MAPENDEKEZO:

 (i) Kamishna wa Forodha awe na mamlaka ya mwisho kuamua idadi ya wakala wa kuondoa mizigo bandarini.

 (ii) Mwombaji yeyote wa Uwakala asipewe lesene bila ya kuzingatia mapendekezo ya Jopo.

 (iii) Mtindo wa viongozi wa Serikali wa kuingilia utendaji kazi wa Mamlaka na Jopo unakwenda kinyume na maadili ya Uongozi na uachwe mara moja.

 (iv) Mamlaka ya Mapato iandae taratibu na kanuni za kuwadhibiti mawakala hao. Kanuni ziweke bayana ‘Code of Conduct’ ya biashara hii pamoja na kuweka hatua kali za kuchukua dhidi ya wakala atakayevunja sheria hii.

 (v) Kampuni yoyote itakayoomba leseni lazima ionyeshe wamilikaji wake, anwani inayokubalika, pamoja na ofisi. Kampuni ambayo wamilikaji wake wana sifa ya uhalifu zisipewe leseni.

 (vi) Kila Kampuni yenye leseni ipewe Namba ambayo itakuwa inaitumia katika kila kadhia itakayoshughulikia.

 (vii) Kila kampuni iwe inatoa hesabu zilizokaguliwa wakati wa kuomba leseni.

 

529. BONDED WAREHOUSES

Eneo lingine lenye mwanya wa rushwa ni “Bonded Warehouses” haya ni maghala maalumu yanayohifadhi mali ambayo haijalipiwa kodi. Mali hairuhusiwi kutoka nje ya maghala haya mpaka ilipiwe kodi. Hata hivyo wenye mali katika maghala haya wamekuwa wakishirikiana na maafisa forodha waliokosa uaminifu na maadili kutoa mali hizo hasa magari bila ya kulipia kodi.

 Serikali imefunga nyingi ya ‘Bonded Warehouses’ ili kuziba mwanya wa uvujaji wa mapato yake. Kwa 100 zilizobakia bado kuna tatizo la uwekaji kumbukumbu pamoja na udhibiti duni unaosababisha mali kutoweka katika maghala. Aidha, baadhi ya maghala haya hayana ubora na usafi wa kuyawezesha kuwa maghala. Mengine yana bidhaa zilizokwishahifadhiwa kwa muda mrefu na wenye maghala hayo kushindwa kulipa ushuru wa bidhaa hizo.

 

530. MAPENDEKEZO:

 (i) Serikali iangalie upya sheria, matumizi na idadi ya ‘bonded warehouses’ nchini ili kurahisisha udhibiti wake.

 

531. KAMPUNI ZA UKAGUZI WA MIZIGO (PRESHIPMENT INSPECTION COMPANIES)

 Kampuni za Ukaguzi wa Mizigo  (PSIs) yanafanya shughuli za ukadiriaji wa kodi kwa mizigo inayozidi thamani ya USD 5000. Makampuni haya yanatumia utaratibu wa ukadiriaji wa World Trade Organisation (WTO) tofauti na ule unaotumiwa na Idara ya Forodha ya Brussels Definition of Value (BDV) na hivyo kufikia viwango tofauti suala ambalo linasababisha mambo yafuatayo:

 (i) Pale ambapo mtumishi wa Idara ya Forodha ni mwaminifu na lazimika kuongeza kodi baada ya ukadiriaji kufanywa na kampuni hizo.

 (ii) Kwa kurubuniwa na mwenye mali mfanyakazi wa idara anaweza kufumbia macho au kuongeza kodi kidogo maadam anapewa rushwa na hivyo kuikosesha serikali mapato.

 Kati ya mwaka wa fedha wa 1994/95 na Januari 1996, Idara ya Forodha imekusanya kodi ya ziada ya Shs. 2.3 bilioni baada ya Tax Assessment Note kutolewa na kampuni hizo. Tazama Kiambatisho F.

 532. Kisheria jukumu la kukusanya mapato ya serikali yatokanayo na kodi ni la Mamlaka ya Mapato Tanzania. Mamlaka kwa kutumia idara zake inatakiwa kuhakikisha kwamba kodi yote inayokadiriwa inalipwa na wateja, kufanya ‘reconciliation’ na benki kuhakikisha kuwa fedha zote zimeingia kwenye mfuko mkuu wa Serikali.

