Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iliyowasilishwa bungeni, imevuja.

Ina taarifa za kutisha ndani yake na ni wazi inawaanika Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema na Gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa Benno Ndulu.

Ripoti hiyo iliyochapishwa na gazeti hili la JAMHURI neno kwa neno, ingawa haikulenga kutafuta mwizi, kwani CAG alifanya ukaguzi maalum wa miamala (transaction) iliyofanyika katika akaunti ya ‘Escrow’ ya Tegeta pamoja na umiliki wa Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL); imefunua uozo.

Ingawa haikutaja majina ya watu waliopokea fedha katika mgao uliosambaa kwa mawaziri, majaji, watendaji ndani ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kwingineko, ripoti hiyo ilielekeza uchunguzi wa kina kufanywa na vyombo vya dola ikiwamo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Taarifa zilizopatikana zinaonyesha kuwa TAKUKURU baada ya kufanya uchunguzi wa kina, ilikuta akaunti ya Kampuni ya VIP Engineering and Marketing iliyopo katika Benki ya Mkombozi jijini Dar es Salaam iliyopokea fedha kutoka BoT ndio ilitumika kusambazia wakubwa hao fedha.

Baada ya hukumu iliyotolewa na Jaji Utamwa wa Mahakama Kuu ya Tanzania kumaliza mgogoro kati ya Kampuni ya VIP inayomilikiwa na James Rugemalira na Mechmar ya Malaysia, mgogoro mpya ulianza serikalini.

Mgogoro huu ulihusu uhalali wa fedha hizo kulipwa au la, na hapo ndipo yalianza mashinikizo ya aina yake kutoka kwa watendaji na baadhi ya viongozi wa kisiasa.

 

Maswi akataa malipo yasitolewe

 

Taarifa ya CAG iliyowasilishwa bungeni inaonyesha kuwa Kampuni ya PAP baada ya kuwa wamepata hukumu Septemba 5, 2013 walipeleka maombi Wizara ya Nishati na Madini wakitaka Serikali iwalipe fedha zao kwa kigezo kwamba walikuwa wamiliki halali wa fedha na mali za IPTL.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi alikataa kutoa malipo hayo. Baada ya mvutano mkali, aliamua kuandika barua ya kuomba ushahidi wa kisheria kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Werema.

Kupitia barua yenye Kumb. Na. CBR.88/147/29 ya Septemba 16, 2013; Maswi alimwandikia AG akipinga malipo hayo kwa hoja mbili.

Hoja ya kwanza alisema haamini kama fedha zote zilizokuwa katika akaunti ya Escrow zilikuwa za PAP kwa vile ziliwekwa katika akaunti hiyo kutokana na mgogoro wa tozo za ‘capacity charge’ ambazo ni gharama za uwekezaji kati ya TANESCO na IPTL. Akasema umiliki halisi wa fedha hizo ungefahamika pale tu mgogoro huo utakapotatuliwa.

Hoja ya pili, asisisitza hoja ya kwanza kuwa PAP anastahili kupata malipo ya kiasi kitakacholipwa kwa IPTL baada ya mgogoro huo kutatuliwa na siyo kiasi chote kilichokuwapo kwenye akaunti ya Escrow. Alihitimisha kwa kuagiza pande zinazohusika kukaa na kukokotoa stahiki ya TANESCO na IPTL.

Maswi hakuishia hapo, taarifa ya CAG inaonyesha kuwa Sepemba 26, 2013 alimwandikia barua Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Servacius Likwelile yenye Kumb. Na. CDB.88/417/31 kutaka kiitishwe kikao cha pamoja kujadili suala la malipo hayo.

Kikao hicho kilifanyika Sepemba 24 na kuhudhuriwa na maofisa wa Wizara ya Fedha, Wizara ya Nishati na Madini, BoT na TANESCO. Kikao kiliunda kamati ndogo ya kufuatilia suala hilo na kuazimia kuwa IPTL na TANESCO wamalize mgogoro wao kwanza ndipo malipo yafanyike.

Ikumbukwe mgogoro uliomalizwa Septemba 5 na Jaji Utamwa, ulikuwa kati ya VIP Engineering na Mechmar wakigombania malipo ndani ya IPTL, hivyo Maswi alikuwa akisema mgogoro kati ya TANESCO na IPTL uliowasukuma kufungua Escrow ulikuwa bado upo hai na hivyo fedha haziwezi kutolewa.

Baada ya msimamo mkali wa Maswi, Katibu Mkuu wa Hazina, Dk. Likwelile, Gavana wa BoT, Profesa Ndulu na AG Werema waliendelea kuwasiliana wao kwa wao hadi malipo yakafanywa.

Werema aagiza PAP walipwe

Ripoti ya CAG inaonyesha kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Likwelile aliamua kuanza kuwasiliana na AG Jaji Werema na kumwacha kando Maswi.

Sepemba 30, 2013 Dk. Likwelile alimwandikia Jaji Werema barua yenye Kumb. Na. CAC/184/211/01/23, iliyojibiwa na Jaji Werema kupitia barua yenye Kumb. Na. AGCC/E.80/6/65 ya Oktoba 2, 2013.

