Baada ya mchezo wa riadha kufanya vibaya kwa muda mrefu na kuanza kupoteza msisimko miongoni mwa Watanzania, sasa unaonekana kurudisha msisimko baada ya mafanikio kutoka kwa mwanariadha Felix Simbu.

Ushindi wa Simbu katika mashindano ya mbio za Standard Chartered Mumbai Maradhon huko India, umeonekana kuwa tumaini jipya katika mchezo huo.

Kijana huyo alimaliza mbio hizo kwa muda wa 2:09:32 na kuzawadiwa dola za Kimarekani 42,000 na kufuatiwa na Mkenya Joshua Kipkorir aliyemaliza katika nafasi ya pili kwa muda wa 2:09:50, akifuatiwa na  Mkenya mwenzake Eliud Barngetuny aliyeshika nafasi ya tatu kwa muda wa 2:10:39.

ushindi huo wa Simbu umeweza kuzishawishi baadhi ya kampuni kufikiria kumdhamini. Moja ya kampuni hizo ni MultiChoice-Tanzania, ambayo imekubali kumdhamini  mwanariadha huyo katika kipindi cha mwaka mmoja, kwa ajili ya maandalizi yake ya mashindano ya dunia yatakayofanyika mwaka kesho.

Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) nayo imeonesha nia ya kutaka kukaa pamoja na wadau wa riadha ili kujadili namna ya kusaidia kuuinua mchezo huo hapa nchini.

Akizunguza na JAMHURI, mwanariadha huyo anasema mchezo wa riadha umekuwa ukikabiliwa na changamoto nyingi ambazo zimechangia kwa kiasi kikubwa wengi wao kushindwa kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali.

“Kukosekana kwa wafadhili wenye uwezo wa kuwadhamini wachezaji wanapokuwa kambini na hata wanapohitaji kusafiri, ni miongoni mwa changamoto za miaka mingi inayoukabili mchezo wa riadha hapa nchini,” amesema Simbu.

Amesema mifano mingi ya mafanikio katika riadha, utawasikia wadau wakiwataja watu kama Juma Ikangaa, Filbert Bayi, Suleiman Nyambui na wengine wengi huku wakisahau kuwa nguli hao walikuwa wakipata maandalizi ya hali ya juu kabla ya kwenda mashindanoni.

Simbu amesema changamoto nyingine inayoukabili mchezo huo ni kutopewa nafasi kubwa shuleni, huku akisisitiza mchezo huo umekuwa na mwamko mdogo kuanzia ngazi za chini hadi juu na pia ukosefu wa viwanja vyenye ubora unaotakiwa.

Simbu aliyezaliwa tarehe 14, Februali 1992 ni mwanariadha wa mbio ndefu, na kwa upande wa Marathon ni miongoni mwa wanariadha wa Kitanzania aliyeshiriki katika Marathon ya mwaka 2015 Beijing nchini China.

Kijana huyo alikuwa miongoni mwa wawakilishi wa Tanzania katika mashindano ya Olympics 2016, iliyofanyika Rio de Janeiro, nchini Brazil. 

Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Mohamed Kiganja, anasema Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) ndiyo chama pekee cha michezo nchini kinachoongozwa na Mkuu wa Mkoa, kwetu sisi (BMT) ni utajiri, hii ni dalili nzuri.

“Migogoro kwenye vyama inakimbiza wawekezaji na wafadhili, siyo vema pindi mambo ya ndani yanapokuwa hayaendi sawasawa kukimbilia kwenye vyombo vya habari,” amesema Kiganja.

Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Anthony Mtaka, amesema lengo la viongozi wa mchezo huo ni kuona wanariadha wanafanikiwa na kuwa na maendeleo ya kiuchumi na pia kulitangaza vyema jina la nchi kimataifa.

Mtaka amesema kutambua kwamba kuna udhaifu katika mchezo wa riadha, RT tayari tumekuja na mbinu na mikakati ya namna ya kujikwamua.

“Lengo letu ni kutaka kuona mchezo huu unachezwa kuanzia ngazi ya awali hadi Taifa pamoja na changamoto kubwa ya ukosefu wa viwanja baada ya vilivyokuwapo kuporwa na watu wenye fedha na kujenga majumba,” amesema Mtaka.

Mtaka amesema tayari wameanza kufanya mchujo wa awali katika mikoa yote, lengo likiwa ni kupata wachezaji chipukizi wenye vipaji watakaokuwa na uwezo wa kuwa wawakilishi wa Taifa kwa muda mrefu.

“Kwenye michuano ya Olympic ya Beijing na London hatukuwa tumezinduka, sasa michuano ya Olympic iliyofayika Rio de Janeiro, Brazil imedhihirisha kwamba tunahitaji mipango na mikakati ya kuwapata wachezaji wenye sifa,” amesema Mtaka.

Kiongozi huyo wa RT ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, amesema kufanya vizuri kwa Simbu katika miaka ya hivi karibuni ni chachu kwa wanariadha wengine chipukizi kufuata nyayo zake.

“Mwaka 1980 kwenye mashindano ya Olympic jijini Moscow nchini Urusi, Bayi na Nyambui walitutoa kimasomaso ambapo kati ya wanariadha 41 walioliwakilisha Taifa, ni wao wawili tu waliopata medali,” amesema Mtaka.

Anasema katika mashindano hayo, Nyambui alitwaa medali ya fedha baada ya kushika nafasi ya pili kwenye mbio za mita 5,000 huku Bayi pia akishinda medali ya fedha baada ya kushika nafasi ya pili kwenye mbio za mita 3,000 kuruka maji na viunzi.

Anasema hii ndiyo iliyokuwa mara ya kwanza na ya mwisho kwa Tanzania kutwaa medali katika mashindano ya Olimpiki hadi leo, ingawa tumekuwa tukishiriki bila mafanikio.