Na Mwandishi wetu, Ruangwa
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Tellak amesema eneo hilo lina fursa nyingi za uwekezaji na utajiri mkubwa wa madini mbalimbali isipokuwa madini ya Tanzanite na Almas pekee.
Tellak akizungumza mjini Ruangwa kwenye ufunguzi wa maonyesho ya madini na fursa za uwekezaji amesema dhana ya kuwa Lindi ni mkoa masikini ni potofu kwani kuna utajiri mkubwa wa madini.
Ametaja madini yanayopatikana ni dhahabu, nickel, ganeti ya kijani, tormarine ya kijani, manganese ore, marble, gypsum na ulanga (kinywe).
Amesema mkoa wa Lindi una ukanda wa bahari wenye urefu wa kilomita 285 wenye fukwe nzuri, kilimo cha mazao ya bahari, kilimo cha mwani na uvuvi wa samaki.
“Pia kuna utalii wa mapango na magofu ya kale yaliyopo Songomnara Kilwa Masoko,mjusi wa kale (Dinosaur) aliyepatikana Tendeguru, Pori la akiba Selou na Hifadhi ya Taifa ya Nyerere,,” amesema Tellack.
Amesema hata vita vya majimaji vilivyopiganwa kuanzia mwaka 1905 hadi 1907 vilianzia Mkoani Lindi eneo la Nandete Kilwa Kipatimu.
Katibu Tawala wa mkoa huo, RAS Zuwena Omary Jiri amesema maonyesho hayo yatafanyika kwa muda wa siku sita kuanzia Agosti 21 hadi Agosti 26 mwaka 2023.
RAS Zuwena amempongeza mkuu wa mkoa huo Tellak kwa kufanikisha maonyesho hayo yaliyowashirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo wa ndani na nje ya nchi.