Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia,Chalinze

Naibu Waziri wa Ardhi ,Nyumba na Maendeleo ya Makazi ,Ridhiwani Kikwete amewaasa wananchi kuheshimu taratibu na sheria kwakuwa ndiyo msingi utakaoleta amani katika jamii yetu.

Amezitaka Serikali za vijiji kuorodhesha majina ya wawekezaji ambao wamehodhi ardhi bila kuiendeleza ili irudishwe kwa ajili ya matumizi mengine.

Ameyasema hayo wakati alipofanya ziara ya siku moja katika kata ya Lugoba ambapo migogoro ya Uvamizi wa Ardhi za Vijiji inaonekana kushamiri.

Ridhiwani amesema ,maeneo mengi aliyopita ikiwemo Kijiji cha Makombe kumekuwa na malalamiko mengi toka kwa wananchi juu ya baadhi ya maeneo yaliyoombwa na wawekezaji hayajaendelezwa na kuwa mapori.

“Vijiji na Vitongoji orodhesheni majina ya wawekezaji wote walio katika maeneo yenu ambao hawajaendeleza ardhi waliyoiomba kufanya uwekezaji lakini wameiacha bila kuiendeleza kwani huo siyo utaratibu ni vema wakanyanganywa na kupewa watu wengine ili kuyatumia kuleta maendeleo,”alisema Ridhiwani.

Alisema kama kuna maeneo mnaona yametelekezwa na wawekezaji wasipate shida wanachotakiwa viongozi kupitia mikutano mikuu ni kutoa hoja na kuandikwa muhutasari kisha upelekwe Halmashauri na kupelekwa Wizarani ili kubadilishwa matumizi na kurudishwa Kijijini na kupangiwa shughuli nyingine.

“Tena kuna baadhi ya wawekezaji wanapokwenda kuomba maeneo wanatoa ahadi nyingi kuwa wakipewa watasaidia huduma za jamii au kutoa ajira kwa Vijana wa eneo husika lakini hawafanyi hivyo ni vema wakaachia ardhi waliyopewa,”alisema Ridhiwani.

Naye Diwani wa Lugoba Rehema Mwene amesema ,changamoto nyingine ni baadhi ya wawekezaji kuchukua maeneo na kutoyaendeleza hivyo kufanya kuwe na mapori makubwa ambayo yanahatarisha usalama wa watu.

Kaimu Mtendaji wa Kijiji cha Makombe Godfrey Nyange akisoma risala ya Kijiji alisema kuwa kuna migogoro ya mipaka baina ya Kijiji hicho na Vijiji vya Kinzagu na Mindutulieni.