Wanaharakati wa mazingira mkoani Kilimanjaro wamemtaka Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makalla (pichani), kufuta maagizo yake ya kuzitaka halmashauri za wilaya kuvuna magogo katika misitu ya asili kwa ajili ya kutengeneza madawati.
Makalla akiwa wilayani Same hivi karibuni, alitoa maagizo hayo baada ya kupokea taarifa ya uhaba wa madawati katika baadhi ya shule za msingi. Maagizo hayo yamezua mjadala mkali.
Baada ya maagizo hayo kuripotiwa kwenye vyombo vya habari, mjadala uliibuka kwenye mtandao wa WhatsApp kupitia kundi la Mada Moto linalowajumuisha watu wa kada zote.
Baadhi ya waliochangia wanamtaka Makalla arejee katazo la kutokata miti lililotolewa na mtangulizi wake, Leonidas Gama, kupitia kikao cha Kamati ya Ushauri cha Mkoa. Sasa Gama ni Mbunge wa Songea Mjini (CCM).
Wadau wanasema kwa miaka minne ambayo Gama aliongoza Kilimanjaro, kumekuwa na mabadiliko makubwa kwenye uhifadhi wa mazingira; hali iliyorejesha uoto wa asili katika Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA).
Baadhi ya wachangiaji wametishia kufanya maandamano ya amani hadi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kupinga agizo hilo.
Kutokana na mjadala huo kuwa mkali na ulioonekana kuchafua hali ya hewa, Mkuu wa Kundi hilo (Admin), Daniel Mjema, alilazimika kumuunganisha Makalla ili ajibu “mashambulizi”.
Kauli ya Makalla
“Nawashukuru wadau kwa michango yenu mizuri juu ya utunzaji wa mazingira. Wapo waliochangia kwa busara na hekima na uzalendo wa hali ya juu na wapo walioipokea hoja kwa mapokeo hasi na kuhitimisha kwa utashi wa kiitikadi, nao nimewaelewa,” amesema.
Anajitetea kwa kusema hajafuta azimio la kikao cha Kamati ya Ushauri Mkoa wa Kilimanjaro; na kuongeza kuwa utunzaji wa miti na mazingira ni ajenda endelevu na imekuwa na manufaa makubwa katika Mkoa wa Kilimanjaro.
Anasema hajaruhusu watu wakate miti ovyo; na kwamba agizo lake limepotoshwa makusudi ili watu wahamasike kukata miti makusudi kwa kisingizio cha madawati.
Akitumia mtandao huo wa WhatsApp, Makallla anasema alichoelekeza kwa halmashauri hizo ni kuzitaka zijitosheleze kwa madawati. Halmashauri hizo ni Same, Mwanga na Siha.
Anasema agizo la Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na waraka wake ni kuwa ifikapo Juni 2016 kila halmashauri iwe inajitosheleza kwa madawati.
Anasema agizo hilo alilitoa kwa kuhoji ni kwanini wanashindwa kupata vibali maalumu vya madawati licha ya misitu kuwapo.
Anasema amezitaka halmashauri za wilaya katika mkoa wake kutenga fedha zinazotokana na mapato ya ndani kwa ajili ya madawati; na halmashauri zenye fursa ya misitu kwa idhini ya wataalamu wa misitu wakijiridhisha watoe vibali maalumu kadri watakavyoona inafaa.
“Naomba nieleweke; jambo hili limepotoshwa kwa makusudi, lakini nimejifunza mengi kuhusu hoja hii nikagundua tulio wengi tunapenda nchi yetu, utunzaji wa mazingira… nawahakikishia hapa kazi tu, tutailinda misitu,” amesema Makalla.
Katika hatua nyingine, waandishi wa habari watatu wanaodaiwa kuripoti habari hizo wamejikuta katika wakati mgumu baada ya Makalla kuwekwa ‘kiti moto’ akidai walimnukuu vibaya.
Waandishi waliokumbana na kadhia hiyo ni Kija Elias (Zanzibar Leo), Paul William (Jambo Leo) na Safina Sarwatt anayeandikia Gazeti la Mtanzania.
Waandishi hao wamekiri kuitwa kwa nyakati tofauti ofisini kwa Mkuu wa Mkoa na kuambiwa kuwa kiongozi huyo hakufurahishwa na namna walivyoripoti habari za madawati.
Mwanaharakati wa mazingira wa kikundi cha Roots and Shoots, Dominic Osoki, ametoa mwito kwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na wakurugenzi wa halmashauri za wilaya kuchukua hatua kwa watu waliojenga kwenye vyanzo vya maji.
Katika taartifa yake kwa vyombo vya habari, amesema baadhi ya watu wanaendesha shughuli za kilimo kando ya mito na kwenye vyanzo vyanzo vya maji huku watendaji wa vijiji na vitongoji wakishuhudia.
“Ni lini nyie viongozi wa wilaya na mkoa mtaanza kuwatoa wanaojenga nyumba mabondeni chini ya meta 60 na kilimo kwenye vyanzo vya maji?” Amehoji.
Inakisiwa kuwa wastani wa hekta 400,000 za miti ya asili zinateketezwa nchini kote kila mwaka kutokana na matumizi ya mkaa, kuni na mbao.
Hali hiyo inaifanya Tanzania kunyemelewa na jangwa endapo hatua za haraka hazitachukuliwa kukabiliana na uharibifu huo wa mazingira.