Polisi wanalea dawa za kulevya

 

Mapendekezo

244. Tume inatoa mapendekezo yenye madhumuni ya kupunguza na hatimaye kuondoa wimbi la rushwa inayotokana na vitendo ndani ya Jeshi la Polisi kama ifuatavyo:

a) Ziwepo jitihada za makusudi zitakazoelekezwa kwenye kuelimishana kuhusu umuhimu wa Jeshi la Polisi katika maendeleo ya taifa letu. Semina na warsha ziwajumuishe pamoja viongozi na watendaji wakuu wa Jeshi la Polisi na wa vyombo vingine vya dola hususan vya ulinzi na usalama kwa madhumuni ya kulielewa vizuri tatizo hili na athari zake kwa nchi ili upatikane msimamo wa pamoja wa kupambana nalo.

(b) Tume inapendekeza kuimarisha kwa uongozi wa ngazi zote za Jeshi la Polisi ili uweze kusimamia na kudhibiti kikamilifu utendaji wa askari. Aidha, usimamizi na uwajibikaji ndivyo viwe vigezo vya uongozi bora. Zoezi hili lianze kwa kusafisha safu za uongozi uliopo wa Jeshi la Polisi. Wenye historia ya kukiuka maadili na kula rushwa au kukumbatia walarushwa waondolewe jeshini na ikibidi wachukuliwe hatua za kisheria.

(c)  Taratibu za ajira ziainishe wazi sifa zote zinazohitajika kwa mtu kuwa askari wa Jeshi la Polisi. Wajihi, kiwango cha elimu, werevu, sifa za uadilifu, mahusiano n.k. vipembuliwe na viwekwe bayana na utekelezaji wake usimamiwe. Adhabu kwa watakaozikiuka zifafanuliwe na ziwe wazi. Aidha, utafiti na sensa ya askari wote unahitajika ili kubaini waliojiunga na Jeshi la Polisi bila kufuata utaratibu au kutokuwa na sifa za msingi. Watakaobainika waachishwe na waliohusika na ajira zao wachukuliwe hatua kwa mujibu wa kanuni na taratibu zilizopo. 

(d) Ili kuziba mwanya uliosababishwa na upungufu wa kitaifa wa viwango vya elimu katika shule zetu, Tume inapendekeza kuwa ajira ya askari wa Jeshi la Polisi si tu iendelee kuweka kiwango cha chini cha elimu kuwa kidato cha nne, lakini pia ifafanue kiwango cha chini cha kufaulu kinachohitajika. Tume inapendekeza kiwango cha kufaulu kiwe daraja la tatu (yaani “division three”) ndani ya mfumo uliopo hivi sasa. Msisitizo huu unatarajiwa kulipatia Jeshi la Polisi askari ambao hawatatokana na watu waliokosa kazi kwingineko bali wenye mapenzi, wito na sifa nyingine maalumu zinazotakiwa katika jeshi.

(e) Tume inapendekeza kuwa mafunzo yapewe kipaumbele katika mfumo mzima wa marekebisho ya mwenendo wa Jeshi la Polisi kwa lengo la kuinua viwango vya elimu, utendaji na tija vya askari. Vyuo vya mafunzo viimarishwe kwa kupatiwa nyenzo za kisasa. Aidha, wakufunzi waandaliwe ipasavyo ili waweze kukidhi haja ya mafunzo ya kisasa.

(f) Tume imebaini kuwepo kwa udhaifu mkubwa katika taratibu na usimamizi wa ajira na upandishaji vyeo askari ndani ya Jeshi la Polisi na inapendekeza kuwa ikama ya Jeshi la Polisi ipitiwe na kufanyiwa marekebisho yanayostahili ili iwiane na mahitaji halisi pamoja na kuzingatia mahitaji ya karne ya 21.

