Familia ya marehemu James Massawe, aliyeuawa kikatili Juni 9, 2009 katika Kijiji cha Kindi Kibosho, Wilaya ya Moshi Vijijini baada ya kutekwa, imemwandikia barua Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) ikihoji kutokamatwa kwa wafanyabiashara watatu ndugu ambao walihusika na utesaji huo.
Familia inapinga kuachiliwa huru washitakiwa wawili wa mauaji hayo na wameitaka Ofisi ya DPP iingilie kati na kuamuru washitakiwa hao wakamatwe na kufikishwa mahakamani kwa mara ya pili kujibu mashitaka ya mauaji ya ndugu yao.


Massawe, ambaye alikuwa Meneja wa baa maarufu ya Mo-Town ya mjini Moshi, anadaiwa kutekwa katikati ya mji wa Moshi na wafanyabiashara ndugu wanaomiliki vitegauchumi kadhaa katika Jiji la Mwanza, na kupelekwa katika moja ya nyumba za wafanyabiashara hao eneo la Kibosho ambako inadaiwa alipewa mateso hadi kufa.
 Baada ya mauaji hayo, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Lucas Ng’hoboko, aliueleza umma kuwa Massawe aliuawa na wananchi, lakini baada ya kelele nyingi kupigwa na familia, hatimaye aliyataja majina matatu ya wafanyabiashara wanaotuhumiwa kuhusishwa na mauaji hayo.


  Wafanyabiashara hao ambao baada ya mauaji hayo walikwenda mafichoni nje ya nchi, walitajwa na Kamanda Ng’hoboko kuwa ni John Joseph Kisoka (Magazeti) na wadogo zake Musa Joseph Kisoka na Deo Joseph Kisoka.
Hata hivyo, pamoja na wafanyabiashara hao kutajwa na kamanda huyo na kutangaza kuwasaka, Jeshi la Polisi liliishia kuwakamata vijana wawili – Idrisa Hassan Munishi na John Mallya (Small Boy) – na kufikishwa mahakamani ambako walishitakiwa kwa mauaji ya Massawe.
 Vijana hao walifikishwa mbele ya Jaji Mfawidhi wa Makahama Kuu Kanda ya Moshi, Stella Mugasha, katika shauri la jinai namba PI 9/2009, lakini Wakili wa Serikali, Theophil Mutakyawe, aliliondoa shauri hilo mahakamani.


Kiini cha kutekwa kwa kijana huyo kinatokana na madai  ya wafanyabiashara hao kwamba Massawe alihusika na mauaji ya mama mzazi wa wafanyabiashara hao, Martha Kisoka (68), aliyeuawa na watu wasiojulikana Mei 2009 baada ya kuvamiwa nyumbnai kwake Kindi, Kibosho.
Mwaka 2007 Massawe na wenzake wanne walihukumiwa kifungo cha miaka 14 jela baada ya kupatikana na hatia ya kuvunja na kuiba nyumbani kwa ajuza huyo, lakini mwaka 2008 waliachiwa huru baada ya kukata rufaa kupinga adhabu hiyo.


Katika barua yao ya Oktoba 7 mwaka jana kwenda kwa DPP, familia hiyo inalalamika kutokamatwa kwa watu muhimu kwenye mauaji ya Massawe lakini pia wakihoji kigezo kilichotumika kuwaachia huru baadhi ya watuhumiwa wa mauaji hayo.
Barua hiyo ya familia iliyotiwa saini na Beda Massawe kama msemaji wa familia, na Peter Lelo Massawe inadai kuwa kifo cha ndugu yao kilikuwa cha kinyama kwani alitekwa na kupelekwa umbali wa kilometa 15 ambako aliteswa kwa kupigwa huku akiwa amening’inizwa kichwa chini miguu juu na kuingizwa chupa ya bia katika sehemu ya haja kubwa.


Baada ya barua hiyo kumfikia DPP, ilipelekwa moja kwa moja kwa Ofisi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) ambako ofisi hiyo ilimwandikia barua Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) ikimtaka afuatilie malalamiko hayo haraka ili abaini ukweli.
“Inspekta Jenerali wa Polisi anakuagiza ufanye ufuatiliaji wa haraka kuhusiana na lalamiko hilo ili kubaini ukweli iwapo kuna ukiukwaji wa maadili wakati wa kushughulikia lalamiko hilo na umjulishe matokeo kabla ya Oktoba 30,” inasema sehemu ya barua hiyo ya Oktoba 9, mwaka jana.


Barua hiyo iliyosainiwa na S.M. Ambika ambaye ni Kamishna Mwandamizi Msaidizi wa Polisi (SACPA) nakala yake ilipelekwa kwa Beda Massawe wa Kijiji cha Kindi, Kibosho ikimtaarifu kufika ofisi ya DCI kwa ajili ya kupata kile kilichoelezwa kwenye barua hiyo kuwa ni ufumbuzi wa suala lake.
Akizungumza na JAMHURI, Beda amesema kuwa licha ya kwenda mara kwa mara ofisi ya RCO Mkoa wa Kilimanjaro, wamekuwa wakipewa matumaini hewa kwamba suala lao linashughulikiwa, lakini wanachoambulia ni kuwaona watuhumiwa wakitamba mitaani na kuwatolea lugha za kejeli.
Amesema kuwa hivi sasa wameanza kukosa imani juu ya maendeleo ya kesi ya mpendwa wao na kuiomba ofisi hiyo ya DCI kuwapa msaada zaidi baada ya ofisi ya RCO Kilimanjaro kutowapa ushirikiano.


Kutokana na danadana hizo wanazozipata kutoka ofisi ya RCO Kilimanjaro ambayo imekuwa ikilalamikiwa na wananchi wengi, familia hiyo imemwandikia tena barua DCI ikimuomba asikilize kilio chao juu ya malalamiko hayo.
“Kwa barua hii, tunakuomba upitie kumbukumbu ya malalamiko yetu na kutuambia hatua iliyofikia au inayotakiwa kufuata ili walau haki ionekane ikitendeka juu ya malalamiko ya ndugu yatu,” inasema sehemu barua ya familia hiyo ya Machi 10, mwaka huu.
Beda anahoji iweje iwe rahisi kwa polisi kuwakamata waandamanaji na kuwafikisha mahakamani, lakini iwe vigumu kwa polisi kuwakamata watuhumiwa wa mauaji.


Juhuzi za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Geofrey Kamwela, ili kuzungumzia hatima ya shauri hili zinaendelea. Wiki iliyopita hakupatikana kutokana na kubanwa kwake na sherehe za ufungaji wa kozi za Maofisa Wakaguzi Wasaidizi wa Polisi zilizofanyika Moshi.