UCHAMBUZI WA KINA
453. Barabara za New Bagamoyo na Pugu-Chanika-Mbagala ndizo ambazo zimethibitika kuhusisha sana matatizo makubwa ya ukikwaji wa taratibu na maadili mema ya kazi.
454. New Bagamoyo Road
(a) Urefu: Kilometa 13.4 kuanzia makutano ya Barabara ya Sam Nujoma hadi njia panda ya kuelekea Kiwanda cha Saruji cha Wazo Hill.
(b) Uchambuzi
(i) K.V Construction Limited waliteuliwa kutoka miongoni mwa makampuni ya ukandarasi matano yaliyokuwa yamerejesha zabuni. Mkataba uliwekewa sahihi tarehe 14 Machi, 1992 kwa makubaliano ya Tshs. 737,956,406/30 sawa na wastani wa Tshs 55,071,374/= kwa kila kilometa moja.
(ii) Tarehe 20 Septemba, 1991 kilifanyika kikao cha kujadili taarifa za uchambuzi wa zabuni hizi chini ya uenyekiti wa aliyekuwa Mhandisi Mkuu ( Chief Engineer Construction). Wajumbe wote wa kikao hicho walikuwa wahandisi wa Wizara ya Ujenzi.
Maamuzi ya kikao hicho yalikuwa pamoja na kupendekeza kuwa M/s K. V. Construction Limited wasipewe kandarasi ya ujenzi wa New Bagamoyo Road ingawa kampuni hiyo ndiyo iliyokuwa imetoa zabuni nafuu zaidi kigharama kuliko nyingine zote. Sababu za ushauri huo zilielezwa kuwa zifuatazo:
Kwamba kampuni ya K.V. Construction Limited haikuelekea kuwa yenye kumiliki vifaa vyovyote vya kazi za barabara. Kikao kilikuwa na wasiwasi dhidi ya hali iliyopelekea M/s K. V. Construction Limited kutumia uthibitisho wa Mahakama Kuu kuonyesha kuwa inamiliki vifaa ambavyo vilikuwa katika kambi ya Masanza Mwanza. Kwa maoni ya Kikao hicho, kuhusishwa kwa Mahakama Kuu ili kupata utekelezaji wa kazi hiyo [lilikuwa tatizo].
Kwamba kampuni ya K. V. Construction Limited ilishindwa kutekeleza agizo la Wizara lililowataka waainishe aina ya vifaa “walivyonunua” kutoka kwa kampuni ya G.S.E. SpA. Aidha kampuni hiyo ilishindwa kueleza kiasi cha fedha walichotumia kwa ununuzi huo pamoja na kutoweza kuelezea mpango wa upatikanaji wa vifaa hivyo. Kikao hicho kilishauri kuwa kandarasi ya ujenzi wa barabara ya New Bagamoyo ipewe kampuni ya ZAKHEM International Construction Ltd iliyokuwa ya pili kwa unafuu wa gharama.
(iii) Katika mawasiliano mbali mbali yaliyofuatia baina ya jopo la wataalam na uongozi wa juu wa Wizara ya Ujenzi, zipo taarifa nyingi ambazo zilipinga kupewa kazi hii kampuni ya K.V. Construction Limited kwa sababu ya uwezo wake mdogo. Hivyo watalaam walikuwa na wasiwasi mkubwa wa kuisababishia Serikali aibu na hasara.
Licha ya maoni hayo ya wataalam wa Wizara waliokuwa wamekabidhiwa jukumu la kusimamia maslahi ya Serikali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi alipinga hoja hii na kuandika dokezo lifuatalo kwa waziri wa Ujenzi tarehe 4/10/91:-
“…Sikubaliani na maoni ya Kamati kuhusu K.V. Construction. Kitu kinachotakiwa hapa ni kama K.V. Construction anayo mitambo au hana. Pamoja na ripoti za mwanzo ambazo zimeona mitambo na kutoa maoni kwani hawana uhakika kama ni ya K.V. Nashauri tumpe ‘benefit of doubt’ na tumpe ‘CONTRACT’ hii. Ila nashauri tumpe muda wa mwezi mmoja kuhamishia mitambo kwenye site. Kama akishindwa basi tumnyang’anye contract”.
