Kaula, Dk. Mlingwa, rushwa ‘iliwapofusha’

 

Zabuni hizo zilipokelewa na kufunguliwa katika ofisi za Halmashauri Kuu ya Zabuni tarehe 26 Juni, 1991 na baadaye kukabidhiwa Wizara ya Ujenzi kwa uchambuzi na tathmini. Zabuni zilifanyiwa uchambuzi na tathmini na wahandisi wa Wizara.

Taarifa ya kamati hiyo ilipendekezwa kuwa “Package” Na. 9 ya barabara ya Pugu- Chanika- Mbagala itolewe kwa kampuni ya UNICO Ltd. Kwa misingi ya gharama zao kuwa nafuu kuliko makampuni mengine yaliyouzabuni mradi huo. Mapendekezo hayo yamo katika dondoo za mkutano wa kamati uliofanyika tarehe 20 Septemba, 1991.

 Hata hivyo nyuma tarehe 23/7/91, katika dokezo alilomwandikia Waziri wa Ujenzi, Katibu Mkuu aliandika hivi (pamoja na mambo mengine)

 “WU

 ADUCO

 Kampuni ya ADUCO ni mojawapo ya makampuni yaliyozabuni miradi ya barabara za Dar es Salaam.  Hivyo, hutokana na zabuni hizi itaonekana kuwa zabuni za ADUCO ziko juu zaidi ya wazabuni wote. Katika hali hii, inakuwa vigumu kusaidia.

 Nawasilisha kwa maelekezo yako zaidi”.

 Tarehe hiyo hiyo, Waziri alimjibu Katibu Mkuu kwamba:

 “Tufanye kazi kwa misingi. Wale ambao figures zao zipo juu sana.”

 Mkutano uliofanyika tarehe 16 Oktoba, 1991 kujadili mapendekezo ya kamati iliyochambua na kutathmini zabuni na ulioongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara uliyakataa mapendekezo ya Kamati na kupendekeza kandarasi ya barabara ya Pugu- Chanika- Mbagala ipewe kampuni ya ADUCO INT. B.V. :

 “The meeting recommends award of contract for Package No. 9 to M/s ADUCO B.V subject to the sum to an acceptable amount and reduce their proposed completion period from 510 calendar days to an acceptable contract period.”

Kumbukumbu zilizopatikana zimeeleza kwamba hatimaye mapendekezo haya yaliwasilishwa Benki ya Dunia na kwenye Halmashauri Kuu ya Zabuni mwezi Novemba, 1991 kwa ajili ya uamuzi na kibali cha utekelezaji. Benki ya Dunia na Halmashauri Kuu ya Zabuni waliidhinisha utekelezaji wa mapendekezo hayo na kuipa Wizara kibali cha kuingia mkataba na kampuni ya ADUCO INT. B.V.

Kufuatia kibali hicho, Wizara ya Ujenzi kwa barua Kumb. Na. MOW/M.30/384/H/1 iliikaribisha rasmi kampuni ya ADUCO INT. B.V. kufanya nao majadiliano ya kufikia mkataba. Wizara ya Ujenzi ilikuwa na hoja ambazo iliziona kuwa za msingi zilizohusu muda wa kumalizika kwa kazi na ziada ya gharama, miongoni mwa mengine.

Katika barua yao ya tarehe 16 Januari, 1992 yenye Kumb. Na. PN/TZ/0153 kampuni ya ADUCO ilikataa kupunguza muda lakini wakakubali kurekebisha gharama ya zabuni yao kwa punguzo la kati ya Tshs. 15m/= na 20m/= badala ya Tshs.56m/= zilizotakiwa zipunguzwe na kamati ya wataalam ya Wizara ya Ujenzi.

 Katika dokezo kwa Katibu Mkuu la tarehe 16/1/1992 aliyekuwa kiongozi wa kamati ya Wizara iliyosimamia majadiliano na mkandarasi aliandika kumtaarifu Katibu Mkuu msimamo wa ADUCO kwa kupunguza Tshs. 15m/- hadi 20m/- badala ya Tshs. 56m/- na kwamba:

 “We are stalemated. The Committee recommends that ADUCO/CSI he given an ultimatum of two days to complete the negotiations with a reduction of not less than Tshs. 56m/- failure of which shall warrant tender negotiations with other bidders.”

