Na Lusungu Helela, JamhuriMedia,Chalinze

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,Ridhiwani Kikwete amesema taaluma ya Uuguzi ni kazi ya uthubutu, utayari pamoja na kujitoa kwa ajili ya kuwahudumia wenye mahitaji ya kiafya huku akiwataka Wauguzi kuendelea kuchapa kazi kwa weledi na kwa kuzingatia miiko na maadili ya taaluma yao.

Kikwete aliyasema hayo juzi wakati akizungumza na Wauguzi wa Mkoa wa Pwani kwenye Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani yaliyofanyika kimkoa katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze ambapo amewahimiza Wauguzi hao kuwahudumia wananchi kwa moyo na upendo wa hali ya juu.

Naibu Waziri,  Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akikabidhi zawadi kwa Mariam Moyo aliyejifungua katika Wodi ya Wazazi iliyopo katika Hospitali ya Chalinze mkoani Pwani ikiwa ni shamrashamara ya Maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani iliyofanyika kimkoa katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze Mkoani humo
 

Alisema, Serikali inatambua kuwa Wauguzi ni kundi muhimu sana kwani ndio shina na mhimili mkubwa wa utendaji na ufanisi wa sekta ya afya nchini na ulimwenguni kote.

Kikwete ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka mazingira mazuri ya kufanyia kazi Wauguzi hao ikiwa ni pamoja na kuweka mikakati mbalimbali ili kuyafikia malengo endelevu ya afya kwa wote.

Aidha,Kikwete alisema Ofisi ya Rais-UTUMISHI inaendelea kuzifanyia kazi changamoto za kimuundo za taaluma hiyo na changamoto nyingine itaishirikisha Wizara husika ya Afya ili ziweze kufanyiwa kazi.

Katika hatua nyingine,Kikwete amekubali ombi la kuwa mlezi wa Wauguzi katika Mkoa wa Pwani huku akiahidi kuwapa ushirikiano ili kuwaongezea morali Watumishi hao katika kutekeleza majukumu yao.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete   akizungumza na Wauguzi wa Mkoa wa Pwani kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani yaliyofanyika kimkoa katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze Mkoani humo ambapo amewahimiza Wauguzi hao  kuwahudumia wananchi na jamii yote ya Kitanzania kwa moyo na upendo wa hali ya juu

‘’Natambua mchango wenu adhimu kwa mustakabali wa afya zetu kwani ziko mikononi mwenu, napenda kuwaahidi mimi kama mlezi wenu niko tayari kuwapa ushirikiano muda wote mtakaponihitaji” amesisitiza Mhe, Kikwete.

Awali Katibu wa Chama cha Wauguzi Mkoa wa Pwani, Bi, Dafroza Mnzava akisoma risala kwa Naibu Waziri Mhe. Kikwete, ameiomba Serikali kuzifanyia kazi changamoto zinazowakabili ikiwemo suala la muundo na posho ya mazingira hatarishi na stahiki mbalimbali.

Pia Katibu huyo ameiomba Serikali kuendelea kuajiri wauguzi ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Maadhimisho hayo yenye kauli mbiu “WAUGUZI WETU, MUSTAKABALI WA AFYA ZETU” yamefanyika mkoani humo ikiwa ni kuenzi kumbukumbu ya Muasisi wa Uuguzi na Ukunga Duniani, Bi. Florence Nightingale wa nchini Italia, aliyejitoa kwa moyo kuwahudumua wenye mahitaji ya kiafya.

Mganga Mkuu wa mkoa wa Pwani, Dkt. Gunini Kamba  akizungumza na Wauguzi wa Mkoa wa Pwani kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani iliyofanyika kimkoa katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze Mkoani humo