Mradi wa reli mpya ya kisasa nchini Kenya SGR umesababisha
hasara ya $100m (£76m) katika kipindi cha mwaka wa kwanza wa
operesheni zake , kulingana na wizara ya uchukuzi nchini humo.
Mradi huo uliofadhiliwa na serikali ya China ambao unaunganisha
mji wa pwani wa Mombasa na Nairobi ulifadhiliwa kwa mkopo wa
kima cha $3bn kutoka kwa benki ya China ya Exim katika kipindi
cha miaka 15.
Serikali ya Kenya ilipinga madai kwamba bei ya ujenzi wa mradi huo
wa reli iliongezwa, haiwezi kudumishwa na haifai kiuchumi.
Reli hiyo ya SGR ni miongoni mwa miradi muhimu ilioahidiwa na
rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi wake, ukizinduliwa mwezi
mmoja kabla ya uchaguzi wa urais uliopita.
Huku treni za abiria zikijaa mara kwa mara, waziri wa uchukuzi
James Macharia aliambia kamati ya bunge kwamba ilikuwa vigumu
kuwarai wenye mizigo kusafirisha mizigo hiyo kupitia reli kutoka
kwa barabara.
Mipango ya kuanza kulipa deni hilo inatarajiwa kuanza mwaka ujao,
na iwapo reli hiyo itashindwa kujilipia deni hilo basi huenda walipa
kodi wa Kenya wakalazimika kulipa deni hilo.
Wanauchumi wanakadiria kwamba China sasa inamiliki asilimia 70
ya deni la Kenya.
Hatahivyo serikali inatumai kwamba reli hiyo itaanza kupata faida
katika kipindi kijacho cha fedha.