 Kufuatia taarifa na mapendekezo hayo, Katibu Mkuu alimwandikia Waziri wa Ujenzi kwa dokezo la tarehe 29/1/92 kwamba:

“Naambatisha taarifa kuhusu majadiliano kati ya Wizara na ADUCO kuhusu Mradi wa Pugu-Chanika-Kongowe. Kwa kifupi taarifa inapendekeza kuwa kutokana na ADUCO kushindwa kuteremsha gharama zake za preliminaries pamoja na kukataa kupunguza muda kutoka miezi 17 hadi 13 ya ujenzi inapendekezwa kuwa mazungumzo na mkandarasi huyo yavunjike na tutafute mkandarasi mwingine.

“Hata hivyo nilikuwa na ushauri ufuatao:

ADUCO walifika ofisini kwangu jana na kueleza kuwa wako tayari kupunguza muda kutoka miezi 17 hadi miezi 14 lakini wasingependa kupunguza bei zitokanazo na kupunguka kwa muda wa ujenzi. Pengine ni vyema ukawaita na kuzungumza nao umuhimu wa kujenga mradi huu katika muda mfupi na katika gharama zinazokubalika. Kama watakubali kupunguza muda hadi kufikia miezi 14 na kupunguza gharama kulingana na muda ni vyema tukawafikiria kuwapa mradi huu.”

 Akijibu dokezo la Katibu Mkuu, tarehe 29/1/92 Waziri wa Ujenzi aliandika, miongoni mwa maneno mengine, kwamba:

 “Tangu negotions (sic) zianze niliwahi kudokeza katika mazungumzo kuwa Contracts Section yetu ipo predicided (sic) kutokumpa ADUCO (sic) kazi hii pamoja na sababu nyingine zinazoweza kuwa za msingi lakini siyo za muhimu. Arrogance towards Contractors dominates the behaviour ya uongozi wa sehemu ya Mikataba. Contractors wengi wameeleza hili pamoja na vielelezo.”

 Aidha katika aya ingine ya dokezo hili, Waziri alimwagiza Katibu Mkuu hivi;

 “In view of the above (1-3) waite ADUCO tuwekeane (Wizara) (sic) nao kwa kupunguza Shs. 35m/- kama walivyoahidi na kupunguza muda wakazi mpaka miezi kumi na nne (14) bila kupunguza gharama kulingana na muda kwani muda wa mvua wa karibu miezi 1 ½ kazi hazitafanyia.”

 Aliendelea:

 “Ultimately sisi, mimi na wewe, na zaidi  mimi tutawajibika kwa lolote la Wizara pamoja na miradi hii ya DSM. Kwa muda mrefu kumekuwa na  a lot of talk about package No.9.  Nilikudokeza talks hizo. Nipo tayari kumweleza Rais na WM & MKR kwa nini  tuwape ADUCO mradi huu in the light of go ahead ya W. Bank, go ahead ya National Committee ya IRP pending negations (sic) ambazo matunda yake ni reductions hizo za fedha na muda.”

 Waziri wa Ujenzi alimalia dokezo lake hilo kwa kuandika:

 “Kwa hiyo Ndugu KM wekeaneni mkataba na ADUCO. Sisi wawili tutawajibika, au ikibidi mimi nitawajibika. Lakini najua tupo pamoja katika principles of reasoning.”

 Amri hiyo ya Waziri aliitoa licha ya barua ya Katibu Mkuu kwa ADUCO ya kukemea ukaidi wa kampuni hiyo ya kukataa punguzo la Tshs 56m/- aliyoandika tarehe 17/1/1992 yenye Kumbukumbu Na. MOW/M.30/384/4/9.

