Serikali ya Kenya imekasirishwa na ripoti iliotolewa na kiongozi wa Muungano wa Ulaya kuhusu uchaguzi mkuu wa urais mwaka uliopita.
Marietje Schaake alitoa ripoti mapema siku ya Jumatano katika mji mkuu wa Ubelgiji , Brussels baada ya kusema kuwa serikali ya Kenya haikuwa tayari kukutana naye.
Taarifa kutoka ubalozi wa Kenya mjini Brussels inasema kuwa madai hayo sio ya ukweli na kwamba alikiuka makubaliano kati ya taifa hilo na EU
Taarifa hiyo iliendelea kusema kwamba mpango wa kuzuru taifa hilo ulikubaliwa kati ya katikati ya mwezi Februari hadi katikati ya mwezi Machi.
Bi Schaake alisema katika taarifa yake kwamba alikuwa anatoa ripoti hiyo ya kuafikia sheria za muungano huo za kutoa ripoti miezi mitatu baada ya uchaguzi.
Ripoti hiyo inaangazia wasiwasi kuhusu utumizi wa mali ya umma na vitisho dhidi ya maafisa wa uchaguzi wakati wa uchaguzi huo uliokumbwa na utata.
Inatoa mapendekezo 29 kuhusu vile mfumo wa uchaguzi wa Kenya unavyoweza kuimarishwa, lakini bi Schaake alisema kwamba ni Wakenya wenyewe wanaoweza kutatua tatizo hilo.
Rais Uhuru Kenyatta alichaguliwa katika uchaguzi wa marudio mnamo mwezi Oktoba ambao ulisusiwa na kiongozi wa upinzani Raila Odinga.
Uchaguzi wa kwanza uliofanyika mnamo mwezi Agosti, ambao bwana Kenyatta aliibuka mshindi ulifutiliwa mbali na mahakama ya juu.
Uchaguzi huo ulikumbwa na ghasia huku makundi ya haki za kibinaadamu yakisema kuwa takriban watu 50 wengi wao wakiwa wafuasi wa upinzani waliuawa na maafisa wa polisi.
Maafisa wa polisi hatahivyo wamepinga madai hayo.

SOURCE: BBC SWAHILI