Ripoti inasema: “Alimwarifu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dk. Servacius Likwelile kuwa ameipatia ripoti husika na kwamba jambo pekee linaloweza kuleta tatizo ni kuhusu fedha zilizowekezwa na Benki Kuu katika hati fungani (Kielelezo 20).

“Mwanasheria Mkuu wa Serikali alishauri kuwa fedha izo zilipwe kwa IPTL ili jambo hilo lifungwe na kuiwezesha Serikali kujiepusha na mashauri yasiyo na tija kwake, na kusisitiza kuwa uamuzi wowote wa kuota fedha kwenye akaunti ya Escrow unalindwa na hukumu ya Mahakama Kuu ya Tanzania (Mh. Jaji Utamwa) ya tarehe 5 Sepemba, 2013 (Rejea Kielelezo 20).”

 

Kasi ya Gavana Kulipa inatisha

 

Gavana wa BoT, Profesa Ndulu, Novemba 25, 2013 aliandika barua kwa Mwenyekiti wa Kampuni ya IPTL, Harbinder Singh Sethi na Novemba 28, 2013 Sethi akafungua akaunti katika Benki ya Stanbic, kisha tarehe hiyo hiyo akaijulisha BoT taarifa za akaunti aliyoifungua na tarehe hiyo hiyo mabilioni yakalipwa.

“Baada ya BoT kupokea maelekezo ya Bw. Harbinder Singh Sethi, malipo ya kwanza ya kiasi cha Sh. 8,020,522,330 na US$ 22,198,544 yalifanyika tarehe 28 Novemba, 2013 katika akaunti za PAP zilizofunguliwa katika Benki ya Stanbic (Kielelezo 29).

“Baada ya malipo hayo kufanyika, umiliki wa hati fungani zenye thamani ya Sh. 157,622,910,000 ikijumuisha mtaji (principle amount) wa Sh. 146,567,363,967 na riba ya Sh. 11,055,546,033 ulihamishwa kwenda PAP tarehe 6 Desemba, 2013 (Kielelezo 30),” inasema sehemu ya taarifa hiyo.

 

Werema aagiza kodi isilipwe

 

Baada ya uamuzi wa Mahakama, TRA iliamua kudai kodi, lakini wakagonga mwamba. “Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia barua Kumb. Na. AGCC/E.080/6/70 ya tarehe 18 Novemba alimfahamisha Gavana wa Benki Kuu Prof. Benno Ndulu kuwa hakukuwa na kodi ya VAT katika fedha zilizokuwepo kwenye akaunti ya Escrow hivyo kutokuwepo kwa kodi iliyopaswa kukusanywa (Kielelezo 87).

“Hata hivyo, katika mahojiano tuliyofanya na Kamishna Mkuu wa Kodi, alithibitisha kuwa TRA wanaendelea na hatua za kuikusanya kodi husika kutoka IPTL (Rejea Kielelezo 84 na 87),” inasema taarifa ya CAG.

Taarifa hiyo imebaini udanganyifu wa hali ya juu, ambako wakati Piper link ilinunua hisa 7 au asilimia 70 ya hisa kutoka kwa IPTL kwa gharama ya dola milioni 6 (karibu Sh bilioni 10), baadhi ya watumishi katika TRA walishiriki udanganyifu na kuonyesha kuwa hisa hizo ziliuzwa kwa Sh milioni 6.

Kampuni ya Piper Link nayo iliuza hisa hizo 7 siku hiyo hiyo iliyozinunua kwa kampuni ya PAP kwa gharama ya dola milioni 20 (karibu Sh bilioni 36), lakini kwa udanganyifu wa hali ya juu maafisa wa TRA wakaonyesha kuwa PAP ilinunua hisa hizo kwa dola 300,000 (sawa na Sh milioni 480). Ni kwa njia hiyo, Serikali ilipoteza kodi.

 

JAMHURI lilipowasiliana na AG Jaji Werema kupata maelezo yake juu ya ripoti hii ya ukaguzi na kumjulisha kuwa zipo taarifa alihongwa dola milioni 5 kufanya uamuzi huu; ajibu kwa Kiingereza na katika tafsiri isiyo rasmi alisema: “Unayaamini hayo kwa chembe yoyote? Ikiwa unayaamini, basi nitakie safari njema ya kuondokana na umasikini. Ikiwa hauyaamini, basi sikitika kama nifanyavyo.”

Baada ya kuhoji kwa nini atajwe yeye, alisema wapo watu waliojipanga kumharibia jina na anafahamu jinsi wanavyopokea au wanavyoomba kupokea rushwa ya magari na fedha tasilimu, lakini wanataka sasa kuhamishia mpira kwa watu wengine.

Mwisho wa mazungumzo, akasema: “Umetaka maelezo yangu. Bunge linapaswa kujizuia kujadili IPTL kwani masuala yanayoibuliwa ni masuala yanayosubiri uamuzi wa Mahakama. Kuna kesi nne katika Mahakama ya Biashara.