 Amri ya Waziri wa Ujenzi ilitekelezwa na ADUCO wakapelekewa taarifa ya kukubaliwa kwa barua yenye Kumbukumbu Na. MOW/M.30/384/H/14 ya tarehe 3/2/1992.

 Matatizo katika utekelezaji wa kandarasi hii yalianza muda mfupi tu baada ya mkataba kutiliwa sahihi. Tatizo ambalo lilipelekea mgogoro mkubwa ni la upatikanaji wa changarawe kwa ajili ya barabara. Tatizo hili liliendelea kuwa kikwazo cha upatikanaji wa barabara imara na hatimaye kusababisha kupanda kwa gharama za mkataba huu.

Baadaye lilijitokeza pia suala la usajili wa mitambo iliyoingizwa nchini na kampuni hii ya ujenzi na kisha uchelewesho wa kupata michoro kutoka kwa “Project Consultants.”

Kilicho wazi hapa ni jinsi ADUCO walivoingiza ulalamishi na kiburi ili kuficha udhaifu wao kiutendaji kama mkandarasi.

Licha ya matatizo ya mkandarasi huyu, tarehe 22 Desemba, 1993 katika barua aliyowaandikia Ubalozi wa Uholanzi hapa nchini yenye Kumbu. Na. MWC/R.30/10/8  kuomba ufadhili wa Serikali ya Uholanzi katika ujenzi wa barabara hii, Waziri alisema, pamoja na maneno mengine, kwamba:

“I would also like Your Excellency to acknowledge the fact that M/s ADUCO International B.V has so far performed to our best satisfaction in the present contract and we would be pleased to continue working with them.”

Aidha, katika barua ya Desemba 1993 yenye Kumbukumbu Na. HVR/UW/9068, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya ADUCO International B.V. Bwana H.A. Van Rozen alimwandikia barua Mheshimiwa Kiula yenye maneno yafuatayo:

 

 “Dear Mr. Kiula,

 On 1 January, 1994 I shall retire from the position of Managing Director of ADUCO International B.V.

 From this date onwards the general management of the Company will rest with Mr. F.J.D. Touber.

 By means of this letter I would like to express my sincerest thanks for the pleasant cooperation I have experienced throughout the years.

 I expect that this cooperation can be continued on the same basis with Mr. Touber.

 

Yours sincerely,

 

Aduco International B.V.

(Signed)

H.A. Van Rozen”

 Suala la “Contract Addendum” lilijitokeza ghafla bila mtiririko unaoeleweka katika kumbukumbu zilizopatikana. Dokezo la tarehe 12 Desemba, 1993 ndiyo kumbukumbu pekee inayoonyesha kuibuka kwa mabadiliko ya thamani ya mkataba kutoka Tshs 606,841,759/70 hadi Tshs. 943,369,000/-.

 Ipo barua ya Wizara waliyowaandikia “Project Consultants” ya tarehe 31 Desemba, 1993 inayotaja Addendum Na.1. Barua ilitiwa sahihi na Mhandisi wa Mkoa wa Dar es Salaam lakini siyo yenye kueleweka wazi. Dokezo linalozungumzia pia “Addendum No. 1 to works contract pack No. 9 (DSM)” liliandikwa na Mkurugenzi wa Barabara na Viwanja vya Ndege kwa Kaimu Mhandisi Mkuu wa Barabara zaVijijini.

 Maoni ya Mwanasheria Mkuu wa Wizara kuhusiana na “Addendum” hii nayo yanadhihirisha utata uliokuwepo. Haijulikani maoni haya yalikuwa dokezo kwa nani lakini linatoa mwanga juu ya utata wa “Addendum” hiyo. Kwa mfano yamo maneno:

 “It has no background as to why such variation (in 2.1 above) had to be given consideration.”

 Hatimaye tarehe 20 Desemba, 1994 Wizara iliikabidhi ADUCO hati yenye uthibitisho wa kukamilika kwa kazi.

Licha ya hati hiyo, tarehe 09 Februari, 1995, chini ya miezi miwili baada ya uthibitisho wa kukamilika kwa barabara, “Project Consultants” walimwandikia Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi kuwa:

“However, the condition of the unsurfaced portions of the Project requires repair sooner than be expected under the proposed Dutch Program.”