(g) Tume inapendekeza kuwa uongozi wa Jeshi la Polisi uimarishe utaratibu wa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa maeneo ya kazi ya askari walio chini yao. Aidha, utendaji kazi wa kila siku wa askari uwekewe kumbukumbu sahihi ili kurahisisha udhibiti wa tabia na mienendo yao katika kila ngazi.

(h) Tume inapendekeza kuwa uteuzi wa viongozi wa juu wa Jeshi la Polisi uzingatie pia nia ya kulifikisha jeshi katika hatua ya kuthamini mchango wa sayansi na teknolojia. Uteuzi usizingatie tu watumishi waliodumu kwa muda mrefu katika Jeshi la Polisi ili kuwezesha jeshi kupata mwelekeo mpya nje ya misingi iliyokwishazoeleka, ambayo tume inaamini inachangia kufupisha upeo wa maendeleo ya jeshi hilo.

(i) Tume inapendekeza kuwa utaratibu wa ukaguzi uambatane na uwajibishaji wa askari, na viongozi wa Jeshi la Polisi watakaobainika kukiuka misingi ya utendaji ya jeshi. Aidha, wakuu wa upelelezi wa vituo, wilaya, mikoa na Makao Makuu ya Jeshi la Polisi walazimike kufuata sheria inayokataza kumzuia mtuhumiwa kituo cha polisi kwa muda mrefu zaidi ya ule ulioruhusiwa kisheria kabla ya kufikishwa mahakamani kufunguliwa shtaka.

Utaratibu huu wa ukaguzi uhakikishe uwazi katika suala hili kwa kubuniwa fomu ambazo zitatumika kuweka kumbukumbu za mtuhumiwa tangu anapofikishwa kituoni. Fomu hizo ziwe na sehemu za kuthibitishwa na mtuhumiwa na shahidi wake.

(j) Tume inapendekeza serikali ilipe Jeshi la Polisi nyenzo muhimu za kazi vikiwemo vyombo vya usafiri, silaha, zana za mawasiliano na sare. Aidha, boti za doria majini ni muhimu ili kuwezesha udhibiti wa uhalifu katika maeneo ya bahari na maziwa.

(k) Ili kuimarisha utunzaji wa kumbukumbu na kuwezesha kupata taarifa kwa haraka, Tume inapendekeza Jeshi la Polisi lipatiwe kompyuta za kutosha ili kuliongezea ufanisi katika utendaji.

(l) Tume inapendekeza kuwa jitihada za makusudi zifanywe na zenye kulenga ufufuaji wa ushirikiano wa kimafunzo na mbinu za kiutendaji baina ya jeshi letu la polisi na majeshi ya polisi ya nchi zenye ujuzi zaidi na zilizoendelea. Aidha, mafunzo maalumu kwa baadhi ya maofisa wa Jeshi la Polisi nje ya nchi nayo yapewe umuhimu unaostahili.

(m) Tume inapendekeza kuwa serikali iangalie upya masilahi ya askari wa Jeshi la Polisi ili yazingatie umuhimu wa majukumu yao. Pia Tume inapendekeza kuwa urejeshwe utaratibu uliokuwepo wa askari kuishi kambini. Aidha, Tume inapendekeza kwamba ule utaratibu wa zamani wa kuwawekea askari maduka katika kambi zao ambayo yaliwapatia mahitaji ya msingi kwa bei nafuu urudishwe. Hali kadhalika utaratibu wa mikopo yenye masharti nafuu kwa ununuzi wa vifaa kama vile majokofu, majiko, samani, n.k. nao urejeshwe.  

 (n) Tume inapendekeza kuwa mamlaka ya Mkurugenzi wa Mashtaka kuhusiana na usitishaji wa kesi katika mahakama yaambatane na wajibu wa kueleza sababu za usitishaji huo.

(o) Ili kuondoa mlundikano wa mahabusu katika magereza, utaratibu wa kipindi maalumu ambacho kesi inaweza kucheleweshwa kutokana na kutokamilika kwa upelekezi katika mahakama uwekwe. Aidha, sheria inayohusika irekebishwe ili izingatie pendekezo hili.