“Ukaguzi wa akaunti ya IPTL ni suala la kawaida, lakini uhalali (kisheria) wa kuhamisha fedha kutoka kwenye akaunti ya Escrow ni suala linalosubiri mashitaka mahakamani.

“Ni dharau kwa Mahakama kuifanyia mzaha. Hata nje ya Tanzania, SCB ina kesi katika uhamishaji (wa fedha). Naomba tupigane vita katika uwanja sahihi. Bunge si moja ya viwanja hivyo, ambako sheria ya asili hutawala, na ambako mbilikimo na mapandikizi ya watu hawakutawazwa kutoa haki,” akasema Jaji Werema.

 

Wakubwa wachota mamilioni

 

Taarifa nyingine ya uchunguzi uliofanywa na TAKUKURU inaonyesha kuwa wakubwa wamegawiwa mamilioni ya fedha zilizoingizwa kwenye Benki ya Mkombozi ya Rugemalira.

Katika orodha ya waliogawiwa fedha na Rugemalira wamo Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka; watumishi wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini; mawaziri wa zamani – Andrew Chenge, William Ngeleja, na Daniel Yona-; na majaji Profesa Eudes Ruhangisa na Jaji Aloysius Mujulizi.

Wakubwa hawa wamepokea kati ya Sh milioni 40.2 hadi Sh bilioni 1.6. Chenge, Profesa Tibaijuka na Kyabukoba & Associate wao wamepokea Sh bilioni 1.6 kila mmoja, huku Jaji Ruhangisa akipokea Sh milioni 404.2. Mfanyakazi wa Ardhi, Rugonzibwa Theophil yeye alipokea Sh milioni 232.4. (Soma kielelezo Uk. 1).

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini, Philip Saliboko aliyeteuliwa kuwa Mfilisi wa IPTL, yeye aliingiziwa Sh milioni 40.2 kwenye akaunti yake. JAMHURI ilipowasiliana naye, alikiri kupokea fedha hizo, ila akasema ameangukia katika mkumbo.

“Kaka mimi ni kweli nilipokea fedha hizo, ila nimekuwa victim of the circumstance (mhanga wa mazingira). Nilinunua shamba kule Malela Mkuranga karibu na Vikindu lenye ukubwa wa ekari 50 na jingine lenye ukubwa wa ekari 20.

“Mjomba wake Rugemalira akataka nimuuzie moja ya mashamba yangu hayo ya Vikindu. Nilimwambia nitamuuzia ekari 20 kwa Sh milioni 65. Alinilipa cash Sh milioni 5 nikabaki namdai Sh milioni 60. Baadaye akaniambia nifungue akaunti Benki ya Mkombozi mjomba wake atamsaidia kulipa deni hilo.

“Nikafungua akaunti, nikakuta ameniingizia Sh milioni 40 tu, kimsingi ikawa bado namdai. Sasa nikasikia kuwa fedha nilizolipwa zimetokana na hili suala la IPTL, kimsingi nilisononeka. Sikushiriki kwa njia yoyote na wala sikuwa nikilipwa fadhila kwa njia yoyote,” alisema Saliboko.

Kwa upande wake, Jaji Ruhangisa aliyechotewa Sh milioni 404 alikaririwa na gazeti la Raia Mwema akisema kuwa fedha hizo alipewa kwa ajili ya masuala ya kifamilia kama sherehe, harusi na misiba.

Naye, Waziri Profesa Tibaijuka yeye alikaririwa na gazeti hilo alisema kuwa fedha hizo alipewa kwa ajili ya kuendeleza shule zake, ingawa wachunguzi wanasema hawakuona fedha hizo zikingia katika akaunti za shule anazomiliki.

 

Wafadhili waendelea kubana

 

Mataifa yanayounda Umoja wa Wahisani umeendelea kuzuia misaada kwa Tanzania wakitoa masharti kuwa Tanzania ijadili na kutolea uamuzi suala la kashfa ya IPTL kwanza, na wahusika wachukuliwe hatua ndipo waruhusu misaada.

Taarifa zinasema hata Marekani imesitisha kwa muda msaada wa Millenium Challenge Corporation (MCC) uliopaswa kuanza Julai, mwaka huu.

Mkutano wa Bunge unaoendelea mjini Dodoma unatarajiwa kutoa majibu au suluhisho la kashfa hii baada ya Ripoti ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) itakapowasilisha ripoti ya uchunguzi uliofanywa na CAG.

Kuna kila aina ya dalili kuwa Serikali itakuwa katika wakati mgumu, na pengine hata kuwalazimu baadhi ya mawaziri kujiuzulu.

Ingawa Waziri Mkuu Mizengo Pinda hatajwi moja kwa moja kwenye ripoti ya CAG, anaweza kuwajibishwa kutokana na kauli zake za mara kwa mara kwamba fedha za Escrow si za umma. Pia anaweza kuwajibishwa kwa sababu yeye kama kiongozi mkuu wa shughuli za Serikali kwa kila siku, alipaswa atambue na kumshauri vema Rais kuhusu fedha hizo.