Aidha, dokezo la Mkurugenzi wa Barabara kwa Waziri wa Ujenzi la tarehe 27/06/1995 lilikuwa na maelezo yafuatayo, miongoni mwa mengine:

“Kama ulivyoniagiza tafadhali pokea nakala ya barua iliyotumwa na Serikali ya Uholanzi kwa ADUCO ikithibitisha kukubaliwa kwa mradi wa kuimarisha barabara ya Pugu/Chanika/Mbagala chini ya mpango wa ORET.

“Gharama za mradi mzima ni Tshs 2,160m/- na zitagharamiwa ifiatavyo:

Serikali ya Uholanzi (60%) Tshs. 1,296m/-.

Serikali ya Tanzania (40%) Tshs. 864m/-.”

Mantiki ya dokezo hili pamoja na barua iliyokuwa imeambatishwa kutoka kwa Serikali ya Uholanzi kwenda kwa kampuni ya ADUCO International B.V. ni kwamba ADUCO (na siyo Serikali ya Tanzania) ndio walio “lobby” kupata fedha hizo na kwamba masharti yaliyowekewa makubaliano hayo ni kwa maslahi ya ADUCO.

Kuthibitisha wasiwasi huo ni hoja kuwa Wizara ya Ujenzi imetayarishiwa rasimu ya mkataba na Kampuni ya ADUCO  – yaani mkandarasi ndiye anayeiamuria serikali “contents” ya mkataba.

“Comments” za mtaalam mmoja wa Wizara kuhusu rasimu ya mkataa kama ilivyotayarishwa na ADUCO zilikuwa kama ifuatavyo:

“…..Scope of works of original contract is quite different from that of the addendum and also there is a big difference in the value of works, therefore, it seems advisable to negotiate for a new contract.”

 

(c ) Tathmini

Mkandarasi M/s ADUCO Int. B.V. aliteuliwa miongoni mwa zabuni nne licha ya wao kuwa wa gharama ya juu kupita wengine wote. Tofauti ya gharama za ADUCO na mkandarasi aliyefuatia kwa ukubwa ni zaidi ya 20%. Vigezo vya uteuzi wa ADUCO havikuwekwa wazi.

Awali maandiko ya Katibu Mkuu yalimweleza Waziri juu ya ughali wa zabuni za kampuni ya ADUCO kwamba zilikuwa juu ziadi ya wazabuni wote na ilikuwa vigumu kuwasaidia ikiwa ni dalili wazi kuwa lilikuwepo ombi au shinikizo la kuwapatia kazi.

Waziri aliafiki na kuamuru kuwa kazi ifanywe kwa misingi – wale ambao gharama zao zinalingana na hali halisi ndio wafikiriwe na kukiri kuwa gharama za ADUCO International B.V zilikuwa juu sana.

Pamoja na “observation” hii upo ushahidi wa Waziri kudharau kwa kebehi maelekezo ya wataalam wake yaliyoshauri hatua ya kupata mkataba wenye maslahi zaidi kwa taifa. Aidha, Waziri aliamuru ADUCO wapewe kazi hiyo na kwa maneno yake, angewajibika.

Mabadiliko haya ya maamuzi ya awali ya Waziri yanatia mashaka na kuelekeza kupindishwa kwa taratibu na kupelekea hisia za mmomonyoko wa maadili ya uongozi. Hakuna shaka kwamba ADUCO walipata upendeleo usiostahili na kwa hasara ya taifa.

Barua kwa Waziri iliyokiri na kushukuru uhusiano kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa ADUCO Int. B.V. aliyekuwa anastaafu nayo haitoi picha ya usimamizi wenye kulinda mashali ya Taifa hasa ikizingatiwa kwam a utendaji wa kampuni hiyo hadi Desemba, 1993, ulikuwa wa wasiwasi na hatimaye kupatikana barabara ya udongo  badala ya changarawe.

