ujangili nje nje
*Wanyamapori wanauzwa bila hofu
*Wateja wakuu ni vigogo serikalini
Kipindi cha uwindaji kinachoruhusiwa kisheria kinachoanza Julai hadi Desemba kila mwaka kimekwisha. Hii haina maana kwamba ulaji wanyamapori umekoma.
Nipo njiani naelekea mkoani Iringa. Kilometa 40 hivi kutoka mjini Morogoro, tunafika katika eneo linaloitwa Lugano. Hapa kunachomwa nyama za kila aina, lakini zinazotawala zaidi ni za mbuzi na swala. Kwa kutambua kuwa naweza kupata nyama ya swala, najenga urafiki na wauza nyama hawa. Nao, bila hiyana wanakuwa wachangamfu kwangu.
Swali langu la kwanza kwao ni, “Naweza kupata nyama ya swala?” Mmoja wa vijana hawa anajibu, “Sema jingine kaka, nyama umepata.” Nauliza swali la pili, “Naweza kupata nyama ya nyati au aina nyingine tofauti na swala?” Najibiwa, “Hapa nyati hupati, labda uende Mkata. Mkata ndiyo kwenye kila kitu.”
Naelekezwa kwamba kutoka hapa Lugano hadi Mkata ni mwendo kama wa kilometa 10 na ushei hivi. Maneno ya vijana hawa ya kwamba Mkata ndiyo kila kitu, yananifanya niwe na shauku ya kufika katika kijiji hicho. Kweli, napanda basi tayari kuelekea Iringa. Punde si punde, kwa msaada wa kondakta na kibao cha utambulisho, napaona Mkata. Naendelea na safari yangu hadi Iringa, lakini akili yangu inanisukuma niandae siku maalumu kwa ajili ya kufuatilia taarifa hizi.
Nasukumwa na ukweli kwamba vijiji kama Lugano, Mkata na Doma vipo jirani kabisa na Hifadhi ya Taifa ya Mikumi. Vijiji hivi vinapitiwa na barabara kuu ya Morogoro-Iringa. Wakubwa wanapita hapa kila siku. Kama hivyo ndivyo, iweje ujangili ushamiri kwa kiasi hiki cha kutisha?
Mwishoni mwa Desemba naamua kufunga safari kutoka Dar es Salaam kwenda Mkata na Doma. Kabla ya safari nampigia simu Kamanda wa Kikosi cha Kupambana na Ujangili katika Wizara ya Maliasili na Utalii, Faustine Masalu.
“Kamanda naelekea mkoani Morogoro kufuatilia taarifa za ujangili. Nakupa taarifa hizi kwa sababu huko naweza kukutana na mambo yasiyokuwa ya kawaida. Lakini kubwa itanipasa niweze kushiriki kununua nyamapori na hata kusafiri nayo bila kibali, kisheria nikikamatwa naweza kushitakiwa. Nakupa taarifa hii kama kinga kwa linaloweza kunipata,” huu ndiyo uliokuwa ujumbe wangu kwa Masalu, kabla ya kuanza safari kwa kutumia gari langu.
Muda ni saa tano asubuhi. Naanza safari ya kwenda Morogoro. Kwa kutambua ugumu wa kazi ninayokwenda kuifanya, namchukua mwandishi mwenzangu, Edmund Mihale.
Tunakwenda hadi Lugano. Hapa tunaegesha gari pembeni kwa ajili ya kuanza kazi. Mvua kubwa inanyesha. Majiko ya nyama ni mengi. Tunaomba tuuziwe nyamapori, lakini kwa hadaa, baadhi ya wauzaji wanatupatia nyama ya mbuzi. Wote tunashituka. Kuona hivyo, mmoja anatuelekeza kwenye jiko lake.
Kweli, tunakula nyama yenye ladha na sifa zote za swala. Kazi imeanza. Nakumbuka kwamba nilishaelezwa na hawa hawa vijana kwamba nyama za kila aina zinapatikana Mkata, mahali ambako sifa zake zinafanana na Mkata ya Handeni, mkoani Tanga, ambako kunauzwa nyama nyingi za mbuzi, lakini si swala na wanyamapori wengine.
Tunaanza safari kwenda Mkata. Si mbali. Baada ya kilometa tano hivi, tunakuta gari la Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) aina ya Land Rover likiwa limepinduka na kuwaumiza askari na raia waliokuwamo. Ni mali ya Kikosi cha 401.
Wanajeshi hawa walikuwa wakitoka kumzika mwenzao Kigamboni, Dar es Salaam, na sasa walikuwa njiani kurejea Songea. Kama ilivyo ada, tunashiriki kutoa huduma kwa wapiganaji na makamanda hawa. Magari mengi yanafika, yanasimama na kuuliza aina ya msaada unaotakiwa. Mwisho, majeruhi wote, isipokuwa mmoja, wanapelekwa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa matibabu.
Kuona hivyo, tunashawishika kuendelea na safari yetu. Vijana wawili wanaomba lifti. Nawauliza wanakokwenda. Wanajibu kwamba wao ni wakazi wa Mkata. Kusikia hivyo, haraka haraka nawakaribisha waingine katika gari. Njiani naanza kuwauliza kama wana uwezo wa kuniwezesha kupata nyama ya swala. Mmoja anajibu, “Sisi hatuuzi swala, lakini tunaweza kukupeleka kwa wanaouza.” Namwuliza kama naweza kupata aina nyingine ya wanyamapori.