(p) Tume inapendekeza kuwa taratibu za kutoruhusu askari kufanya kazi mahali pamoja au kituo kimoja kwa miaka mingi zifufuliwe; yaani askari ahamishwe kila baada ya miaka kama mitatu katika sehemu ya kazi. Aidha, utaratibu wa uhamisho wa askari kati ya Bara na Visiwani upewe kipaumbele ili kuondokana na dhana kwamba ni askari wenye asili ya Zanzibar pekee ndio waongoze visiwani kwa ngazi zote za taifa, mikoa na vituo.

 

Madawa ya kulevya

245. Katika miaka ya hivi karibuni, Tanzania imeshuhudia ongezeko kubwa la tatizo la madawa ya kulevya. Tatizo hilo hivi sasa linaonekana katika sura tatu; usafirishaji, uuzaji na utumiaji. Kwanza kwenye miaka ya mwishoni mwa 1980 Tanzania iliibuka kama kituo muhimu cha kupitishia madawa (transit route) kutoka Mashariki ya Kati na Asia ya Kusini Mashariki kwenda Afrika Kusini, Marekani na Ulaya. Baadaye sehemu ya madawa hayo “ilidondoka” kwenye soko la humu nchini na hivyo kutumiwa hapa. Hivi sasa taifa lina tatizo kubwa la watumiaji hasa katika Jiji la Dar es Salaam na Zanzibar. 

246. Katika mwaka 1995 zilikamatwa hapa nchini tani nne za bangi na tani 10.9 za aina nyingine za madawa ya kulevya. Kiasi hiki ni kikubwa ikilinganishwa na tani 2.9 za bangi na kilo 745.2 za aina nyingine za madawa ya kulevya zilizokamatwa mwaka 1994. Aidha, mwezi Februari 1996 tani 10 za madawa ya kulevya zilikamatwa hapa nchini zikiwa zimesafirishwa kutoka nchi jirani ya Zambia kuelekea Ulaya.

Unguja, mwaka 1996, zilikamatwa kilo 88 za madawa ya kulevya aina ya mandrax. Tarakimu hizi ni ushahidi wa kutosha wa kuonyesha mwenendo wa ongezeko la biashara ya madawa ya kulevya hapa Tanzania linaloambatana pia na ongezeko la aina mbalimbali za madawa hayo.

247. Aina ya madawa ya kulevya yanayopitishwa nchini ni mandrax, heroine na hashish. Madawa haya yanatoka Mashariki ya Kati hasa Lebanon, Iran na Bara Hindi – Pakistan, India, Afghanistan na hata Thailand. Madawa haya yalianza kuja nchini kupitia Zanzibar. Baadaye yakaanza kusafirishwa kwa kupitia ndege, hasa zinazotoka Mashariki ya Kati na India. Wasafirishaji wengine wametumia kituo cha Nairobi na kuingia nchini kupitia Namanga.

Aidha, wengine wamediriki kupitia Entebbe, Uganda na kuingia nchini kupitia mpaka wa Mutukula. Umekuwepo ushahidi wa kuonyesha wasafirishaji wengine wamediriki kuingiza nchini madawa ya kulevya kupitia bandarini.

248. Sehemu kubwa ya madawa yanayoingia nchini husafirishwa nje ya nchi. Mengine huenda Ulaya kwa kutumia nyaraka zinazoonyesha ni bidhaa za biashara kama chai. Sehemu nyingine husafirishwa kwenda Afrika Kusini kutumia mipaka ya Kyela kupitia Malawi na Tunduma kupitia Zambia. Sehemu nyingine ya madawa hutumiwa humu humu nchini ili kupata fedha za kuweza kugharamia matumizi ya humu humu nchini.