Waziri alikubana na ushauri wa Katibu Mkuu wake kwa marekebisho tu ya muda wa kuhamisha mitambo kuwa miezi mitatu badala ya mwezi mmoja. Tarehe 16 Oktoba, 1991 katika kikao kilichoongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi kama Mwenyekiti uamuzi wa kuipa kampuni ya K.V. Construction Limited kandarasi ya ujenzi wa New Bagamoyo Road ulipitishwa rasmi, hivi:
“Since the bidder has cleared the problem associated with ownership of equipment/plant, the meeting recommends award of contract for Package No. 2 to M/s K.V. Construction, the lowest bidder”.
Uamuzi wa kikao kilichoketi chini ya uenyekiti wa Katibu Mkuu kilichopita mapendekezo ya Kamati na kuamua kutokubaliana nayo kuhusiana na “package” ya New Bagamoyo Road ulifikishwa kwa Waziri kwa dokezo la 16/10/91 la Katibu Mkuu (Ujenzi). Waziri alikubali kandarasi ya barabara ya New Bagamoyo wapewe M/s K. V. Construction Limited badala ya ZAKHEM International Construction LTD.
Masuala mengine yaliyokuwa na utata kuhusiana na M/s K.V. Construction Limited ni ya umilikaji wa mitambo aliyokuwa ameiorodhesha kuwa yao. Utata wa umilikaji wa mitambo hiyo uliendelea kwa muda mrefu na kusababisha pamoja na sababu nyingine Wizara kushauriwa na Washauri wa Mradi (project consultants) kwamba uwepo uangalifu mkubwa katika kufikia makubaliano nao. Katika barua yenye kumbukumbu Na. DCMK/MOW/Pkg. 2.03 ya tarehe 25 Februari, 1992, Washauri wa Mradi wameitahadharisha Wizara ya Ujenzi katika ukurasa wa mwisho wa barua hiyo hivi:
“K.V. Construction Limited is a brand new company with no experience in building roads; has acquired all their equipment by a round – about method and has shown reluctance to submit detailed verification of clear ownership and has made what appears to be a serious error in their tendered price for a major construction item which could mean a Tshs. 50 million loss of revenue which amounts to 10 percent of the net contract amount and a majority of their potential profit. We have also failed to locate their office. At each of the locations which they have designated, our messengers have drawn a blank – no one has heard of K. V. Construction Limited. Their designated Site Agent is inexperienced in road construction management.
“We have recently written to them, Ref. DCMK/Pkg.2/Gen/02 21 February, 1992 (copy attached) instructing them to submit;
1. Documentation verifying the multiple transfer of equipment.
2. Certified Financial Statement for K. V. Construction Limited
3. Particulars of key personnel
We recommend caution in signing a contract with K. V. Construction Limited, particularly for the New Bagamoyo Road which is the highest visibility package. K.V. Construction Limited should be required to submint full performance securities and bank guarantees for advance payments before the contract is signed.” Maelekezo yanayofanana na yale ya mshauri wa mradi yaliyofanywa kwa Katibu Mkuu na “Tender Negotiations Committee” tarehe 10 Machi, 1992.
Bila kuzingatiwa kwa maelekezo yote yaliyofanyika, tarehe 13 Machi, 1992 kwa barua yenye Kumbukumbu Na. MOW/M. 30/384/A/9 kwa K.V. Construction Ltd. Wizara ya Ujenzi ilimtaarifu mkandarasi huyo kuwa zabuni yake imekubaliwa. Barua ilitiwa sahihi na Bw. H. G. Urio kwa niaba ya Katibu Mkuu. Tarehe 6 Mei, 1992 kwa barua Na. SHC/R. 270/2 kwa Mheshimiwa N.L Kiula (MB), Waziri wa Ujenzi, Rais wa Jamhuri ya Muungano aliandika miongoni mwa mengine, hivi:
“Ujenzi huo ulikuwa uanze 8 Aprili, 1992. Huakuanza. Baadaye Project Manager alikuja kwenu kuomba radhi tarehe 20 Aprili, 1992. Mpaka leo 6 Mei, 1992 kazi bado haijaanza. Umuhimu wa barabara hiyo ni pamoja na kuhudumia shughuli za utalii katika Hoteli za Kunduchi ambako tayari baadhi ya wateja wanahama kutokana na usumbufu wa kusafiri kwenye barabara mbovu zinazo waumiza. Huku ni kuhujumu uchumi!” Katika mawasiliano hayo hayo Rais alisema, ndani ya aya nyingine, hivi:
“Inasemekana pia kuwa tenda hii imetolewa kwa njia za upendeleo kwa hasara ya Taifa. Kutokana na hali hii ni vyema mkataba na Kontrakta huyu ukavunjwa na kupewa watu wengine wenye vifaa na uwezo.” Tarehe 13 Mei, 1992 Washauri wa Mradi waliipelekea Wizara ya Ujenzi barua yenye kumbukumbu Namba CMK/MOW/Pkg.2/Con/48 yenye kupendekeza naye na kuelezea kwa undani sababu tatu za kufanya hivyo.
