Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Mbinga
NAIBU Waziri wa Nishati Judith Kapinga amezindua na kuwasha umeme katika Kijiji cha Litumbandyosi kilichopo Kata ya Litumbandyosi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga vijijini mkoani Ruvuma huduma ambayo haijawahi kupatikana tangu nchi ipate uhuru.
Umeme huo ambao umewashwa rasmi jana majira ya saa 6 mchana na kushuhudiwa na wananchi kutoka katika vijiji vinne vya kata hiyo ambavyo ni Kingole, Mabuni, Luhagara na Litumbandyosi umetokana na mtambo wa kuzalishia umeme toka Wakala wa Umeme Vijijini (REA) .
Naibu Waziri wa Nishati Kapinga akizungumza na wananchi hao kwenye uzinduzi huo amesema kuwa umeme huo kwa awamu ya kwanza utawashwa kilometa moja na awamu ya pili utawashwa kilometa mbili na tayari Serikali imeshatoa fedha kwa miradi yote miwili.
Amesema kuwa huduma za nishati za umeme vijijini (REA) ni muhimu kwa sababu wananchi wamekuwa wakijishughulisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo kuanzisha viwanda vidogo vidogo kwa lengo la kujiletea maendeleo na si vinginevyo.
Naibu Waziri Kapinga amesema kuwa umeme huo utaweza kuzalisha umeme ambao utakidhi mahitaji ya wananchi wa vijiji vya Kata hiyo ya Litumbandyosi na vitongoji vyake na kuwafanya waondokane na adha ya kukosa huduma hiyo nyeti kwa miaka mingi.
” Ndugu zangu wa vijiji vilivyobakia niwahakikishie nyote mtapata umeme kwa sababu rais wetu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amekwisha toa fedha kwa vijiji vyote vilivyobakia hakupepesa macho alisema anataka kumaliza vijiji vyote changamoto ya umeme na fedha imeshatoka” amesema Kapinga.
Wakati huo huo, Naibu Waziri wa Nishati Kapinga amesikitishwa na lasi ndogo ya mkandarasi Namis Corporate Limited Shaidu Rutakolezibwa kutokana na kuchelewesha kukamilishwa kwa miradi hiyo ya REA kwa wakati jambo ambalo linachelewesha maendeleo kwa wananchi ambao wengi wao ni maskini.
Amesema kuwa mkandarasi akimaliza kazi zake analipwa kwa nini umeme usiende kwa kadri alivyotakiwa kupeleka hatakubaliana na uzembe wa aina yoyote na kwamba hadi kufikia Otoba 30 mwezi huu vijiji vyote vya awamu ya kwanza viwe vimeshawashwa umeme.
Kwa upande wao wanakijiji hao wameishukuru Serikali kwa kuwaletea mradi wa huo wa umeme ambao utaleta tija kubwa kwa wananchi ambao wapo mbali na mjini na utawawezesha kuchakata bidhaa zao hapo hapo kijijini badala ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za umeme.
Aidha wameiomba Serikali kuharakisha kusambaza umeme huo kwa wananchi na taasisi za serikali ikiwemo Zahanati ,Kituo cha afya, shule na ofisi za chama na Serikali ili uweze kuleta tija na si vinginevyo.