Na Mwamvua Mwinyi,JamhuriMedia,Kibaha
Halmashauri nchini zimehimizwa ,kuvikopesha vikundi vya ujasiriamali vilivyoanzishwa na wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya maskini TASAF, kama ilivyo vikundi vingine ili walengwa wajikwamue kiuchumi.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Ridhiwani Kikwete ametoa rai hiyo wakati alipofika kitongoji Cha Mwembebaraza,kata ya Janga Kibaha Vijijini Mkoani Pwani, kujionea shughuli za wanufaika wa TASAF na mradi wa shamba darasa,kilimo Cha Mjini.
Ridhiwani amesema kwa hakika moja ya eneo ambalo limetekeleza mpango huo kwa vitendo na wanufaika kufaidika ni kata ya Janga, ambapo aliipongeza Tasaf na Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kibaha Ndalahwa Butamo kwa usimamizi mzuri.
Amemuelekeza Mkurugenzi huyo kuvipa vipaombele na vikundi vya ujasiriamali vilivyoanzishwa na wanufaika wa TASAF, kwenye mikopo ya asilimia 10 inayopelekwa kwa wanawake,vijana na walemavu.
“Kuvaa madela na kanga isiwe kigezo cha kuwanyima mkopo ya halmashauri, mafanikio ya mtu hayaangaliwi kwa umaridadi wake, wanawake hawa nao wanauhitaji wa mikopo hii.
“Nimesikia ni kikundi kimoja tu cha walengwa wa TASAF ndio kimekopesheka, msifanye hivyo.”ameeleza Ridhiwani.
Ridhiwani ameelezea, Rais Samia Suluhu Hassan anafanya kazi kubwa kuwapigania Watanzania kuondokana na hali mbaya ya maisha, ambapo ndani ya miaka miwili Bilioni 51 zimepelekwa kuwezesha wanufaika hao.
Vilevile amewataka watendaji wa TASAF kuendelea kutambua wenye uhitaji bila kuweka vikwazo.
Ridhiwani ameeleza kwamba, waratibu wa TASAF waendelee pia kupata elimu ya kutambua wanufaika.
Awali mratibu wa TASAF Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Sijaona Muhunzi alieleza kitongoji Cha Mwembebaraza ni miongoni mwa maeneo/Vijiji 46 vinavyotekeleza mpango wa kunusuru kaya maskini katika Halmashauri ya wilaya ya Kibaha mpaka kipindi cha malipo ya January -february 2023 kitongoji hicho kina Jumla ya kaya za walengwa 45.
Amesema kati ya kaya hizo kaya 44 sawa na asilimia 98 zinalipwa kupitia mtandao ikiwemo simu ama bank.
Muhunzi amefafanua, kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kitongoji kimepokea million 10,464,606 kwa ajili ya malipo ya walengwa ambapo kati ya fedha hizo 1,462,135 zinalipwa taslimu 9,002,471 zimelipwa kwa njia ya mtandao.
Amesema, katika kutekeleza mpango wa akiba na kukuza uchumi wa kaya unalenga kuwajengea uwezo walengwa wa mpango kuweka akiba ndogo ndogo.
Alibainisha hadi sasa kuna vikundi vinne vyenye wanachama 45 na wana akiba ya 465,000.
“Ukarabati wa jengo la wazee umefanyika ili kuinua kipato chao , upande wa elimu walengwa wa TASAF kuonyesha mafanikio makubwa katika kuanzisha miradi na kusomesha watoto wao hadi chuo”hii ni hatua chanya inayoonyesha matokeo mazuri ya mradi”ameeleza Muhunzi.
Ridhiwani Kikwete yupo mkoani Pwani kwa ziara ya siku tano kuzungumza na watumishi wa Umma pamoja na kujionea utekelezaji wa mradi wa TASAF ,kwa kupata taarifa, na kutoa maelekezo.