Katika dokezo alilomwandikie Mkurugenzi wa Barabara na Viwanja vya Ndege la tarehe 28/5/1992, Katibu Mkuu Ujenzi aliagiza notisi ya kumfukuza kazi mkandarasi K.V. Construction Limited isogezwe mbele kwa siku nyingine 10 kwa sababu, Katibu Mkuu aliandika; “Tulimwandikia Mkandarasi kupitia kwa Consultant kuwa tumempa siku 14 kukamilisha maandalizi yake na kuwa mitambo iwe imewasili kwenye ‘site’ ifikapo leo tarehe 28/5/92.
Taarifa nilizonzao kutoka Mwanza ni kwamba mitambo mingi tayari imepakiwa kwenye mabehewa na kuondoka Mwanza, mingine bado iko Mwanza South ikisubiri kusafirishwa kwa kutumia TRC. Aidha karibu mitambo yote sasa imeisha toka Masanza Camp. Kwa taarifa hiyo si vyema tukamfukuza Constructor kenye ‘site’. Waziri wa Ujenzi tayari amemweleza Rais kuwa deadline ya mobilization ni tarehe 8 Juni, 1992 kutokana na kuwa Barua ya commencement alipewa tarehe 8/4/92. Kuheshimu yote haya ni vyema tukamwagiza siku nyingine Consultant aka-extend 14 days notice kwa kumi.”
Tarehe 9 Juni, 1992, Washauri wa mradi waliindikia Wizara barua Na. DCMK/MOW/Pkg.2/Gen/52 kuitaarifu maendeleo yaliyotokana na kusogezwa mbele kwa tarehe ya notisi ya kumfukuza mkandarasi, kwamba, “On 8 June 1992, at approximately 1800 hrs, I inspected the equipment mobilized by K. V. Construction for the above Contract. There wasi one grader and one tipper truck with water tank on board…
“The above is all the evidence there is of the Contractor’s mobilization as of the extended date for complete mobilization.
“It is your Consultant’s opinion that K. V. Construction Ltd. Has, by its inaction, defaulted under Clause 63 of the General Conditions of Contract. We recommend that the Ministry act in accordance with Clause 63 to terminate the employment of K.V. Construction as of this date, having given the required 14 days notice on 15 May, 1992 and an extension on 5 June 1992”. Katika barua ingine ya tarehe 9 Juni, 1992 yenye Kumb. Na.DCMK/MOW/Pkg.2/Gem/53 kwa Wizara na Washauri wa Mradi wamesisitiza.
“Terminate K.V. Construction without prejudice, cancel their performance bonds, pay them for the small amount of Advance Maintenance they carried out, and allow them to tender for smaller projects, where they can gain the experience they now lack.”
Wizara ya Ujenzi kwa barua iliyotiwa sahihi na Dr. P.P. Komba kwa niaba ya Katibu Mkuu ya tarehe 10/06/1992 na yenye Kumb. Na. MOW/M. 30/384/A/25 ikielekezwa kwa Washauri wa Mradi na kunukuu barua Kumb.Na DCMKMOW/Pkg.2/Gem/53 iliamuru pamoja na mambo mengine, hivi:
“Ministry has taken note of the recommendations mentioned in the above referred letter and found that physical evidence to support the recommendations is lacking.”
Kwa barua yenye Kumb. Na. MOW/M.30/384/A/28 ya tarehe 26 Juni, 1992 iliyowekewe sahihi na H.G. Urio kwa niaba ya Katibu Mkuu. Wizara imekataa ushauri wa Washauri wa Mradi wa kusitisha mkataba kwa maandishi yafuatayo:
“In light of efforts which the Contractor (M/s K. V. Constructions) has shown so far and due to the fact that some equipment has already arrived on site from Mwanza we would like to revisit your recommendation. May we request you to appraise the Employer on the current status of the project and whether there is any intent on the part of the Contractor to start the road works.”
