Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Zanzibar
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy amesema Wakala utaendelea kufanya tafiti za bidhaa za Nishati Safi za Kupikia ili kubaini ufanisi wa teknolojia zinazosambazwa kwa wananchi.
Mhandisi Saidy amesema hayo Agosti 23, 2024 alipotembelea Banda la Wakala katika Tamasha la Kizimkazi eneo la Kizimkazi Dimbani Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.
“Tutaendelea kufanya utafiti wa bidhaa mbalimbali za Nishati Safi za Kupikia ili kutimiza dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha Nishati Safi ya Kupikia kwa wote inapatikana kwa gharama nafuu na yenye ufanisi,” amesema.
Amesema dhamira ni kuwa na teknolojia sahihi, rafiki na yenye gharama nafuu ili kumuwezesha na kumrahisishia kila Mwananchi kuwa na bidhaa bora.
“Tutahakikisha lengo la Serikali kupitia Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024-2034 la kufikisha asilimia 80 ya wananchi wanaotumia Nishati Safi ya Kupikia ifikapo 2034 linafikiwa,” amesema.
Mhandisi Saidy vilevile alitembelea mabanda ya Wadau wanaojihusisha na uandaaji, uuzaji na usambazaji wa Nishati Safi ya Kupikia na kujadiliana masuala mbalimbali hususan namna bora ya kuendelea kuboresha bidhaa zao ili kuleta tija inayokusudiwa.
Awali kabla ya kutembelea Maonesho ya Kizimkazi, Mhandisi Saidy alishiriki Kongamano la Nishati Safi ya Kupikia lililoandaliwa na Taasisi ya Mwanamke Initiatives Foundation (MIF) na Benki ya Uwekezaji ya Tanzania (TIB) kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati na Taasisi zake ikiwemo REA ambapo Wakala ulipata fursa ya kuelezea suala la Upatikanaji wa Fedha katika kuendeleza Nishati Safi ya Kupikia.