Na Lookman Miraji

Ikiwa ni mwezi Disemba ambapo hivi karibuni mwaka 2024 utakwenda kuhitimika kwa sikukuu za mwisho mwaka, mataifa mawili ya Tanzania na Urusi yameendelea kudumisha ushirikiano wake uliokuwepo tangu miongo kadhaa nyuma.

Ushirikiano kati ya Tanzania na taifa la Urusi umekuwa ukizidi kudumishwa na wawakilishi wa mataifa hayo mawili, yakiongozwa marais wake, Dkt:Samia Suluhu Hassan pamoja nae Vladimir Putin ambae ni Rais wa taifa la Urusi.

Katika kuelekea kuhitimika kwa mwaka 2024 , Urusi kupitia ubalozi wake nchini Tanzania unaoongozwa na Balozi wake Andrey Avetisyan umetoa ripoti ya mwaka 2024 ambayo imezungumzia mafanikio yaliyopigwa, mikakati iliyowekwa kuelekea mwaka ujao pamoja hatua muhimu ambazo ziko katika mchakato wa kukamilika hivi karibuni.

Akitoa ripoti hiyo katika hafla na waandishi wa habari, Balozi wa Urusi nchini Andrey Avetisyan amezitaja hatua muhimu zilizopigwa kati yao na Tanzania katika sekta mbalimbali ikijumuisha elimu, biashara pamoja na utalii.

    SEKTA YA ELIMU.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotolewa imeelezea kwa namna Tanzania inavyoendelea kunufaika katika sekta ya elimu kupitia fursa za watanzania kwenda kupata ujuzi na taaluma nchini Urusi. Akizungumza Balozi Avetisyan amesema kuwa mpaka sasa Urusi ina jumla ya wanafunzi 500 wakitanzania wanaoendelea na masomo nchini humo. Wanafunzi hao wamekuwa wakipata ufadhili wa masomo nchini humo kutoka kwa serikali ya Urusi kupitia mfumo rasmi wa uombaji ambao umekuwa ukitangazwa mara kwa mara na ubalozi wa Urusi nchini.

Aidha balozi huyo ameongeza kuwa katika kuzidi kuiboresha sekta hiyo ya elimu, ukiachana na idadi ya wanafunzi wanaochaguliwa kupata ufadhili wa masomo nchini humo kila mwaka wamelenga kutoa nafasi kwa watanzania takribani 150 kwa mwaka ujao. Takwimu zinaonesha idadi hiyo itazidi kupanda kutoka idadi ya watanzania 90 waliopata fursa hiyo kwa mwaka uliopita.

     MAGEUZI YA LUGHA YA KISWAHILI.

Tukigeukia katika nafasi ya lugha ya Kiswahili katika mahusiano baina ya nchi hizo mbili, Balozi Avetisyan amesema kuwa Urusi inaunga mkono jitihada za serikali ya Tanzania kuirasimisha lugha ya Kiswahili kuwa lugha rasmi katika nchi jumuiya za Umoja wa mataifa. Na kwa kulithibitisha hilo balozi huyo amebainisha kuwa mwaka jana serikali ya Urusi ilipitisha mpango wa lugha ya Kiswahili kufundishwa mashuleni na mpaka kufikia sasa idadi ya shule na vyuo 5 nchini humo vimeanza kufundisha lugha hiyo.

Hatua hiyo imetajwa kama sehemu ya mahusiano kati Urusi na Tanzania ikichagizwa na ukuaji wa lugha hiyo inayozidi kushamiri ulimwenguni kwa sasa hivyo balozi Avetisyan anaamini kuwa idadi ya shule na vyuo vinavyofundisha lugha ya Kiswahili itaongezeka.

 UTALII NA BIASHARA.

Katika sekta hizi mbili za utalii pamoja na biashara baina ya nchi hizo takwimu zinaonesha kuwa mpaka kufikia miaka ya hivi karibuni sekta hizo bado zimekuwa katika kiwango cha chini katika nchi hizo mbili.