Aidha, kukiri kwa Waziri kwamba “ADUCO have so far performed to our best satisfaction in the present Contract and we would be pleased to continue working with them” ni maelezo yenye kuthibitisha kuwepo kwa jitihada za makusudi za kuficha udhaifu wa ADUCO na kulinda maslahi ya nafsi kwa hasara ya Taifa.

Upendeleo walioupata ADUCO kutoka wa Waziri ndiko kulikopelekea kudeka na kutumia malalamiko kama ngaoya kuficha udhaifu na kujipa sababu za ongezeko la gharama za mradi na faida.

Aidha,  mazingira yaliyopelekea mabadiliko yaliyosababisha gharama ya mradi kupanda kutoka Tshs. 606,841,859/70 hadi 943,369,000/- hayana uwazi uliothibitika. Gharama zimepanda ingawa “quality” ya barabara iliyojengwa ni duni kuliko ilivyokusudiwa na mkataba.

Imepatikana barabara ya udongo badala ya changarawe na chini ya miezi miwili baada ya kazi kukamilika na kutolewa hati ya kukamilika kwa kazi na Wizara, uharibufu mkubwa wa barabara uliohitaji matengenezo uliripotiwa.

Kujiingiza kwa ADUCO katika kuutafutia ufadhili mradi huu na baadaye wao kuandaa rasimu ya mkataba ni kinyume cha utaratibu uliozoeleka na dalili ni kwamba hayo yalifanywa ili kuficha madhambi ya awali pamoja na kujinufaisha. Kwamba Wizara na serikali hawakuona udhaifu na kasoro hii ni jambo pia linalozua mashaka.

 

MAPENDEKEZO YA JUMLA YA MRADI WA BARABARA ZA D

Uzembe

456. Matayarisho ya uteielezaji wa Mrari wa Matengenezo ya Dharura ya Barabara za Dar es Salaam (Dar es Salaam Emergency Road Repair Programme) imedhihirika kwamba yalikuwa duni na yaliyokosa upeo. Aidha, usimammzi wa utekelezaji wake haukuwa wa kuridhisha. Mifano ya kupuuzwa kwa hoja za wataalam ni mingi na dalili za maamuzi nje ya mwenendo wa maadili mema ya utendaji serikalini ni kubwa.

457. Vigezo vya uteuzi wa washauri wa miradi (Project Consultant) havikuelezwa na zipo dalili kwamba washauri wa mradi huu hawakupewa muda wa kutosha wa kupanga na kuusanifu mradi. Uteuzi wao ulifanywa baada ya mikataba kuwa imeshawekewa sahihi na pande mbili za makandarasi wa Wizara.

458. Kusingiziwa dharura kuwa ndilo chimbuko la udhaifu katika mipango ya utekelezaji si hoja ya msingi kwa kazi za kitaalam na zenye gharama kubwa kama za ujenzi wa barabara. Haiwezi kamwe kuwa kisingizio cha kusababisha kazi duni za viwango dhaifu wala kuwa msingi wa kusamehe matumzi mabaya ya fedha za serikali kwa kusababisha matumizi makubwa ambayo yangeweza kuzuilika.

459.  Hata hivyo, taarifa zenye kuonya juu ya kasoro za utekelezaji wa mpango huu wa matengenezo ya barabara za Dar es Salaam na kuelezea madhara yatakayotokana nao zilifikishwa kwa Mkurugenzi wa Barabara na kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi tangu mapema mwezi Februari, 1992.

Kazi hiyo ya kutoa tahadhari ilifanywa na Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi (Works Inspectorate) cha Wizara ya Ujenzi. Dokezo aliloandikiwa Mkurugenzi wa Barabara Bwana Urio la Februari, 1992 lilitamka wazi pamoja na maneno mengine kwamba:

“In brief the supervision of the work seems to be inadequate. On top of the lack of design there is an even higher risk than previously that the end result will be sub-standard.”

Aidha, dokezo la Mtaalam wa “Works Inspectorate” kwa Katibu Mkuu lilitahadharisha hivi:

“All the contracts are now signed without any attempt to accommodate proposed improvements.”