 Chini ya utaratibu wa sasa wa kutumia PSI inakuwa vigumu kubaini kama wote wanaopewa TAN na kampuni hizi wanalipa kodi hizo. Uchambuzi uliofanywa na Tume umebaini kwamba makadirio ya kodi yaliyofanywa na kampuni ya InchCape Testing Services kwa bidhaa mbalimbali zilizoagizwa katika kipindi cha Oktoba 1995 na Januari, 1996 ni Shs. 16.4 bilioni.

Misamaha ya kodi ilifikia Shs 7.1 bilioni sawa na asilimia 43 ya kodi yote. Kati ya kodi ya Shs 9.3 bilioni iliyotakiwa kulipwa ni Shs 4.5 bilioni tu au asilimia 48 iliyolipwa kama inavyoonyeshwa katika Kiambatisho G.

 

534.  MAPENDEKEZO:

(i) Kwa kuwa kisheria jukumu la kukusanya mapato ya serikali ni la Idara ya Forodha, na kwa kuwa PSIs wamepewa jukumu la kukadiria kodi kwa mikataba ya muda maalum kwa kutegemea kwamba Mamlaka ya Mapato itakayoanzishwa itakuwa na uwezo wa kukadiria kodi hizo, mikataba kati ya serikali na kampuni ya Ukaguzi wa Mizigo iangaliwe upya ili bidhaa hizo ziwe zinakaguliwa hapa nchini kabla hazijatoka bandarini – (Post Shipment Inspection). Tume inaamini kwamba huu ni wakati mzuri wa kushirikisha kampuni za Kitanzania au zinazomilikiwa kwa kiasi kikubwa na Watanzania kufanya kazi hii.

(ii) Kwa vile ukaguzi utafanyika hapa nchini, mizigo yote bila kujali thamani yake itakaguliwa na kuondoa ukwepaji kodi wa kusingizia mizigo mingine ni chini ya thamani ya  US$ 5,000 – wakati ni zaidi.

 (iii) Sheria za Uagizaji bidhaa zitazamwe upya ili kuhakikisha kwamba zitakazokataliwa kuingia nchini kwa sababu mbalimbali kama uhalifu wa bidhaa zinarejeshwa zilikotoka kwa gharama za mwagizaji.

 

MATUMIZI YA RISITI BANDIA

535. Tatizo la risiti bandia limeathiri sana mapato ya serikali. Katika zoezi la kulipa kodi ya magari lililofanyika mwaka 1994, imebainika kwamba baadhi ya wenye magari walipewa risiti bandia katika vituo vya Idara ya Mapato. Aidha, katika msako uliofanywa katika Jiji la Dar es Salaam mihuri bandia kadhaa ilikamatwa. Tatizo hili limeenea hadi Idara ya Forodha ambapo baadhi ya watu kwa kushirikiana na watumishi wa Idara ya Forodha hasa Watunza Fedha wanatumia risiti bandia zinazochapishwa hapa nchini kuondoa mizigo bandarini.

 

536.  MAPENDEKEZO:

 (i) Serikali iimarishe sehemu ya Security Printing ya Idara ya Mchapaji Mkuu wa Serikali ili kumpa uwezo wa kuchapa nyaraka nyeti za Serikali. Watumishi watakaofanya kazi katika sehemu hii wawe wamepekuliwa (vetted) na wapewe vivutio kuwaondolea vishawishi vya kutoa nje nyaraka hizo.

 (ii) Ili kudhibiti viwanda vya uchapaji hapa nchini serikali iandae sera itakayoweka maadili ya sekta hii. Hii ni pamoja na kuweka adhabu kali kwa wenye viwanda vitakavyochapa nyaraka za serikali bila idhini.

 (iii) Vyombo vya dola vichukue hatua za makusudi za kutokomeza tatizo hili.

 

IDARA YA KODI ZA MAUZO NA KODI ZA NDANI

 537. Idara hii ilianzishwa mwaka 1976 chini ya Sheria Na. 13 ya mwaka 1996 (Sales Tax Act No. 13 of 1976). Jukumu la Idara hii ni kukusanya na kuhasibu kodi za serikali katika mfumo wa ‘Indirect Taxation.’ Chini ya mfumo huu kodi inalipwa na mteja baada ya kupatiwa mali au huduma inayotozwa kodi kwa mujibu wa sheria.

