SERENGETI
Na Mwandishi Wetu
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja, amesema michezo ina nafasi kubwa ya kuimarisha uhusiano na ujirani mwema miongoni mwa wadau wa utalii nchini.
Akizungumza baada ya kushiriki mbio maalumu za Serengeti Safari Marathon wiki iliyopita, Mary anasema mbali na kuimarisha uhusiano na ujirani mwema, pia mbio hizo zitasaidia katika kutangaza utalii maeneo ya Kanda ya Ziwa.
“Ninapenda kutumia nafasi hii kuwaomba wadau kutumia michezo kama mbio hizi kujenga na kuimarisha uhusiano kati yao na Hifadhi za Taifa (TANAPA).
“Si wananchi wa eneo hili (Kanda ya Ziwa) pekee, bali katika maeneo yote ambako hifadhi za taifa hupatikana na kupakana na jamii,” anasema Naibu Waziri Mary Masanja.
Mbio hizo maalumu zimefanyika ndani ya Hifadhi ya Serengeti na kujumuisha wanariadha kutoka maeneo mbalimbali duniani.
Naibu Waziri amewamwagia sifa waandaaji wa mbio hizo akisema: “Mbio hizi ambazo mimi mwenyewe nimeshiriki, zimeandaliwa vema huku zikiambatana na matukio mbalimbali yenye faida kwa jamii.”
Miongoni mwa matukio yaliyoambatanishwa na Serengeti Safari Marathon ni kukutanisha jamii za wavuvi, wafugaji, wafanyabiashara na wananchi wengine wa Kanda ya Ziwa na wadau wa uhifadhi wakiongozwa na TANAPA na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).
Mary amewataka waandaaji kusambaza mpango huo katika hifadhi nyingine nchini ili kukuza utalii huku pia wakiimarisha afya ya wadau, wakitoa elimu ya uhifadhi kwa kuieleza jamii faida ya kuwapo kwa hifadhi za taifa na kujumuisha jamii.
Mmoja wa waandaaji, Timothy Mdinka, anawashukuru UNDP na TANAPA kwa kukubali kushiriki, hivyo kufanikisha tukio analoliita muhimu na la kihistoria.
“Unaweza ukadhani ni mbio tu zinazochukua saa kadhaa kwa siku, lakini ukweli ni kwamba mbio zenyewe zilikuwa ni kilele cha matukio mbalimbali yaliyodumu kwa wiki nzima,” anasema Mdinka.
Matukio hayo yalianza Novemba 8, 2021 kwa kufanyika mashindano ya mbio za baiskeli kwa wanaume na wanawake.
Washindi 10 wa kwanza wa mbio za baiskeli watapatiwa mafunzo ya uongozaji watalii kama moja ya njia ya kuwapatia ajira.
“Tukio la siku iliyofuata ilikuwa ni kupanda Mlima Balili uliopo Bunda. Miongoni mwa washiriki walikuwa ni wanafunzi wa utalii kutoka vyuo vilivyopo Kanda ya Ziwa,” anasema.
Matukio mengine yalikuwa ni kikao kati ya mameneja wa hoteli zilizopo katika Hifadhi ya Serengeti, Umoja wa Wakulima wa Mboga (TAHA), Benki ya NMB, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) na TANAPA.
Kikao hicho kiliwashirikisha pia wakulima na wafugaji katika kujadili jinsi watakavyofanya biashara kwenye hoteli hizo na kunufaika kuliko ilivyo sasa.
“Hali ilivyo kwa sasa bidhaa zote katika hoteli ndani ya hifadhi hutoka Kanda ya Kaskazini, ilhali zinapatikana Kanda ya Ziwa,” anasema.
Ni ndani ya wiki hiyo hiyo UNDP wakatembelea miradi wanayoifadhili katika wilaya zinazozunguka Hifadhi ya Serengeti, kikiwamo kituo cha masista kilichopo Kibara, ambako wamewapa mashine ya kutengeneza jibini (cheese).
Mwandaaji mwingine wa Serengeti Safari Marathon, Henry Kimambo, anasema Novemba 13, 2021 ndiyo ilikuwa kilele cha mbio hizo.
“Tumepata mafanikio makubwa kwa kuwa zaidi ya washiriki 800, wakiwa na ari kubwa, walijitokeza. Usajiri uliendelea hadi siku ya mwisho, kwa kuwa watu walikuwa wakiendelea kuomba kujiorodhesha!” anasema Kimambo.
Anasema maandalizi mazuri ikiwa ni pamoja na kuwatumia wataalamu waliobobea yamesababisha kukamilika kwa tukio zima bila kuwapo tatizo lolote, wala majeraha.
Anasema tukio hili la kila mwaka limekuwa kivutio kwa wanamichezo wengi na moja ya njia sahihi za kutangaza utalii wa Tanzania.
Mbio hizo zilishirikisha wakimbiaji wa mbio fupi na ndefu; yaani kilometa tano, 10, 21 na 42 huku mashindano ya baiskeli yakienda hadi kilometa 80.