249. Baada ya vyombo va dola kuongeza upekuzi kwenye Bandari ya Dar es Salaam, Tume imeelezwa kuwa hivi sasa wasafirishaji wa madawa ya kulevya kutoka Zanzibar wanasafirisha kupitia Mafia na Kilwa na kutoka huko madawa hayo hupelekwa Mtwara ambako hupakiwa upya na kusafirishwa kwenda Afrika  Kusini na Msumbiji.

250. Pamoja na jitihada za vyombo vya dola kuwakamata wasafirishaji ambazo zimefanyika mpaka mwaka huu, Tume inaamini huwa ni wachache kulinganisha na ukubwa wa biashara hiyo. Jitihada za vyombo hivyo zinalenga kwa wasafirishaji na siyo wafanyabiashara wa madawa (drug barons) wenyewe. Wamekamatwa vijana wanaotumika kama kasha (containers) bila kuwafahamu waliowaajiri.

Hali hii haiwezi kutoa mazingira yanayowezesha kukabiliana na tatizo kikamilifu. Tume inaamini ili taifa liweze kukabiliana na ongezeko la madawa ya kulevya, hapana budi kuwasaka na kuwachukulia hatua kali wafanyabiashara wa madawa ya kulevya. Baadhi yao wamo katika jamii yetu. Tume haikuridhishwa na hatua zinazochukuliwa na vyombo vya dola kuwasaka wafanyabiashara hawa.

251. Biashara ya madawa ya kulevya inaleta mapato makubwa ya haraka na haramu. Fedha hizi hutumiwa kuhonga maofisa mbalimbali wa umma ili kufanikisha njama za wahusika. Inaposhamiri, biashara hii huchochea ueneaji wa rushwa na uhalifu mkubwa.

Bila rushwa kuwepo biashara hii haiwezi kufanikiwa. Hali hii imejitokeza kwenye nchi nyingine hasa za Amerika ya Kusini hususan Colombia ambako wafanyabiashara wa madawa ya kulevya walifikia kuwa na nguvu za kushindana na serikali. Hali hii ikiachwa kuendelea itaashiria uibukaji wa vikundi vyenye pesa vinavyoweza kuyumbisha serikali au vyombo vyake.

252. Pamoja na rushwa, athari nyingine ya biashara ya madawa ya kulevya ni kuharibika kwa tabaka la vijana kutokana na matumizi ya madawa hayo. Watumiaji wa madawa ya kulevya huathirika kiafya kutokana na kupumbazika akili, kupoteza uwezo wa kufikiri na wa kufanya kazi na kuongezekewa na tabia ya kutenda uhalifu wa aina mbalimbali. Utumiaji wa madawa ya kulevya unasababisha mmomonyoko wa maadili ya kitaifa.

253. Tume pamoja na kwamba haikupata msaada kutoka vyombo vya dola kuweza kufanya uchambuzi wa kina, imebaini yafuatayo kuwa ndiyo yamechangia katika ongezeko la kasi ya biashara na matumizi ya madawa ya kulevya:

(a) Sera  ya kulegeza masharti ya biashara ambayo haikuambatana na tahadhari; sera hii imeongezea mtiririko wa wafanyabiashara wa nchi yetu kukutana zaidi na watu wa mataifa mengine na hivyo kuiga kwa tamaa ya utajiri wa haraka haraka;

(b) Ongezeko la wawekezaji wa vitega uchumi kutoka nje ya nchi na udhibiti mdogo wa mienendo na matendo yao; uwekezaji umetumiwa na baadhi ya watu kama kivuli cha kuingiza nchini magenge ya wafanyabiashara wa madawa ya kulevya;

(c) Vyombo vya dola kutokuwa vimejitayarisha vya kutosha kukabiliana na ongezeko hilo; vyombo hivyo ni pamoja na Idara ya Usalama wa Taifa, Taasisi ya Kuzuia Rushwa, Idara ya Forodha, Idara ya Uhamiaji na Jeshi la Polisi. Wafanyabiashara wa madawa ya kulevya wanauelewa udhaifu huo na wanautumia kwa manufaa yao;