  538. Idara inaongozwa na Kamishna akisaidiwa na Kamishna Msaidizi wanaoongoza sehemu za shughuli (Operations). Ukaguzi na Upelelezi (Audit and Investigation), Utafiti wa Sera na Ufuatiliaji wa Mapato (Policy Research and Revenue Monitoring). Idara ina Kanda 3 zifuatazo:

 Kanda A: – Dar es Salaam

Kanda B:  – Arusha, Mwanza, Tanga, Kilimanjaro, Morogoro, Dodoma, Kigoma,

Iringa, Mbeya, Mara, Kagera na Shinyanga.

 Kanda C: – Ruvuma, Mtwara, Tabora, Singida, Rukwa, Pwani na Lindi.

 

Idara ina ofisi katika kila mkoa na wilaya Tanzania Bara.

 Taratibu za Ukusanyaji kodi

 539. Ukusanyaji wa Kodi ya Mauzo na Kodi za Ndani umegawanyika katika makundi matatu ambayo ni:

 (i) Zinazokusanywa kila mwisho wa mwezi.

(ii) Zinazokusanywa wakati inaobidi kwa mfano leseni za biashara, kodi za viwanja n.k.

(iii) Zinazokusanywa mipakani kwa mfano Transit Charges, Airport na Port Charges.

 

Kodi kutoka bidhaa zinazotengenezwa nchini:

 540. Ukusanyaji wa Kodi ya Mauzo unafanyika kwa kuwaweka maafisa wakazi (Resident Officers) katika viwanda vinavyotengeneza bidhaa hizo. Maafisa hawa wanaangalia malighafi inayoingia katika viwanda hivyo na kutumia utaalamu wao wanajua ni bidhaa kiasi gani zitakazotengenezwa. Maafisa hawa hupiga hesabu ya kodi ya mauzo kwa bidhaa zilizouzwa na mwenye kiwanda kutakiwa kulipa kodi hiyo. Mfumo wa Indirect Taxation unahitaji uaminifu na uadilifu wa hali ya juu miongoni mwa watumisi wa Idara na walipa kodi amabo ndio wanatoa taarifa za mali na huduma waliyozalisha au kutoa.

 541. Kwa hiyo utaratibu huu una kasoro au matatizo yafuatayo:

 (i) Wenye viwanda wakati mwingine wanakuwa wadanganyifu na kutoonyesha idadi kamili ya bidhaa walizotengeneza na walizouza kwa Maafisa Wakazi wa Idara na hivyo kukwepa kulipa kodi. Hali hii inatokana na ukweli kwamba Afisa Mkazi anafanya kazi kwa zile saa za mfanyakazi wa serikali wakati kiwanda kinaweza kuendelea kuzalisha hata wakati wa usiku. Aidha, wanaweza kuendelea na mauzo hata baada ya Afisa wa Kodi kuondoka.

 (ii) Maafisa Wakazi (Resident Officers) ni watumishi ambao walikuwa wanalipwa mishahara midogo sana. Kutokana na makali ya maisha wanakula njama na wenye viwanda na kupewa rushwa ili  waandike idadi ndogo ya bidhaa iliyouzwa na hivyo kumfanya mwenye kiwanda kulipa kodi ndogo.

 Aidha, watumishi hawa hawana hata usafiri. Yanayotokea ni kwamba kila siku baadhi ya wenye viwanda wanatoa usafiri kwa maafisa hawa kwenda kiwandani na kurudi nyumbani. Maafisa hawa wamekuwa kama waajiriwa na wenye viwanda na pale ambapo mzalishaji anakwenda kulipa kodi wamekuwa wanafumbia macho kwa kuogopa kukosa fadhila.

 (iii) Sheria ya Sales Tax inamtaka mwenye kiwanda auze mali yake ndipo alipe kodi. Chini ya sheria hii hakuna kipengele kinachomzuia mwenye kiwanda kusimamisha utengenezaji kama hajalipa kodi.  Kwa maana nyingine ni kwamba hakuna ‘automaticity’ katika sheria hii. Matokeo yake ni kwamba baadhi ya viwanda vimelimbikiza madeni makubwa ya kodi ya mauzo na hivyo kuinyima serikali mapato.

 (iv) Baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu wamekuwa wananunua mali kutoka viwandani na kudanganya kwamba wanasafirisha kwenda nchi jirani (Exporters). Bidhaa hizo zimekuwa zinauzwa humu nchini na hivyo kutolipiwa kodi ya mapato. Kwa mfano Mr. Henry Ssenoga wa t/a Agro Links ya Uganda alinunua Konyagi kwa ajili ya ya kupeleka Uganda lakini aliuza humu nchini na kuikosesha serikali kodi ya Shs. 65,358,000/-.  Kesi hii iko Mahakama Kuu ya Rufaa. Bas-Iteh Co. Ltd, ilinunua Konyagi na kuziuza humu nchini na kuikosesha serikali Shs. 43,572,000/-. Kampuni hii ilishtakiwa na kulipa fedha hizo.

