*Wamo Polisi, Kada CCM, wafanyabiashara
*Vigogo Polisi Kigoma, Mugumu wahusishwa
Idara ya Ulinzi, Kitengo cha Intelejensia cha Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), imetoa ripoti ya ujangili iliyo na majina ya wahusika wakuu na namna wanavyolindwa na vyombo vya dola nchini. JAMHURI imepata ripoti hiyo ya kurasa 30 iliyosainiwa na Mhifadhi wa Intelejensia, Renatus Kusamba.
Kubwa zaidi kwenye ripoti hiyo ni kwamba hali ya ujangili katika hifadhi zote nchini inatisha, usalama wa wanyamapori uko shakani, idadi ya wanyamapori inaelekea kupungua, na juhudi za lazima zinatakiwa kuchukuliwa na jamii nzima katika kukabiliana na hali hiyo.
Chanzo cha kuwapo uchunguzi huo ni mauaji ya faru jike na mtoto wake katika Hifadhi ya Taifa Serengeti, Mei mwaka huu. Ingawa dhima ya kitengo hicho cha intelejensia ilikuwa kufuatilia mauaji ya faru hao, mambo mengi yameibuliwa kwenye uchunguzi huo.
Imebainishwa kuwa mtandao wa ujangili nchini unahusisha wafanyabiashara, watumishi wa idara za Serikali (Polisi, na Idara ya Wanyamapori – watumishi wa halmashauri) na baadhi ya raia wa kigeni.
“Kundi hili ndilo linalofanya mipango ya kutafuta na kuleta silaha (bunduki hasa za kivita) na risasi na kuwapatia baadhi ya majangili/majambazi hao. Wafanyabiashara hao hukusanya meno (ya tembo na faru) na kuyasafirisha kutoka wilaya zinazozunguka Hifadhi ya Serengeti. Wafanyabiashara wakubwa wanawafadhili wafanyabiashara wadogo wa meno ya tembo.
“Wafanyabiashara wako katika wilaya za Bariadi, Kasulu, Kibondo na Lunzewe wilayani Kahama,” inasema sehemu ya taarifa hiyo.
Pamoja na makundi hayo, taarifa ya Tanapa imebaini kuwa waganga wa kienyeji wanatumika mno kwenye ujangili. Wanatumiwa kuwazindika majangili na majambazi kwa imani kwamba hawataweza kukamatwa wakati wa kuendesha vitendo hivyo.
Kwa upande mwingine, baadhi ya viongozi wa Polisi wanatuhumiwa kuwamo kwenye mtandao wa kuwalinda majangili. Hayo yanathibitishwa na ripoti hiyo katika ukurasa wa 20 kwa mfano mmoja wa matukio hayo.
“Asubuhi ya Juni 12, 2012 alikamatwa mtuhumiwa mwenye umri wa miaka 43 (jina tunalihifadhi kwa sasa) na bastola yenye risasi 10. Ni mkazi wa Magu. Katika mahojiano alionyesha kibali cha umiliki (photocopy) ambacho kinatia shaka na alidai bastola hiyo aliletewa na polisi aitwaye Mbogo aliyeko Mwanza na kwamba yeye hajui kuitumia.
“Aliachwa Kituo cha Polisi Mugumu Wilaya ya Serengeti ili mpango wa kufuatilia uhalali wa umiliki wake ukifanyika, lakini OCD wa Mugumu alimwachia muda mfupi baada ya askari wa Tanapa kumkabidhi kituoni hapo,” imesema ripoti.
Katika tukio jingine, ripoti inasema Julai 12 mwaka huu, taarifa za kiintelejensia zilionyesha kuwa mtuhumiwa mkuu wa ufadhili wa ujangili (jina tunalihifadhi kwa sasa), mkazi wa Kijiji cha Busunzu, Kibondo mkoani Kigoma, alionekana katika Kijiji cha Kifula wilayani Kibondo.
Mtuhumiwa alikuwa akisakwa kwa muda mrefu kutokana na kutajwa na watuhumiwa wengine waliokamatwa Mei 11 mwaka huu, wilayani Serengeti wakiwa na risasi 430 na kufunguliwa kesi namba MUG/IR/1330/2012.
Watuhumiwa hao walimtaja kiongozi wao (mkazi wa Busunzu) wanayesema huingiza silaha za kivita na risasi kutoka Burundi. Silaha hizo ndizo zinazotumika kufanyia ujangili katika Hifadhi za Taifa za Serengeti, Tarangire, Ziwa Manyara, Katavi, mapori ya akiba ya Moyowosi, Maswa, Rukwa/Rukwati na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.
“Mfadhili/jangili huyu ana uwezo mkubwa wa kifedha na ana mtandao mkubwa ulioenea karibu nchi nzima palipo na maliasili,” imesema ripoti.
Ripoti inasema kwamba afisa wa intelejensi alitumwa Juni 12 mwaka huu kumfuatilia. Alionekana katika Kituo cha Polisi Kifula akifungua kesi ya kuibiwa vitu katika baa yake.
“Mtuhumiwa akiwa kituoni hapo, Kitengo cha Intelejensia kilichokuwa Serengeti kilimuagiza afisa wake aliyekuwa akimfuatilia amkamate mara moja kwa kuomba msaada wa polisi kituoni hapo. Hata hivyo, afisa huyo hakupata ushirikiano ikamlazimu kutumia mbinu za kisasa kufukuzana naye na kisha kufanikiwa kumkamata na kumrudisha kituoni.
“Wakati huo Kikosi cha Tanapa (Serengeti) kwa kushirikiana na askari polisi kutoka Kituo cha Mugumu, walikuwa wako njiani kumfuata mtuhumiwa huyo na walipofika walimkuta ameshakamatwa.
“Mtuhumiwa alipelekwa katika Kituo cha Kibondo ili kusubiri askari kutoka Serengeti wamchukue. Mara baada ya askari wetu kufika kituoni hapo walikataliwa kumchukua kwa amri ya RPC Kigoma, RCO Kigoma, OCD Kibondo na OCD-CID Kibondo. Kutokana na hali hiyo RPC na RCO Kigoma walituma kikosi maalumu cha kumfuata na kumpeleka Kituo cha Polisi Kigoma mjini.
“Hali hiyo ililazimu kuomba msaada kwa Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa Tanzania ili awasiliane na ngazi za juu kuangalia uwezekano wa kumchukua mtuhumiwa huyo na kumfikisha Kituo cha Polisi Wilaya ya Serengeti (Mugumu) aweze kujibu mashitaka.
“Mkurugenzi Mkuu wa Tanapa alituma Kamanda mstaafu Venance Tossi kwenda Kigoma kwa ndege ya shirika kumchukua mtuhumiwa huyo na kumleta Serengeti-Seronera na kumkabidhi mtuhumiwa huyo kwa Mkuu wa Hifadhi na kupelekwa Kituo cha Polisi Mugumu,” imesema ripoti.
Watuhumiwa wengine wa ujangili wanaotajwa ni Bwana Nyama Wilaya ya Karatu aliyetajwa kwa jina moja la Simon. Anamiliki rifle aina ya 404, Mzee Lazaro anayetajwa kwamba ni Mwenyekiti wa CCM Kitongoji cha Karatu, na watumiwa wengine ambao ni watu maarufu.
JAMHURI ITACHAPISHA RIPOTI KAMILI KATIKA MATOLEO YAJAYO.