(d) Upungufu mkubwa wa ajira uliosababisha vijana wengi kukosa kazi; baadhi ya vijana hao ndio waliogeuka kuwa watumiaji wakubwa wa madawa ya kulevya na hivyo kuistawisha biashara hiyo kutokana na “demand”;

(e) Wimbi la ongezeko la vijana mijini;

(f) Kukaa kwa maofisa uhamiaji na wa forodha sehemu moja kwa muda mrefu na hivyo kuzoeana na wasafirishaji.

254. Tabaka la watu lililo chimbuko la kukua kwa biashara ya madawa ya kulevya ni watu wenye madaraka au wafanyabiashara. Hawa wana uwezo wa kutumia nafasi na fedha zao kufukia nyayo za wasafirishaji kwa kuhonga ili ushahidi usifichuliwe. Wanaokamatwa ni watumiaji tu.

Kwa mfano hivi sasa tunao vijana 71 wakitumikia vifungo katika magereza ya nje ya nchi baada ya kukamatwa na madawa ya kulevya. Hakuna hata mfanyabiashara mmoja aliyekwisha kamatwa na kufungwa.

255. Huko Zanzibar Mei 1996, polisi walikamata kasha uwanja wa ndege likiwa na mandrax yenye uzito wa kilo 80 mali ya mfanyabiashara Andrew na Cornel Demello. Wafanyabiashara hao walifikishwa mahakamani na kuachiwa. Mara tu baada ya kuachiliwa walitoroka nchini.

 

 Mapendekezo

256. Ili kukabiliana na tatizo la madawa ya kulevya hapa nchini, pamoja na kwamba Tume haikupata taarifa za kuiwezesha kufanya uchambuzi wa kina wa tatizo hili kutoka kwenye vyombo vya dola, inapendekeza kama ifuatavyo:

(a) Sheria iviagize vyombo vya dola vifanye uchunguzi wa ndani kuhusu wafanyabiashara wanaohusika katika biashara ya madawa ya kulevya na vishauri namna ya kukabiliana na tatizo hilo.

(b) Serikali iichukulie biashara ya madawa ya kulevya kuwa moja ya adui mkubwa wa taifa letu. Taratibu za udhibiti wa mipaka ya nchi yetu pamoja na maeneo mengine ya kuingilia nchini bandarini na viwanja vya ndege ziimarishwe.

(c) Vyombo vya dola vijiimarishe ili vimudu mapambano dhidi ya wimbi la ongezeko la biashara hiyo. Mikakati yao ya kujiimarisha iambatane na upatikanaji wa zana za kisasa za kufanyia kazi ya utambuzi pamoja na mafunzo ya wataalamu.

(d) Pawepo ushirikiano wa karibu zaidi baina ya vyombo mbalimbali vya dola vyenye jukumu la kupambana na biashara ya madawa ya kulevya.

(e) Jitihada kubwa zaidi ielekezwe katika kutambua wanaohusika na usafirishaji badala ya watumiaji.

(f) Serikali ihamasishe jitihada za kuelimisha umma juu ya madhara ya matumzi ya madawa ya kulevya kupitia vyombo vya habari, mafunzo mashuleni na sinema vijijini.

(g) Udhibiti wa humu nchini uoanishwe na mawasiliano ya karibu zaidi na vyombo vya mataifa mengine vyenye majukumu ya udhibiti wa madawa ya kulevya.

(h) Maofisa wanaohusika na udhibiti wa madawa ya kulevya wasikae kwenye kituo kimoja kwa zaidi ya miaka miwili.

 

Je, unajua Jaji Warioba katika ripoti hii aliyoiandaa mwaka 1996 alipendekeza nini kuhusu idara ya Uhamihaji? Usikose JAMHURI wiki ijayo. Mhariri.