Baada ya miezi mitano hivi, Washauri wa Mradi (Project consultants) waliipelekea Wizara ya Ujenzi barua yenye Kumb. Na. DCMK.MOW/Memo/01 iliyoandikwa tarehe 8 Desemba, 1992 iliyoilalamikia Wizara kwa maelezo makali sana juu ya udhaifu wa K.V. Construction katika kuutekeleza mkataba huu. Waliandika, pamoja na mengineyo, hivi:
“As of 25 Novemba, 1992 approximatel 63% of the Contract Period had elapses with about two (2%) of the works completed.
“We have twice recommended that this Contractor be terminated for lack of lack of progress and gross inexperience. Both times the process dragged out to where the Ministry said to drop the recommendation.
Our credibility has been badly corded and has reached the point where the Contractor simply ignores instructions. This attitude had visibly expanded to other contractors.
“We would like to meet with the Principal Secretary and yourself to decide what the Ministry is prepared to do and how to proceed.”
Utendaji wa K.V. Construction Limited uliendelea kwa kujikokota na utaratibu wa kumfukuza kazi uliendelea kupigwa vita hadi Waziri wa Ujenzi alipokiri bayana kwa dokeza kwa Katibu Mkuu la tarehe 13/1/93 kwamba:
“Barabara hii mbele ya Lugalo imeanza kutisha. K.V. hawezi kazi hii. Enough is enough.” Tarehe 20/1/1993 Dr. P.F.C. Komba Chief Engineer wa Rural Roads wizarani alimwandikia dokezo Mkurugenzi wa Barabara na Viwanja vya Ndege akikiri kwamba ni kweli maendeleo ya kazi yanakatisha tama, lakini wakati huo huo kukataa pendekezo la “Project Consultant” la kumfukuza kazi badala yake alishauri eti K.V. waachiwe sehemu ya kazi wakati mkandarasi mwingine awe “subcontracted” kutekeleza sehemu nyingine ya mkataba. Pendekezo hilo, kwa maajabu, lilikubaliwa na Mkurugenzi wa Barabara na baadaye Katibu Mkuu.
Hata hivyo, tarehe 21 Aprili, 1993 “Project Consultants” M/s De Leuw Cather International kwa barua yenye Kumb. Na. DCM/MOW/Pkg.2/240 waliiandikia tena Wizara ya Ujenzi kuishauri kusitisha mkataba na K.V. Construction Ltd: “Contract was signed on 14 March, 1992 with a 300 day Contract Period. This Period has now expired with only (4%) percent of the certified Despite numerous instructions and warning the Contractor has failed to perform. We bereby recommend that you as the Engineer, declare the Contractor. K.V. Construction Ltd, to be in default….”
Hatimaye busara ya mlolongo wa maelekezo na ushauri ilionekana machoni mwa wataalam wa ngazi ya juu pamoja na uongozi wa Wizara ya Ujenzi na tarehe 22 Aprili, 1993 kwa barua yenye Kumb.MWC/R/30/10/97 Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Dr. George Mlingwa aliwaandikia M/s K.V. Construction Limited barua ya kusitisha mkataba.
(iv) Taratibu za usitishaji mkataba zilikamilika tarehe 8 Septemba, 1993 na kazi kukabidhiwa kwa kampuni ya MECCO tarehe 20 Agosti, 1993. Katika makubaliano ya awali na K.V. Construction Limited gharama za ukarabati wa barabara hiyo zilikuwa Tshs. 737, 956,406/30 sawa na wastani wa Tshs. 55,071,374/= kwa kila kilometa moja.
Gharama halisi za mradi huu zilifikia Tshs. 1,861,120,832/44 sawa na wastani wa Tshs. 138,889,614/= kwa kila kilometa moja. Kazi ilikamilishwa rasmi tarehe 31 Januari, 1995. Ongezeko hili la asilimia 152 lilichangiwa, pamoja na sababu nyingine, na ucheleweshaji wa kukamilika kwa kazi kulikotokana na uteuzi mbaya wa mkandarasi pamoja na ukaidi wa baadhi ya wataalam na viongozi wa Wizara ya Ujenzi wa kukataa kutekeleza maelekezo na ushauri wa wataalam wa chini yao pamoja na ule uliotolewa mara nyingi na “Project Consultants.”
