Eleuteri Mangi, WUSM, Zanzibar
Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdullah amewataka Wahariri kushirikiana na mabaraza ya Kiswahili ya BAKITA na BAKIZA ili kuendeleza lugha ya Kiswahili.
Amesema kuwa lugha ya Kiswahili imevuka mipaka na sasa kuna redio na runinga 38 duniani zinazorusha matangazo yao kwa kutumia lugha ya Kiswahili ndiyo maana kaulimbiu ya maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani inahimiza kuwa “Kiswahili Chetu; Umoja Wetu”.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwinjuma amesema lugha ya Kiswahili ipewe hadhi na ukubwa wake na mahali bora zaidi kuanzia ni Jukwaa la wahariri ambao wanafanyakazi ya kutoa mwelekeo wa lugha na mambo mbalimbali kwa kusoma, kutazama na kusikiliza.
Naibu Waziri Mwinjuma amesema hayo Julai 4, 2023 Mjini Zanzibar wakati wa mkutano na Jukwaa la Wahariri kuelekea Siku ya Kiswahili Duniani mada ikiwa ni “Nafasi ya Wahariri Wakuu katika kusimamia matumizi ya Kiswahili sanifu katika vyombo vya Habari”.
“Hamu yangu ni kukaa kwenye mkutano huu kuanzia mwanzo hadi mwisho bila kusikia neno la lugha nyingine zaidi ya lugha sanifu na sahihi ya Kiswahili” amesema Naibu Waziri Mwinjuma.
Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili yam waka 2023 ni ya pili bbada ya kuadhimishwa kwa mara ya kwanza mwaka 2022 ambayo ni siku maalum ya kuadhimishwa lugha hiyo baada ya kutangazwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) Novemba 23, 2021.