“Hapo kila kitu utapata, hakuna wasiwasi,” anajibu kwa lafudhi ya Kimaasai. Baada ya kilometa kama saba hivi, tunafika Mkata. Nashangaa kuona magari mengi yakiwa yameegeshwa kando ya barabara. Nauliza kama kuna sherehe mahali hapa. Mmoja wa vijana hawa anajibu, “Siyo sherehe, watu wanakuja wote kula nyama hapa.”
Tunakwenda moja kwa moja hadi mahali kunakouzwa. Wenyeji wetu hapa hawana wasiwasi, pengine kutokana na hawa vijana wawili wenyeji waliotufikisha hapa. Tunawakuta wateja wengi wakila nyama. Jiko limejengwa ndani ya nyumba mbovu ya miti na kuezekwa kwa nyasi.
Anayechoma nyama hapa ni maarufu kwa jina la Mangi. Baadaye tunamwuliza jina lake halisi na anajitambulisha kuwa anaitwa Mrosso Anthony. Kuna nyama ya nyati, swala na pofu. Pande linauzwa kuanzia Sh 10,000. Mimi nasita kuchukua nyama kubwa, naomba atutengee ya Sh 5,000. Wateja wote tuliokutana hapa ni kama vile tulishaonana siku nyingi, maana wengine wanakata “kilaji” (bia). Wanatukaribisha tunywe. Ni katika mazingira ambayo watembezi huyaita “adventure”.
Upande wa pili wa nyumba hii, kuna nyama mbichi iliyotundikwa. Inavutia kweli kweli. Inavuja damu mbichi kabisa. Kuna miguu na mikono. Pembeni mwa hiyo nyama, kuna kijana mmoja mwenye uso uliojaa makovu. Anaitwa Pengo. Sijui kwanini anaitwa Pengo, pengine ni kutokana na kutokuwa na meno mengi mdomoni. Namwuliza; “Pengo, vipi bwana, mbona uso umeharibika, wewe ni mgomvi au ulikuwa ukipambana na nyati?” Anajibu kwa tabasamu, “Siyo nyati mkuu, hii kitu ndiyo imefanya yote haya,” anasema huku akinionesha pikipiki.
Wageni wanazidi kumiminika hapa, na nyama zinauzwa kwa kasi. Ghafla, Pengo na Mangi wanaonekana kuhamaki baada ya kuwaona wateja wengine wawili wasiowajua wakija mahali tulipo. “Wale nani?” Anahoji Mangi. Pengo anajibu, “Ni wateja tu, siyo watu wabaya.”
Nyama tuliyoilipia ipo tayari. Tunaanza kula, lakini ni ngumu. Yaelekea ni ya upande wa shingo. Nimeshindwa kutelemka na kamera yangu kubwa. Hali hii inalilazimu nitumie kamera maalumu kupata picha za hapa na pale.
Ili nisiweze kushitukiwa, nauliza bei ya mguu wa pofu. Naambiwa kuwa bei yake ni Sh 120,000. Naomba niuziwe kipande cha Sh 20,000. Pengo anachukua mguu wa pofu. Anaupeleka nje kwenye gogo maalumu. Anakata. Kuona hivyo, walaji wenzetu nao wanaanza kununua. Wanakatiwa kadiri ya fedha zao. Wengine wanaingia wakiwa na bia zao kabisa. Nyama ni nyingi na hakuna mwenye wasiwasi.
Mwisho, nikiwa nimeshajiridhisha kuwa nyama inayouzwa ni ya pori, namwuliza Pengo wapi wanakopata nyama. “Hii nyama tunanunua kwa Waarabu wa Morogoro wanaokuja kuwinda huku.” Namwuliza, “Mbona muda wa kuwinda umekwisha?” Anakosa jibu.
Tumeshajiridhisha pasi na shaka kuwa hapa ni kwenye mnada wa wanyamapori. Tunaaga, lakini kabla ya kuondoka, Mangi anatupatia namba yake ya simu. “Chukua namba yangu ya simu, ukiwa unahitaji kabla ya kufika hapa wewe piga simu kabisa tukuandalie. Namba yangu ni 0655 093795. Karibu sana,” anasema.
Ingawa mwanzoni alinieleza kwamba jina lake ni Mrosso Anthony, usajili wa namba hii unaonesha kuwa ni ya Christian Joseph. Hii inazidi kunipa shaka.
Baada ya hapo naanza uchunguzi wa hapa na pale. Najiridhisha kuwa pikipiki iliyopo hapa ni moja ya zana zinazotumika kusafirisha nyama. Naelezwa na mmoja wa vijana kwamba pamoja na kuwapo kundi la vijana wanaoendesha ujangili, baadhi ya nyama wanazipata kutoka kwa askari wanyamapori wa Mikumi.
Wiki ijayo naendelea kueleza vituo vingine vya uuzaji wanyamapori. Ushiriki wa maofisa na askari wanyamapori katika biashara hii haramu. Je, Mkurugenzi na mwenye dhamana ya kupambana na ujangili nchini, Paul Sarakikya; Kamanda Masalu, Mkuu wa KDU (Kikosi Dhidi ya Ujangili), Majid Lalu; Mkuu wa Hifadhi ya Mikumi; Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Mvomero, Sarah Limuna; Ofisa Wanyamapori Mkoa wa Morogoro, Joseph Chuwa.
Nao, Askari Wanyamapori Wilaya ya Mvomero aliyepewa dhima ya kusimamia wanyamapori eneo la Doma, Peter Mayapila; Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Paschal Shelutete; wanasemaje? Je, kuwapo kwa huduma za mitandao ya simu hifadhini na katika mapori pamoja na kuruhusu matumizi ya bodaboda kunachangiaje wimbi la ujangili nchini? Usikose JAMHURI toleo lijalo.