 (v) Baadhi ya walipa kodi wanakula njama na maafisa wa Idara na kutoa stakabadhi bandia kama ushahidi wa kulipa kodi. Wengine hata bila ya kufika katika Ofisi za Idara hupeana fedha popote pale dhidi ya hizo stakabadhi bandia na baadaye kuzionyesha kwa mlipa kodi aliyewatuma kama ushuhudi kamili wa kodi iliyolipwa.

 Hali hii imejitokeza kutokana na kuvurugika kwa mfumo wa zamani wa kudhibiti vitabu vya stakabadhi za serikali kwa upande mmoja na kuzuka kwa wachapaji wa risiti bandia kwa upande mwingine. Chini ya utaratibu wa zamani kila ofisa wa kukusanya kodi alikuwa anapewa kitabu cha stakabadhi ambacho alitakiwa kila mwisho wa mwezi kurejesha vitabu hivyo vikionyesha vishina vilivyotumika na risiti zote ambazo hazikutumika kwa ajili ya ukaguzi ili kudhibiti matumizi yake.

 (vi) Baadhi ya Watunza Fedha katika vituo vya Idara wamekuwa wanaiba fedha zinazolipwa na wateja kwa njia ya ‘carbon slipiping.’ Mwenye kulipa kodi anapewa stakabadhi inayoonyesha kiasi halali alicholipa lakini haweki ‘carbon paper’ anapoandika risiti hiyo. Baadaye mtunza fedha anakuja kuandika katika nakala ya risiti hiyo kiasi kidogo kuliko kile alicholipa mteja na kuchukua tofauti inayojitokeza.

Aidha, wengine wanakuwa na kitabu cha risiti bandia na wale wateja wenye kulipa fedha nyingi hupatiwa risiti hizo. Kodi zinazohusishwa mara nyingi ni zile ndogo zisizokuwa na rejesta kamili kwa mfano Stamp Duty, Driving Licence, Transfer Tax, Registration Tax, n.k.

 (vii) Baadhi ya wenye viwanda nchini wamekuwa wananunua bidhaa chini ya

Registered Dealers Certificate. Chini ya utaratibu huu bidhaa inayonunuliwa hutumika kama malighafi (Law materials) kwa mfano sukari katika utengenezaji wa mikate na bia na hawatakiwi kulipa kodi ya mauzo. Wafanyabiashara hawa wamekuwa wanauza bidhaa hizo badala ya kuzitumia kama malighafi na hivyo kukwepa kulipa kodi.

(viii)      Eneo lingine ni stakabadhi kutotolewa na wauza mali au huduma kama inavyotakiwa chini ya Sheria ya Ushuru na stempu ya mwaka 1972. Chini ya sheria hii muuzaji anatakiwa kutoa stakabadhi sahihi ya kiasi cha fedha anazopokea na mnunuzi naye anatakiwa ahakikishe amepewa stakabadhi hiyo. Sheria hii imekuwa inakiukwa na hivyo kukosesha serikali mapato.

 Aidha, Maafisa wa Idara ambao mara kwa mara wamekuwa wanafuatilia wanaokiuka sheria hii wamekuwa wanapewa chochote ili wasiwachukulie hatua za kisheria. Tatizo moja kubwa hapa ni kwamba kila mfanyabiashara ana kitabu chake cha stakabadhi. Bado hatuna utaratibu wakuwapa wauzaji hawa vitabu maalum vya serikali (Standardised Documentation System). Kwa hiyo hata kama wauzaji wote watatoa stakabadhi haitakuwa rahisi kuweza kufanya ukaguzi wa vitabu hivyo kwa sababu vingi vitakuwa vimefichwa.

 

Je, unafahamu Jaji Warioba katika ripoti hii aliyoiandaa mwaka 1996 alipendekeza ni hatua zipi zichukuliwe? Ingawa ripoti hii imeandikwa mwaka 1996, inaendelea kuwa na maudhui yenye uhalisia na yenye kuonyesha upungufu ule ule hadi sasa na hivyo inastahili kufanyiwa kazi. Usikose JAMHURI wiki ijayo. Mhariri.