“Repeating my main points on Dar es Salaam Road Emergency Repair with Shekilango Road as an example:

“The ‘emergency repair’ is not any more an emergency repair – not cost-wise, not technically and possibly not even time-wise.”

Katika moja ya aya zake, dokezo hili lilikuwa na maandishi yafuatayo:

“It is possible to keep costs down by stage – construction of the pavement. However, it would be a very serious and costly mistake to construct the road following the present “design.” The technical competence of this Ministry might be questioned by the public immediately the road is opened to traffic!”

460. Maelezo haya ni ushahidi dhahiri kwamba ushauri wa kuboresha usanifu na utekelezaji wa mradi huu ulitolewa mapema, lakini ulipuuzwa na viongozi wa ngazi za juu na ndicho chanzo cha ucheleweshaji, ongezeko kubwa la gharama na kazi duni. Ushahidi huu unapinga hoja za Mkurugenzi wa Barabara alizozitoa katika moja ya mazungumzo yake na Tume kwamba mazingira ya mikataba hiyo hayakutoa nafasi ya usanifu na matayarisho ya kina na hivyo kuwa sababu iliyochangia hasara kubwa kwa serikali katika utekelezaji wa mradi huu.

 

Rushwa

 461. Likiachiliwa mbali suala la uzembe na upungufu wa uwezo wa kupanga na kusimamia, limekuwepo pia suala la maadili duni lililojitokeza awali katika hatua za kutoa zabuni. Suala la maadili duni katika zabuni limedhihirika wazi kabisa mikataba miwili ya K.V. Construction Limited kwa barabara ya New Bagamoyo na ADUCO Int. B.V kwa barabara ya Pugu-Chanika-Mbagala.

 

(a)  K.V. Construction Limited  

Katazo la wataalam wa Wizara la kutowapa K.V. Construction Limited kandarasi ya ujenzi Mkuu wa Wizara ya Ujenzi wakati huo Dr. George Mlingwa alipinga ushauri wa jopo wa Barabara ya New Bagamoyo na kusimamia kupewa kandarasi kwa kampuni hiyo. Baadaye ushauri wa wataalamu wa Wizara ulirejewa na washauri wa mradi hata kabla ya taratibu za kutiliana sahihi mkataba kutekelezwa.

Ukaidi wa kupinga ushauri wa kutoingia mkataba na kampuni ya K.V.Construction Limited ulifuatiwa na upinzani dhidi ya ushauri wa kusitisha mkataba huo uliotolewa mara tatu tofauti na washauri wa mradi pamoja na mara moja na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wahusika wakubwa na pingamizi hili kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopatikana walikuwa Waziri wa Ujenzi (wakati huo Mheshimiwa Nalaila Kiula), Dr. P.F.Komba ambaye alikuwa Mhandisi Mkuu wa Barabara za Vijijini na Bwana H.G. Urio wakati huo Mkurugenzi wa Barabara na Viwanja vya Ndege.

Ni maoni ya Tume kwamba ushauri kuwa serikali isiingie mkataba na K.V. Construction Limited na baadaye wa kusitisha mkataba uliokwishaingiwa ulikuwa sahihi na uliojali maslahi ya Taifa na kwamba kupingwa kwa ushauri huo kumepelekea hasara na fedheha kwa serikali. Aidha, Tume inaamini kwamba pingamizi dhidi ya ushauri huo ulilenga katika kunufaisha maslahi ya kibinafsi na wa bahati mbaya, bali uliofanywa kwa dhamira.

 

Je, unafahamu Jaji Warioba katika ripoti hii aliyoiandaa mwaka 1996 alibaini nini katika miradi mingine ya ujenzi wa barabara na jinsi wakubwa walivyojipatia rushwa? Ingawa ripoti hii imeandikwa mwaka 1996, inaendelea kuwa na maudhui yenye uhalisia na yenye kuonyesha upungufu ule ule hadi sasa na hivyo inastahili kufanyiwa kazi. Usikose JAMHURI wiki ijayo. Mhariri.