Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete amezitembelea familia na makazi yenye migogoro ya ardhi ya muda mrefu kwa kuzifuata katika maeneo yao kwa lengo la kujionea uhalisia wa migogoro na kupata maelezo ya kina kabla ya kizitafutia ufumbuzi.
Naibu Waziri Kikwete amefanya hayo mkoani Morogoro jana tarehe 18 Agosti 2022 ambapo ametembelea baadhi ya maeneo na familia zenye migogoro ya muda mrefu ambapo miongoni mwazo ametembelea familia ya Bwana Felician Bupiripiri na Bwana Rajabu Kyara ambao wamekuwa wakigombea kiwanja namba 1 na namba 3 vilivyopo mtaa wa Boma Road katikati ya mji wa Morogoro.
Katika hali isiyo ya kawaida Naibu Waziri Kikwete alifika katika nyumba hiyo na kumkuta Bibi Neli Lukwaja ambaye ni mke wa Bwana Felician Bupiripiri na kutembeza maeneo yote ya nyumba hiyo ambayo wamekuwa wakiimiliki kwa muda mrefu huku akilalamika kutotendewa haki na Rajabu Kyara ambaye nae anadai kumilikishwa kwa hati.
Mara baada ya kutembelea makazi hayo Naibu Waziri kikwete alielekeza kuitwa kwa familia zote mbili ili kuwasikiliza kwa kina na kutafutia ufumbuzi wa mgogoro wao katika kikao chake alichokifanya katika Chuo cha Ardhi cha Morogoro (ARIMO).
Katika kikao hicho Naibu Waziri Kikwete alishirikisha Maafisa kutoka Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi Morogoro na Maafisa wa sekya ya ardhi kutoka Ofisi ya Manispaa ya Morogoro ili kupata melezo ya kina ya chnazo na sababu za mgogoro husika.
Hata hivyo, baada ya kusikiliza kwa kina mgogoro huo Naibu waziri kikwete ameelekeza kuja mara moja kwa Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani kutoka Wizarani Bwana Hamduni Mansouri ili aje kupitia upya ramani na mipaka ya viwanja hivyo vyenye mgogoro.