Hivi karibuni Tanzania imepokea tuzo za dunia za utalii (World Travel Award) ikitambulika kama sehemu maridhawa zaidi kwa utalii wa safari duniani.

Hatua hiyo ya ushindi imeamsha wengi kuitambua Tanzania kama sehemu sahihi zaidi linapokuja suala la utalii.

Balozi Avetisyan nae amekiri kuwa Tanzania ni sehemu salama zaidi katika ukanda wa Afrika mashariki na kati na tayari wameshaweka mipango kuongeza ushawishi kwa makampuni ya kitalii ya Urusi kuja kuvitembelea vivutio vilivyopo hapa nchini na kupeleka ujumbe kwa watu wengine nchini Urusi pamoja na kuandaa safari za kutembelea vivutio mara kwa mara hapa nchini.

Akiongeza balozi huyo amesema kuwa Urusi iko tayari pia kutangaza utalii wa nchi ya Urusi hapa nchini kwani itasaidia kuleta maendeleo ya uchumi kati ya mataifa hayo mawili.

Katika upande mwingine pia amesema kuwa kumekuwa na mipango baina ya Tanzania na Urusi huku miongoni mwake ni ujio wa safari za ndege. Mpango huo umeelezewa kuwa msaada mkubwa kwa sekta ya utalii na kibiashara katika nyanja ya usafirishaji. Balozi Avetisyan amebainisha kuwa safari hizo za ndege zinatarajiwa kuanza kuanzia mwakani kama endapo kila kitu kitaenda sawa.

“Tayari tumejaribu kuzungumza na makampuni ya ndege na yako tayari kwa hilo kama endapo kutakuwepo na abiria. Jambo hili limekuwa likienda taratibu lakini nina imani kuwa tutafanikiwa.” Alisema balozi huyo.

SEKTA YA NISHATI.

Kwa siku za hivi karibuni Tanzania inatajwa kama nchi inayokuwa kwa kasi kubwa katika matumizi ya nishati. Hatua hiyo ni matokeo ya jitihada za serikali katika kuleta mageuzi kutoka katika matumizi ya nishati chafu (mkaa, kuni na nk) kwenda katika matumizi ya nishati safi(Gesi).

Jitihada hizo zimeonekana kuzaa matunda kwani Tanzania anatarajiwa kuwa mwenyeji mkutano mkuu wa nishati wa Afrika utakaoangazia dira ya maendeleo kuelekea malengo ya kuhakikisha mpaka kufikia mwaka 2030 watu zaidi ya millioni 300 wanafikiwa na nishati ya umeme. Mkutano unaotarajiwa kufanyika mapema mwakani 2025.

Aidha Balozi huyo wa Urusi katika hilo amekiri ukuaji wa Tanzania katika upande huo wa sekta ya nishati na kuongeza kuwa serikali ya Urusi iko tayari kushirikiana na Tanzania katika kuleta mageuzi ya nishati nchini.

Pia balozi Avetisyan ameitaja kampuni ya usambazaji nishati kutoka nchini urusi ya GAZPROM kuwa iko tayari kushirikiana na washirika wengine kuleta mabadiliko katika soko la Tanzania.

"Tutafurahi kumuona, Dkt: Tulia nchini Urusi" balozi Avetisyan ameyasema kufuatia mjadala uliokuwepo katika mkutano wa 149 wa umoja wa mabunge duniani (IPU) uliofanyika miezi kadhaa iliyopita mjini Geneva, nchini Uswisi.

“Rais Putin alikutana na Tulia ulikuwa ni wakati mzuri kikubwa ni kuwa tutafurahi kumuona tena Dkt:Tulia nchini Urusi, na ninachojua amepewa mualiko na bunge la Urusi kuja Urusi tena kama spika bunge la Tanzania au kama muwakilishi wa umoja wa mabunge duniani (IPU) ,atakaribishwa vizuri sana nchini Urusi” Alisema balozi Avetisyan.

Ripoti hiyo imetolewa hapo jana na balozi wa Urusi nchini Tanzania Andrey Avetisyan ikiangazia masuala mbalimbali yanayolihusu taifa hilo la Urusi.