(c ) Tathmini:
Tume baada ya kuchambua mtitiriko wa matuko na vitendo (na mahali pengine ukosefu wa vitendo) katika zoezi zima la ajira ya kampuni ya K.V. Construction Limited katika mkataba huu, imeridhinishwa kwamba kampuni hiyo ilikuwa imepewa upendeleo maalum wa makusudi na usiostahili wenye kukiuka maadili na ambao haukuzingatia kabisa maslahi ya Taifa.
wamba Waziri wa Ujenzi na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo walikusudia kuweka vikwazo dhidi ya hatua za kutowekewa sahihi mkataba na baadaye dhidi ya kusitisha mapema mkataba baina ya Wizara na K. V. Construction Limited.
Aidha wataalam wa ngazi ya juu wa Wizara, hususan Mkurugenzi wa Barabara (DRA) Bwana H. G. Urio na Mhandisi Mkuu wa Barabara za Vijijini (CE/RR) Dr. P.F. Komba walishindwa kutimiza wajibu wao wa msingi wa kulinda maslahi ya Taifa na maadili ya kitaaluma kwa kutoshauri kwa wakati dhidi ya mkataba huo kama mapendekezo ya “Project Consultant” na wataalam wa chini yao wizarani yaliyokuwa yakielekeza. Kwa vitendo vyao Taifa limepata hasara na kufedheheka na kuwasababishia kero kubwa wananchi kupungukiwa imani na Serikali yao.
455. Barabara ya Pugu- Chanika – Mbagala
(a) Urefu: Kilometa 46.7 za barabara ya changarawe
(b) Uchambuzi:
(i) Mkataba wa ujenzi wa barabara hii ya vijijini uliwekewa sahihi tarehe 4 Februari, 1992 baiana ya Wizara ya Ujenzi na mkarandarasi kampuni ya ADUCO INT. B.V. ya Uholanzi kwa gharama ya Tsh. 606,841,760/= sawa na wastani wa Tshs.12.994,470/= kwa kila kilometa moja. Maelekezo ya mkataba ni kupata barabara ya changarawe kwa urefu wa kilometa 46.7.
(ii) Mkataba ulifanyiwa mabadiliko (contract addendum) yaliyosababisha gharama kupanda na kufikia Tshs. 962,152,460/= (wastani wa Tshs. 20,602,836/40 kwa kila kilometa moja).
(iii) Taarifa rasmi ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi kwa Tume imearifu kuwa utekelezaji wa mradi huu ulikabiliwa na matatizo ya ukosefu wa udongo mzuri kwa ajili ya tuta la barabara; aidha mahitaji makubwa zaidi ya matengenezo yalisababisha ongezeko kubwa la kazi na kwamba kazi za mkataba wa awali uliojumuisha “contract addendum” iliyoelekezewa katika (ii) zilikamilika tarehe 31 Desemba, 1993 kwa kiwango cha barabara ya udongo.
(iv) Taarifa ya Katibu Mkuu imeongeza kuwa Serikali iliomba msaada kutoka Serikali ya Uholanzi wa kuweka lami au changarawe kwenye barabara hii na kwamba Serikali ya Uholanzi ilikubali kutoa msaada huo mwezi Oktoba, 1995 lakini kwa sharti kwamba kazi hizo zitekelezwe na mkandarasi Yule Yule wa mwanzo yaani kampuni ya ADUCO INT . B.V na kwa kutumia mkataba ule ule wa awali. Makubaliano ya nyongeza hii ya pili ya mkataba (contract addendum no. 2) yalitiwa sahihi tarehe 18 Oktoba, 1995.
Kwahiyo mkataba wa ujenzi wa barabara hii umefanyiwa marekebisho mara mbili. Ya kwanza yalibadilisha gharama kutoka Tshs. 606,841,760/= hadi ya pili yaliyoizifikisha gharama hizo kuwa Tshs.2,750,321,582/= ambazo ni sawa na wastani wa Tshs. 58,893,396/= kwa kila urefu wa kilometa moja ya barabara.
(v) Mfululizo wa matukio yaliyoufikisha mkataba huu katika hatua ya ujenzi wa barabara ya udongo badala ya changarawe na hatimaye kusababisha kuwapa gharama mara “mbili” wananchi na Serikali ni kama ifuatavyo:
Je, unafahamu Jaji Warioba katika ripoti hii aliyoiandaa mwaka 1996 alipendekeza hatua zipi zichukuliwe kudhibiti rushwa katika na hasa barabara hii ya Bagamoyo? Ingawa ripoti hii imeandikwa mwaka 1996, inaendelea kuwa na maudhui yenye uhalisia na yenye kuonyesha upungufu ule ule hadi sasa na hivyo inastahili kufanyiwa kazi. Usikose JAMHURI wiki ijayo. Mhariri.